Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 12 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu 186 wa Shirika la Mtakatifu Augustino Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 12 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu 186 wa Shirika la Mtakatifu Augustino  (Vatican Media)

Wosia wa Papa Francisko kwa Shirika la Mt. Augustino, OSA

Shirika la Mtakatifu Augustino limeachiwa urithi na utajiri mkubwa unaosimikwa katika maisha ya sala na ya kijumuiya; utambulisho wao katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto ya kuendelea kuwa waaminifu kwa karama na kamwe wasiingiwe na kishawishi cha kutaka kukata mizizi na kujitenga na karama hii, kwani hapo watakuwa wanajitafutia maafa makubwa katika utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Mtakatifu Augustino, OSA, Septemba 2019 lina adhimisha mkutano wake 186 tangu lilipoanzishwa. Hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Shirika ndani ya Kanisa na katika ulimwengu. Mkutano huu unawajumuisha wanashirika 80 kutoka katika nchi 52 wanakotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Alhamisi, tarehe 12 Septemba 2019, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewapongeza kwa utumishi unaofumbatwa katika furaha na unyenyekevu  wa Kiinjili; umuhimu wa kujikita zaidi katika mizizi ya uaminifu wa karama na maisha ya Shirika; ufukara wa Kiinjili, Sala, toba na wongofu wa ndani; nadhiri ya unyenyekevu pamoja na kuendeleza mchakato wa uinjilishaji wa awali.

Baba Mtakatifu ameungana na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino, OSA. kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ushuhuda wa imani uliotolewa na Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, wakati huu wanapoadhimisha “Mwaka Karama ya Shirika”. Familia ya Mtakatifu Augustino imeendelea kujisadaka katika huduma na utumishi unaofumbatwa katika furaha na unyenyekevu unaobubujika kutoka katika kiini cha Injili. Mtakatifu Augustino ni mtu mashuhuri sana ndani ya Kanisa kutokana na mafundisho, wito na utume wake, uliomwezesha kuwa wazi na mkweli kwa watu wa Mungu na ukawa ni kikolezo cha ujenzi wa jumuiya, kiasi kwamba, hata alipoitupa mkono dunia, aliacha urithi mkubwa wa monasteri kwa ajili ya watawa wa kike na kiume.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Shirika la Mtakatifu Augustino limeachiwa urithi na utajiri mkubwa unaosimikwa katika maisha ya sala na ya kijumuiya; utambulisho wao katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto ya kuzama zaidi katika mizizi kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa karama ya shirika lao na kamwe wasiingiwe na kishawishi cha kutaka kukata mizizi na kujitenga na karama hii, kwani hapo watakuwa wanajitafutia maafa makubwa katika maisha, utume na historia yao kama Shirika. Hii ni historia inayofumbatwa katika ushuhuda wa Kikristo, fadhila ya unyenyekevu na ambayo inamwilishwa katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa watu. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa ufukara wa Kiinjili kama utambulisho wa utume wao. Wanashirika wanapaswa kuwa makini ili kusikiliza ujumbe wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao.

Unyenyekevu wa Kiinjili ni ufunguo wa ukuaji na ukomavu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mchakato wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu anawapongeza katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa Shirika kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika unyenyekevu wa Kiinjili, unaowafanya kuwa wazi mbele ya Mungu na watu wake. Unyenyekevu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu analitaka Shirika la Mtakatifu Augustino kuendeleza mchakato wa uinjilishaji wa awali, kwa kuwa waaminifu kwa Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu ameungana na wamisionari hawa kuwakumbuka na kuwaombea wamisionari wote walioyamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni changamoto kwa wamisionari kuendelea kutembea bega kwa bega na Kristo Yesu katika maisha na utume wao, kwani kwa hakika Kristo anaishi!

Papa: Mt. Augustino
12 September 2019, 15:54