Tafuta

Papa Francisko, tarehe 1 Oktoba 2019, Mwanzo wa Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Mkesha wa Sala: Kuamasisha ari na mwamko mpya wa kimisionari duniani. Papa Francisko, tarehe 1 Oktoba 2019, Mwanzo wa Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Mkesha wa Sala: Kuamasisha ari na mwamko mpya wa kimisionari duniani. 

Papa: Ufunguzi wa Mpango Mkakati Mwezi Oktoba 2019

Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 yanafunguliwa rasmi na Papa kwa njia ya Masifu ya Jioni, tarehe 1 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Tarehe 7 Oktoba 2019 kutakuwa na Rozari ya Kimisionari Kimataifa na kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 20 Oktoba 2019, kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Papa Francisko. Utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwezi Oktoba 2019, umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa mwaka huu 2019, Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Papa Benedikto XV katika Waraka huu, alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani mihimili ya uinjilishaji! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”.  Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 yanafunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, kwa njia ya Masifu ya Jioni, tarehe 1 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, tarehe 7 Oktoba 2019 kutakuwa na Rozari ya Kimisionari Kimataifa, itakayotangazwa moja kwa moja kutoka kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma na kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 20 Oktoba 2019, kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu linawahamasisha waamini kutoka katika Majimbo mbali mbali kufanya hija katika ngazi za kiparokia, kijimbo na kitaifa ili kukuza na kuimarisha ari na mwamko wa kimisionari kati ya watu wa Mungu. Iwe ni fursa ya kusali, kutafakari na kusikiliza shuhuda za kimisionari kutoka katika mihimili ya uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Huu ni muda muafaka wa Injili kutangazwa, Sakramenti za Kanisa kuadhimishwa na Wakristo kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuendelea kujikita katika Tafakari ya Neno la Mungu. Baraza pia linaendelea kuandaa fursa makini za malezi na majiundo ya kimisionari na kisomi ili kushirikishana sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.

Papa: Masifu
30 September 2019, 11:43