Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Mchakato wa Uinjilishaji unafumbatwa katika huduma kwa maskini, utangazaji na ushuhuda wa Neno la Mungu pamoja na uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Papa Francisko: Mchakato wa Uinjilishaji unafumbatwa katika huduma kwa maskini, utangazaji na ushuhuda wa Neno la Mungu pamoja na uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.  (AFP or licensors)

Papa: Safari ya Injili Ulimwenguni: Ushuhuda na Huduma makini!

Huu ni ushuhuda amini wa watoto wa Mungu, wanaojisadaka na kujiaminisha mikononi mwa Mungu, kwa kusamehe wale wote wanaowatendea jeuri, kama ushuhuda wa imani. Papa anasema, leo hii kuna idadi kubwa ya mashuhuda wengi wa imani pengine kuliko hata ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Damu ya mashuhuda ni mbegu ya Ukristo; chemchemi ya ukuaji wa Neno la Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Septemba, 2019 ameendeleza Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume. Hii ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana mchango wa Neno la Mungu na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji: Wahusika wakuu katika mchakato huu ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu lina mwendo mkali, linapyaisha na kunyeeshea kila mahali linapopita. Mwenyezi Mungu ametumia maneno ya kibinadamu kwa njia ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayeyatia nguvu na kuyatakasa na hatimaye, kuyawezesha kuwa ni chemchemi ya maisha mapya! Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Kitabu cha Matendo ya Mitume, waamini wanapata fursa ya kutafakari kuhusu uhalisia wa safari ya Injili ulimwenguni, inayosimikwa katika maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, mwanzo wa changamoto na matatizo katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii ni Jumuiya ambayo iliwapokea na kuwakarimu si tu Waebrania bali hata Wayahudi wa Kiyunani. Ni watu waliokuwa makini sana katika kufuata mapokeo, katika muktadha huu, kunaanza kuibuka manung’uniko na majungu, hatari sana kwa umoja na mafungamano ya Kikanisa. Changamoto kubwa iliyojitokeza ni kuweka uwiano mzuri kati ya huduma na ushuhuda wa imani tendaji. Katika muktadha huu, Mitume wa Yesu wakaanisha mchakato wa kufanya mang’amuzi na upembuzi yakinifu ili kuangalia vyema matatizo na kwa pamoja waweze kupata suluhu ya kudumu. Kwa pamoja wakaafikiana kugawana madaraka, ili kusaidia mchakato wa ukuaji na ukomavu wa Jumuiya ya Wakristo wa mwanzo, ili Mitume waendelee kutangaza Injili na maskini pamoja na wajane wapate huduma. Mitume wakajikita katika kusali, kutangaza na kushuhudia Injili na wakachaguliwa Mashemasi saba kwa ajili ya huduma mezani. Mashemasi ni kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mashemasi ni walinzi wa huduma ya Kanisa, ili kuweka uwiano mzuri kati ya kutangaza Injili na huduma ya upendo kwa maskini, inayolisaidia Kanisa kukua na kukomaa.

Stefano mtu aliyejaa Roho Mtakatifu pamoja na Filipo ni kati ya Mashemasi waliopewa uzito wa juu katika orodha nzima ya Mashemasi saba. Stefano alikua amejaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Mahubiri yake yaliwabwaga wapinzani wake, kiasi cha kumtafutia “zengwe” ili kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia. Wanafanikiwa kuwapata mashuhuda wa uongo, “Saratani anayotumia Shetani, Ibilisi” kwa ajili ya kuchafua majina ya watu na sifa yao njema na kwa kufanya hivyo, wanataka pia kuharibu Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kuchanganya mafao binafsi na mapungufu yao maisha. Mtindo wa mashitaka dhidi ya Stefano unafanana sana na ule wa Kristo Yesu. Stefano alikamatwa, akapelekwa mbele ya baraza na kumtuhumu kwa kusema maneno ya kashfa dhidi ya Hekalu. Stefano katika hotuba yake ya kujitetea, anawasaidia wasikilizaji wake kusoma tena historia ya ukombozi inayokita mizizi yake kwa Kristo Yesu, kama njia ya kujilinda.

Hii ndiyo Pasaka ya Kristo yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, kiini cha historia nzima ya wokovu. Stefano kwa ushupavu mkubwa anakemea unafiki ulioneshwa tangu mwanzo kwa “kuwafyekelea mbali Manabii” hadi kwa Kristo Yesu mwenyewe. Stefano Shahidi anatangaza na kushuhudia Ukweli, kiasi cha wasikilizaji wake kuchomwa mioyo na kuanza kumsagia meno. Stefano anahukumiwa kifo na kupondwa kwa mawe hadi kukata roho, lakini kabla ya kifo, alisali na kuomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu”. Akaitupa mkono dunia kama mwana wa Mungu, huku akiwasamehe watesi wake kwa kusema “Bwana usiwahesabie dhambi hii! Huu ni ushuhuda amini wa watoto wa Mungu, wanaojisadaka na kujiaminisha mikononi mwa Mungu, kwa kusamehe wale wote wanaowatendea jeuri, kama ushuhuda wa imani. Baba Mtakatifu anasema, leo hii kuna idadi kubwa ya mashuhuda wa imani na wafiadini, pengine kuliko hata ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo.

Damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo; chemchemi ya ukuaji wa Neno la Mungu. Hawa ni watu walioosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo na sasa wameshinda. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujifunza kutoka kwa mashuhuda na wafiadini, ili kuishi kikamilifu, kwa kuwa waaminifu wa Injili ya Kristo kila siku ya maisha yao pamoja na kuendelea kuimarishwa na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao.

Papa: Katekesi

 

 

25 September 2019, 17:22