Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kujijengea marafiki kwa mali na utajiri wa ulimwengu huu ili waweze kukaribishwa kwenye maisha na uzima wa milele. Papa Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kujijengea marafiki kwa mali na utajiri wa ulimwengu huu ili waweze kukaribishwa kwenye maisha na uzima wa milele.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Tumieni utajiri wenu kujijengea marafiki wema!

Waamini wakitumia vyema utajiri, wale wanaowasaidia wataweza kuwakaribisha katika makao ya milele. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, mali na utajiri wa dunia vinakuwa ni chombo cha ujenzi wa udugu na mshikamano, ili kuweza kukaribishwa kwenye maisha na uzima wa milele, si tu na Mwenyezi Mungu, bali na wale wote walioshirikiana nao katika kusimamia mali ya dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 22 Septemba 2019, ametafakari kuhusu mfano wa wakili dhalimu na “mwerevu” aliyeshutumiwa kwa kutapanya mali ya bwana wake na alikuwa tayari kuachishwa kazi. Katika muktadha huu, wakili dhalimu, hajutii kosa lake, wala kutaka kusafisha jina lake na wala hakutaka kukatishwa tamaa. Akaamua kutafuta njia ya mkato, ili kujijengea mazingira ya kesho yenye matumaini. Wakili dhalimu anafikiri na kutenda katika ukweli na haki; anatambua na kukiri udhaifu wake; anawaza na kutenda kwa ujasiri mkubwa, huku akiendelea kumwibia tajiri wake kwa mara ya mwisho, ili atakapo ondolewa uwakili wake, waweze kumkaribisha nyumbani kwao.

Wakili dhalimu akajenga urafiki kwa mali ya rushwa; bwana wake akampongeza kwa rushwa; kwa bahati mbaya huu ndio ukweli wa mambo katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yesu ameweka mfano huu mbele ya macho ya wafuasi wake si kwa ajili ya kusifia ukosefu wa uaminifu, bali ule werevu, ujanja na busara aliyotumia yule wakili dhalimu, kiasi hata cha kufanikiwa kuvuka vizingiti vya ugumu wa maisha vilivyokuwa mbele yake. Ujumbe wa Yesu unapatikana mwishoni mwa mfano huu kwa kusema: “Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele”. Katika muktadha huu, hapa watu wengi wanaonekana kuchanganyikiwa na fundisho hili la Kristo Yesu! Lakini ukweli wa mambo si hivyo ulivyo!

Mali ya udhalimu mara nyingi ni fedha, inayoitwa na wengi “sabuni ya roho”, “uchafu wa Shetani, Ibilisi” unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika malimwengu. Mali na utajiri vinaweza kumsukuma mtu kujenga kuta za utengano, dharau na nyanyaso. Kristo Yesu anachukua fursa hii, akiwataka wafuasi wake kuwa na mwelekeo chanya kwa kujitengenezea rafiki kwa mali ya udhalimu. Watumie mali na utajiri wa dunia hii kwa kujenga mahusiano fungamani, kwa sababu utu na heshima ya binadamu inathamani kubwa kuliko vitu. Wanaheri wale ambao wanatumia mali na utajiri wao kujenga mahusiano na urafiki na watu wengine. Utajiri huu unaweza kuwa ni karama na mapaji mbali mbali ambayo mtu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Waamini wakitumia vyema utajiri, wale wanaowasaidia wataweza kuwakaribisha katika makao ya milele.

Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, mali na utajiri wa dunia viwe ni chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mshikamano, ili kuweza kukaribishwa kwenye maisha na uzima wa milele, si tu na Mwenyezi Mungu, bali na wale wote walioshirikiana nao katika kusimamia mali ya ulimwengu huu kwa hekima na busara. Sehemu hii ya Injili iamshe ndani ya waamini swali msingi, Je, baada ya kufukuzwa na mwajiri wao, wanapaswa kufanya kitu gani? Kwa kuzingatia udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, Yesu anapenda kuwahakikishia wafuasi wake kwamba, daima upo muda wa kuweza kurekebisha ubaya wa moyo na dhambi zilizotendeka, kwa kufanya matendo mema. Kwa wale waliowasababishia wenzao, kutokwa machozi, basi wajitahidi, kuwapatia furaha watu wengine, wale waliodokoa na kuiba mali ya jirani zao, sasa wawasaidie maskini na wahitaji zaidi.

Kwa kufikiri na kutenda hivi, waamini wataweza kusifiwa na kupongezwa na Mwenyezi Mungu kwa vile wametenda kwa busara. Hii ni busara ya wale wanaojitambua kuwa ni watoto wateule wa Mungu, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria, awasaidie kuwa na busara ili waweze kupata mafanikio si kwa kumezwa na malimwengu, bali kwa kupata maisha na uzima wa milele, ili wakati wa hukumu ya mwisho, maskini na wahitaji waliowasaidia katika shida na magumu ya maisha yao, waweze kushuhudia kwamba, katika maisha yao, wamemwona na kumhudumia Kristo Yesu!

Papa: Mali na Busara

 

22 September 2019, 15:07