Papa Francisko: Jengeni hoja katika ukweli; dumisheni mafungamano ya kijamii; kwa kuheshimu watu, kwa kujitahidi daima kusema ukweli na kuondokana na kiburi! Papa Francisko: Jengeni hoja katika ukweli; dumisheni mafungamano ya kijamii; kwa kuheshimu watu, kwa kujitahidi daima kusema ukweli na kuondokana na kiburi! 

Tasnia ya habari: Wajumbe wa: haki, amani na mshikamano!

Papa waandishi wa habari wawe ni mashuhuda wa dhamiri nyofu katika muktadha wa mawasiliano ya jamii kwa kupambanua wema na ubaya; mambo msingi katika maisha ya binadamu; kwa kujenga hoja katika ukweli, sanjari na ujenzi wa mafungamano ya kijamii; daima wakijitahidi kusema ukweli kwa gharama yoyote ile; kwa kuwaheshimu watu sanjari na kuondokana na kiburi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Wachapaji Wakatoliki Italia, UCSI, ulianzishwa rasmi tarehe 3 Mei 1959 na kujikita katika mambo makuu matatu: ukweli, haki na udugu. Umoja huu unaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake. Katika muktadha huu, wajumbe wa UCSI, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya wito wa maisha ya kijumuiya. Umoja huu unawaunganisha wataalam na viongozi Kanisa katika tasnia ya mawasiliano kwa ajili ya huduma ya Injili pamoja na kueneza mafundisho ya Kanisa. Utume huu hauna budi kuendelezwa kwa kuzingatia: imani, historia na matukio ya watu pamoja na kuzingatia utu wa binadamu, kanuni, sheria na taratibu za mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa Jarida la “Desk, Wavuti, Shule ya Uandishi wa habari ya Assisi pamoja na shughuli mbali mbali zinazoendeshwa na Umoja huu ni ushuhuda tosha kabisa kwamba, upo kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawataka wawe ni mashuhuda wa dhamiri nyofu katika muktadha wa mawasiliano ya jamii kwa kuhakikisha kwamba, wanasaidia waandishi wa habari kupambanua wema na ubaya; mambo msingi katika maisha ya binadamu; kwa kujenga hoja katika ukweli, sanjari na ujenzi wa mafungamano ya kijamii; daima wakijitahidi kusema ukweli kwa gharama yoyote ile; kwa kuwaheshimu watu sanjari na kuondokana na kiburi. Waandishi wa habari wanapaswa kutangaza na kushuhudia ukweli unaobubujika katika Maandiko Matakatifu, “ndiyo” iwe ni “ndiyo” na “siyo” iwe ni “siyo” kwa kuwa yazidiyo hapo anasema Baba Mtakatifu yatoka kwa yule Mwovu. Mawasiliano yanahitaji maeneno ya kweli, jambo ambalo ni uwajibikaji mkubwa, kwa ajili ya kutangaza mambo mazito yanayoendelea kujiri ulimwenguni. Matokeo yake, waandishi wa habari wanaweza kusaidia kutengeneza mianya ya uhuru au kuwatumbukiza watu utumwani; kwa kuwajengea uwezo au kuwa watumwa wa viongozi na wenye madaraka.

Wanahabari wanapaswa kuwa ni wajumbe na mashuhuda wa: amani, haki, mshikamano unaofumbatwa katika ushuhuda makini, ili kusaidia ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na mshikamano. Baba Mtakatifu anasema, katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii, mwandishi wa habari anayo dhamana ya kuhakiki vyanzo vyake vya habari; kuweka habari katika mazingira yake; kuitafasiri na kuipatia uzito unaostahili. Mwenendo wa habari kwa wakati huu ni ushindani wa mwenye nguvu mpishe na wala si tena utu, heshima na haki msingi za binadamu. Matokeo yake ni umati mkubwa wa watu kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni jambo la msingi kuwa ni sauti ya wanyonge; kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii; jumuiya za watu pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wajumbe hawa kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Huu ni waraka wa kiekolojia na kijamii unaotoa dira na mfumo mpya wa maendeleo fungamani ya binadamu, ili kujenga utamaduni wa ushirikiano na mshikamano; kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu. Umoja wa Wachapaji Wakatoliki Italia, UCSI, kwa unyenyekevu unapaswa kupambua mapungufu na changamoto katika ulimwengu mamboleo, tayari kufanya rejea katika utume wake, bila woga wala makunyanzi ili kufanya mageuzi kwa ajili ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wanaalikwa kuendeleza ushirikiano na Mapadre wanaoandika makala kwenye “Civiltà Cattolica” Jarida linalochapishwa na Wayesuiti. Itakumbukwa kwamba, tarehe 12 Juni 2010, Mama Kanisa alimtangaza mtumishi wa Mungu Manuel Lozano Garrido kuwa Mwenyeheri. Huyu ni mwamini mlei na mwandishi wa habari, aliyeishi wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania. Huu ni wakati ambapo, kujitambulisha kama Mkristo kulihatarisha maisha ya watu.

Akabahatika kuishi miaka 28, licha ya kushambuliwa na ugonjwa uliomfanya kiwete, lakini bado, aliipenda taaluma yake. Akawataka watu kulipia gharama ya ukweli, watafute chakula cha habari ambacho ni safi kabisa, kwa kuweka chumvi ili kukoleza maisha; chachu ya maisha ya uzima wa milele, hatimaye, kufurahia maisha katika ukweli na matumaini; mfano bora wa kuigwa!

Papa: Umoja wa Wachapaji

 

 

 

 

23 September 2019, 16:57