Tafuta

Vatican News
Papa Francisko. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kujikita katika: Uaminifu, Uwajibikaji na Ujasiri. Papa Francisko. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kujikita katika: Uaminifu, Uwajibikaji na Ujasiri.  (ANSA)

Papa Francisko: Ujumbe Mkutano Mkuu wa 74 Baraza Kuu la UN

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa anasema, bado kuna nafasi ya kuweza kufanya mabadiliko kwa kujikita katika uaminifu, uwajibikaji, akili na busara kwa ajili ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Uchafuzi wa mazingira ni changamoto ya kanuni maadili na utu wema inayofumbatwa katika usawa na haki jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya Video kwenda kwa wajumbe wa Mkutano wa 74 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa uliofunguliwa rasmi, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2019, amekazia kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015, unaozitaka nchi tajiri zaidi duniani kuonesha mshikamano wa dhati katika mchakato wa mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi ili kulinda mazingira nyumba ya wote. Bado kuna nafasi ya kuweza kufanya mabadiliko makubwa, kwa kujikita katika uaminifu, uwajibikaji, akili na busara kwa ajili ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Uchafuzi wa mazingira ni changamoto ya kanuni maadili na utu wema inayofumbatwa katika usawa na haki jamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video, anawashukuru viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, kwa kukutana ili kuweza kujadili changamoto hii inayopaswa kushughulikiwa kwa namna ya pekee kwa kujikita katika: uaminifu, uwajibikaji na ujasiri. Kwa njia ya Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015, Jumuiya ya Kimataifa ilianza kugundua umuhimu wa kushikamana na kujibu kipeo cha athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, mazingira nyumba ya wote inajengwa na wote. Imekwisha yoyoma miaka minne tangu Mkataba wa Paris ulipopitishwa, lakini ahadi zilizotolewa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, bado zimeendelea kuwa “dhaifu sana”, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni vigumu kufikia malengo yaliyobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu anasema, haya ni malengo ambayo yanapaswa kutekelezwa na Serikali mbali mbali pamoja na jamii katika ujumla wake. Hapa kuna haja ya kuonesha utashi wa kisiasa kwa kutenga rasilimali watu, fedha na teknolojia ili kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ndio waathirika wakuu. Muda unaendelea kuyoyoma kwa kasi kubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Bado ipo fursa ya kuweza kubadili mwelekeo huu kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanakuwa na leo na kesho yenye maisha bora zaidi. Hii ni kwa sababu ya mbeleni yako mikononi mwa vijana.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ingawa katika historia zama za viwanda zinaonekana kuwa ni zama ambazo hazikuwajibika kuhusiana na suala la mazingira, hata hivyo ipo kila sababu ya kuleta matumaini kuwa karne ya ishirini na moja binadamu atakumbukwa kwa majukumu makubwa aliyoyafanya kuhusiana na mazingira. Uaminifu, uwajibikaji, ujasiri na busara anasema Baba Mtakatifu, inaweza kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo fungamani, ambayo ni maridhawa, yenye utu, kijamii na timilifu, kwa kukita uchumi kwa ajili ya huduma ya binadamu, katika mchakato wa ujenzi wa amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Uchafuzi wa mazingira ni changamoto ya kanuni maadili na utu wema inayofumbatwa katika usawa na haki jamii.

Uchafuzi wa mazingira ni mambo ambayo yanagusa utu, maadili na masuala jamii yanayofanywa na binadamu kila kukicha. Huu ni mwaliko wa kutaza upya mfumo wa ulaji na uzalishaji; mchakato wa elimu na utambuzi ili mambo haya yaende sanjari na utu wa mwanadamu. Changamoto kubwa inayoikabili Jumuiya ya Kimataifa ni kuhusu “Ustaarabu” dhidi ya mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kuwa na suluhu mbali mbali zinazoweza kutekelezwa katika ngazi ya mtu binafsi; ikiwa kama watu watazingatia mtindo wa maisha binafsi na kijamii inayofumbata na kuambata misingi ya uaminifu, uwajibikaji pamoja na ujasiri. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake kwa njia ya video anasema, anapenda kukazia mambo makuu matatu: uaminifu, uwajibikaji pamoja na ujasiri kama mwongozo wa shughuli zao katika mkutano huu.

Papa: Ujumbe UN
24 September 2019, 16:00