Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Ujumbe Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira. Wongofu wa Kiekolojia; Matendo ya kinabii na kuwa mstari wa mbele kubadili mfumo na mtindo wa maisha. Papa Francisko: Ujumbe Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira. Wongofu wa Kiekolojia; Matendo ya kinabii na kuwa mstari wa mbele kubadili mfumo na mtindo wa maisha. 

Siku ya Kuombea Utunzaji wa Mazingira: Wongofu wa Kiekolojia

Huu ni muda wa toba na wongofu wa kieokolojia, ili kuanza mchakato wa kuwa karibu zaidi na mazingira nyumba ya wote, Kitabu cha Mungu kilichofunguliwa wazi mbele ya macho ya binadamu. Ni muda wa kutafakari kuhusu mtindo wa maisha, ili hatimaye, kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha utunzaji wa mazingira; kwa kuwa na teknolojia na nishati rafiki kwa mazingira na unabii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 1 Septemba 2019 amewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Kanisa linaadhimisha Siku ya Kiekumene ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba yote. Familia ya Mungu inahamasishwa na Mama Kanisa kutambua umuhimu na uzito wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kubadili mtindo wa maisha kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi na hatimaye jamii katika ujumla wake, ili mtindo na mfumo huu wa maisha uweze kuwa ni fungamanishi.

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015 kama sehemu ya mchakato endelevu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kumbwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Dunia mama!

Matukio kuhusu utunzaji bora wa mazingira katika kipindi hiki chote, yanapania pamoja na mambo mengine, kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiekolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu,heshima ya binadamu, haki msingi pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anasikitika kusema kwamba, kazi ya uumbaji iliyokuwa nzuri machoni pa Mwenyezi Mungu na kuikabidhi kwa binadamu kama zawadi imeharibiwa kwa uwepo wa dhambi, ubinafsi na uchoyo unaotaka kuinyonya kwa uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta; kilimo cha mashamba makubwa pamoja na ukataji ovyo wa misitu hali ambayo imesababisha kupanda kwa joto duniani pamoja na kuongezeka kiwango cha bahari. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa kwa kutupa ovyo taka za plastiki; mambo yanayotishia usalama wa maisha ya viumbe hai duniani.

Huu ni muda wa toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuanza mchakato wa kuwa karibu zaidi na mazingira nyumba ya wote, Kitabu cha Mungu kilichofunguliwa wazi mbele ya macho ya binadamu. Ni muda wa kutafakari kuhusu mtindo wa maisha, ili hatimaye, kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha utunzaji wa mazingira; kwa kuwa na teknolojia na nishati rafiki kwa mazingira. Hiki ni kipindi cha kufanya matendo ya kinabii kwa kusikiliza na kujibu kilio cha vijana wa kizazi kipya wanaotaka kuona Jumuiya ya Kimataifa ikijizatiti kwa vitendo zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ndio wakati uliokubalika wa kuhakikisha kwamba, sauti na kilio cha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhusu utunzaji bora wa amzingira kinawafikia wakuu wa Serikali na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. Lakini, waamini wawe mstari wa mbele kubadili mfumo na mtindo wa maisha yao kwa kufanya sadaka kubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, linaloadhimisha Siku ya 30 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote, kwa mwaka 2019 anasema, tunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya imani kwa Wakristo inayofumbatwa katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu. Maisha na utume wa Kanisa unamwilishwa katika matukio mbali mbali yanayogusa na kumwambata mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Taalimungu ya kiekolojia inagusa pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kujizatiti katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kutokana na uchafuzi wa mazingira ambao unaendelea kusababisha athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mambo msingi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo imepewa nafasi ya pekee katika Liturujia Takatifu, hususan katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha muhtasari wa utimilifu wa nyakati. Hii ndiyo karamu kuu inayodhihirisha utimilifu wa utukufu wa Ufalme wa Mungu.

Papa: Mazingira
02 September 2019, 11:22