Papa Francisko anawataka wadau mbali mbali katika huduma kwa wafungwa magerezani kuwa ni: madaraja kati ya magereza na jamii; vyombo vya Injili na mashuhuda wa ujasiri na matumaini. Papa Francisko anawataka wadau mbali mbali katika huduma kwa wafungwa magerezani kuwa ni: madaraja kati ya magereza na jamii; vyombo vya Injili na mashuhuda wa ujasiri na matumaini. 

Utume kwa wafungwa: Madaraja, Injili, Ujasiri & Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu utume wa Kanisa kwa wafungwa magerezani amekazia kwa namna ya pekee kabisa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili sanjari na kuwa na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” imeadhimishwa na Mama Kanisa, Jumamosi, tarehe 15 Septemba 2019. Hii imekuwa ni fursa kwa viongozi wa Jeshi la Polisi nchini Italia, wanaosimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao pamoja na Jeshi la Magereza linalopaswa kulinda na kudumisha haki, amani na utulivu, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mkutano huu umewajumuisha pia washauri na wahudumu wa maisha ya kiroho kwa wafungwa magerezani. Mkutano huu wa sala kwa mwaka 2019 umeongozwa na kauli mbiu “Wajenzi wa haki na wajumbe wa amani”. Hizi ni juhudi zinazojikita katika maboresho ya magereza, ili yaweze kuwa na hadhi ya kibinadamu na wala si nyumba ya mateso na watu kukata tamaa ya maisha. Zaidi ya watu 11, 000 elfu kutoka katika magereza 190 ya Italia wameshiriki.

Hii imekuwa ni nafasi ya kutafakari Fumbo la Msalaba katika maisha ya wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, Msalaba ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu ameshiriki sala na shuhuda zilizotolewa na wadau mbali mbali zinazolenga kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafunga magerezani. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani,  kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili sanjari na kuwa na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu anawapongeza Askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii.

Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasi wasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka Askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapaswa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi yao.

Kufurika kwa wafungwa magerezani nchini Italia ni kati ya changamoto changamani kwa wakati huu, hali ambayo inachangia pia kudhohofisha maisha ya Askari magereza, kiasi hata cha kukosa imani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wafanyakazi na wafungwa wanaishi maisha yenye hadhi na utu wa kibinadamu, vinginevyo magereza yatageuka kuwa nyumba cha chuki na uhasama badala ya kuwa ni mahali pa kurekebisha tabia na mwenendo wa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wa huduma mbali mbali magerezani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza. Wanapokumbana na umaskini wa wafungwa magerezani, watambue kwamba, hawa ni watu wanaohitaji kwanza kabisa msamaha na huruma ya Mungu. Wawe na ujasiri wa kusamehe kama mashuhuda waaminifu wa msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wawe ni watu wa faraja na kamwe wasimwache mtu hata mmoja kutumbukia katika upweke hasi, unaoweza kusababisha watu kumezwa na utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi magerezani kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuokoa maisha ya wafungwa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha ya Zakayo Mtoza ushuru. Wawe na ujasiri unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na kamwe wasiruhusu kugubikwa na giza totoro katika maisha na nyoyo zao. Katika shida na mahangaiko ya ndani, wamkimbilie Kristo Yesu chini ya Msalaba na kumwelezea mahangaiko yao katika ukweli na uwazi. Msalaba ni chemchemi ya ujasiri, amani na utulivu wa ndani. Kamwe wasikubali kuzima utambi wa matumaini katika maisha yao. Hii ni dhamana na wajibu wa watu wote. Haki, matumaini, upatanisho pamoja na mchakato wa wafungwa kurejea tena katika maisha ya kawaida ndani ya jamii ni mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana. Wadau katika huduma ya wafungwa  magerezani wasikubali kujifungia katika gereza lisilokuwa na matumaini katika maisha. Kila mtu anayo haki ya matumaini  na haki ya kuanza kuandika tena ukurasa wa maisha yake kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Papa: Magereza

 

 

15 September 2019, 14:03