Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu. Tarehe 14 Mei 2020 kutafanyika mkutano kuhusu mabadiliko ya mfumo wa elimu kimataifa Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu. Tarehe 14 Mei 2020 kutafanyika mkutano kuhusu mabadiliko ya mfumo wa elimu kimataifa 

Papa Francisko: Ushirikiano wa kimataifa katika sekta elimu makini

Papa Francisko anatanabaisha athari za mwendokasi katika mchakato wa elimu; umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu; matumizi sahihi ya rasilimali watu sanjari na umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma makini katika jamii. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu kujikita katika mchakato utakaoleta mabadiliko ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake unaounga mkono jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu, kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, tukio litakaloadhimishwa hapo tarehe 14 Mei 2020 anatanabaisha athari za mwendokasi katika mchakato wa elimu; umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu; matumizi sahihi ya rasilimali watu sanjari na umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma makini katika jamii. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote” anawaalika waamini pamoja watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato utakaoleta mabadiliko ulimwenguni. Ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, watu wanatumia karama na mapaji yao katika kubadili uso wa nchi, jambo linalohitaji elimu makini inayokita mizizi yake katika mshikamano ili kujenga jamii yenye ukarimu zaidi!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaunga mkono tukio la kimataifa litakaloadhimishwa hapo tarehe 14 Mei 2020, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya mfumo wa elimu kimataifa”. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti, kwa kujikita katika elimu fungamanishi inayowataka vijana kuwa wasikivu, wajenzi wa majadiliano pamoja na kuongeza jitihada za kufahamiana, changamoto mamboleo, ili kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu. Baba Mtakatifu anasema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu hali ambayo imesababisha hata kinzani na mabadiliko si tu katika masuala ya kitamaduni bali pia kuhusiana na elimu ya binadamu, kwa kuunda lugha mpya ambayo inawatenga na kudhohofisha dhana ya elimu ya jadi. Leo hii kuna kile kinachoitwa mchakato wa mwendokasi wa elimu unaofumbatwa katika kasi kubwa ya teknolojia na matumizi ya komputa yanayokinzana na kasi ndogo ya mabadiliko ya kibaiolojia.

Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika elimu unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote kadiri ya dhamana zao wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi kwa ajili ya ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa elimu. Kuna umuhimu wa kuanzisha kijiji cha elimu kabla ya kuanza kutoa elimu, kwa kuandaa mazingira ya udugu wa kibinadamu pamoja na kuondokana na ubaguzi. Kijiji cha elimu anasema Baba Mtakatifu ni jukwaa ambalo inakuwa rahisi kuweza kufikia muafaka wa elimu fungamani inayomheshimu binadamu na kuunganisha masomo na hali halisi ya maisha kati ya wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, michezo, siasa, biashara na wenyeji wote wa nyumba ya wote. Ili kuweza kufikia ujenzi wa kijiji cha elimu, kwanza kabisa binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kukazia mifumo rasmi na isiyo rasmi ya elimu, ili kuwa na mwelekeo wa pamoja kuhusu: elimu ya binadamu, uchumi, siasa, ukuaji na maendeleo fungamani.

Katika mchakato wa ekolojia fungamani, utu na heshima ya kila kiumbe inapaswa kuzingatiwa kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Hatua ya pili anasema Baba Mtakatifu ni ujasiri, uwajibikaji na ubunifu pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali watu. Yote haya yatasaidia kuwaunda watu ambao wako tayari kusikiliza, kujadili pamoja na kutafakari na wengine; wakiwa na uwezo wa kujenga na kudumisha mafungamano ya kifamilia na kati ya kizazi kimoja na kingine; vyama vya kiraia na hatimaye, kuweza kuunda ubinadamu mpya! Hatua ya tatu anasema Baba Mtakatifu ni umuhimu wa kuwaundia watu mazingira ya kujisadaka kwa ajili ya huduma makini katika jamii. Hii ni huduma inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini ili kujenga mshikamano; kuna furaha zaidi kutoa kuliko kupokea. Kumbe, kuna umuhimu wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: malengo na mbinu zitakazosaidia utekelezaji wa utume wa elimu katika jamii.

Baba Mtakatifu anatanguliza shukrani zake za dhati, huku akiwaalika wajumbe wote katika tukio hili muhimu linalopania kuanzisha mchakato wa ushirikiano wa kimataifa katika elimu. Mwito huu pia anautoa kwa viongozi na wadau katika sekta ya elimu, waliopewa dhamana ya kutoa elimu na malezi kwa vijana wa kizazi kipya, kwamba, watakubali na kuitikia mwaliko wake. Baba Mtakatifu anawataka vijana kushiriki kikamilifu katika mkutano huu, kama njia ya kuchangia ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi. Mkutano huu utafanyika tarehe 14 Mei 2020 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI mjini Vatican. Lakini semina zitaendeshwa kwenye vituo mbali mbali vilivyoko mjini Roma. Baba Mtakatifu anawaalika wote kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa mfumo mpya wa elimu, kwa ajili ya matumaini kwa siku za usoni, kwa kujenga udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika mshikamano kama kielelezo cha mpango wa Mungu kwa binadamu!

Papa: Elimu

 

 

12 September 2019, 16:40