Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2019. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2019. 

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO SIKU YA WAKIMBIZI & WAHAMIAJI 2019

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Hili si suala la wahamiaji na wakimbizi peke yake, bali linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican

Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa Jumapili,  tarehe 29 Septemba, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Si Wahamiaji peke yao”. Baba Mtakatifu  Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Hili si suala la wahamiaji na wakimbizi peke yake, bali linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kutowatenga watu kwa sababu ya maamuzi mbele, kwani kwa kufanya hivi, ni kuendeleza ukatili dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawataka wahamiaji na watu wenye mashaka wawe na imani, matumaini na mapendo katika kukabiliana na changamoto za vurugu na migogoro ya kiuchumi na kijamii inayoendelea kusambalatisha hali ya utu na heshima ya binadamu ulimwenguni.

Katika ujumbe wake Baba Mtakatifu, amefafanua sehemu ya Maandiko Matakatifu, Injili ya Mtakatifu Luka sura ya 14:27 inayosema “Jipeni moyo, ni mimi, msiogope.” Ameeleza kuwa, walengwa wa siku ya uhamiaji siyo tu wakimbizi bali ni kila mtu aliye na fikra za kumwogopa asiyemfahamu, aliye mgeni, aliyesetwa na jamii anayebisha hodi akihitaji ulinzi, usalama na kuwa na maisha bora ya baadaye. Hofu hii mwanzoni huonekana kuwa sahihi kwa sababu ya kutokufahamiana, lakini baadaye hugeuka kuwa tatizo linajikita katika ubaguzi unaomfanya mtu kutokuwa mvumilivu na kujifungia ndani mwake. Katika mazingira hayo, hofu huzuia ile hamu na uwezo wa kukutana na mtu mwingine na hata kukutana na Bwana wetu Yesu Kristo. Aidha, Baba Mtakatifu akieleza sehemu ya Andiko linalosema; “maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? (Mt 5:46) ” amefundisha kuwa, siku ya wahamiaji duniani ni siku ya kutafakari juu ya upendo na hapa upendo unaosisitizwa ni pale jamii inapowasaidia wahitaji na hasa wale wasioweza kurudisha hata shukrani. Maendeleo yatapimwa kwa kuwajali wale wanaobisha hodi.

Baba Mtakatifu akitumia mfano wa huruma ya msamaria mwema (Lk 10:33) amesisitiza juu ya heshima ya utu inayoonekana hata kwa wageni. Huruma ni mvuto wa ndani kabisa unaomfanya mtu kuwa jirani kwa wote walio katika mahangaiko kama Kristo alivyofundisha kuwatambua wanaoteseka na kuwasaidia. Kuwa na huruma ni kuwa mkarimu na muwazi na kujitoa sadaka kwa wengine. Baba Mtakatifu ameendelea kutoa mafundisho juu ya kutowabagua wengine katika maslahi ya pamoja. Amesema, ulimwengu wa leo unakumbwa na changamoto hiyo ya nchi tajiri kuendelea kuzinyonya nchi maskini katika soko huria.  Silaha zinatengenezwa na kupelekwa kwa nchi zenye migogoro na wale wanaolipa kodi si matajiri bali ni wale maskini wasio na namna ya kufanya. Hapo ndipo Kanisa linasimama kidete kumsaidia mnyonge na kupinga maendeleo yanayomfanya tajiri kuwa tajiri zaidi na maskini kugandamizwa zaidi.

Siku ya wahamiaji na wakimbizi ulimwenguni ni siku ya kumwinua mtu wa hali ya chini, yule anayeelemewa na mzigo, yule aliyekata tamaa na ni siku ya kupinga mitazamo ya kiulimwengu inayomtazama maskini kuwa ni chombo cha kukuzia uchumi bila kuangalia utu na kuguswa na mahangaiko yake. Hiyo ndiyo maana ya utumishi uliotukuka unaoelezwa na mwinjili Marko kuwa “anayetaka kuwa mkubwa kwenu atakuwa mtumishi wenu” (10:43-44).    Utume wa Kanisa unaelekezwa katika ukamilifu wa mtu na kwa mataifa yote. Mungu anataka watu wote wapate zawadi ya ukamilifu wa maisha yao katika shughuli zote za kisiasa, za kimkakati, za kichungaji, mtu ndiye awe kiini cha utume. Hivyo maendeleo yaanze na mtu mwenyewe na kuenea hadi kuwafikia watu wote.  Akielezea juu umuhimu wa maisha kutoka Injili ya Mtakatifu Yohane inayosema “Mimi nilikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (10:10) Baba Mtakatifu amesema, Utume ujikite katika ujenzi wa jiji la Mungu na jiji la wanadamu lenye kuwapa hifadhi wanaohangaika na uhamiaji wa kidigitali.

Kila mtu anapaswa kuwa ndugu kwa wengine katika kukaribishana, kuheshimiana, na kupendana ili kuweza kujenga jamii ya kidemokrasia na Jumuiya Injilifu. Katika kuhitimisha ujumbe wake Baba Mtakatifu Francisko amependekeza mbinu zitakazosaidia kutatua changamoto hizo kwa matendo manne tu yaani; kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Matendo hayo hayawahusu tu wahamiaji na wakimbizi bali yanalihusu taifa lote la Mungu. Kwa kufanya hivyo, ulimwengu utakombolewa na Bwana kutoka katika kujitenga, sintofahamu na utamaduni wa kutojali.  

Papa: Wahamiaji 2019

 

 

 

25 September 2019, 17:48