Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Septemba 2019 ametembelea na kusali na Jumuiya ya  "Nuovi Orizzonti" iliyoko mjini Frosinone Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Septemba 2019 ametembelea na kusali na Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti" iliyoko mjini Frosinone  (Vatican Media)

Papa Francisko: Maisha mapya yanajengwa kwa sala na kazi!

Papa Francisko: Ujenzi wa Hekalu ya Mungu; mchakato wa ujenzi wa maisha mapya yanayosimikwa katika neema ya Mungu; nguvu ya Fumbo la Msalaba katika maisha ya waamini na umuhimu wa Sala na Kazi katika upyaisho wa maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu anasema, watu wa Mungu walipata changamoto kubwa kujenga tena Hekalu lililokuwa limebomolewa kwa miaka mingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” iliyoanzishwa na Chiara Amirante kwa mwaka 2019, inaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Hii imekuwa ni historia yenye matatizo, changamoto na fursa za kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo! Ni Jumuiya ambayo imekuwa ni chemchemi ya matumaini mapya kwa wasichana wanaojikuta wametumbukizwa kwenye: umaskini, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti" kuendeleza kumbu kumbu ya huruma na wema wa Mungu katika maisha yao, kama fursa ya kukutana na Mungu. Huyu ndiye Mungu ambaye amewasindikiza, akawawezesha kukua na kukomaa. Mwenyezi Mungu amewakuta katika jangwa tupu litishalo, akawazunguka, akawatunza na kuwahifadhi kama mboni ya jicho!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 24 Septemba 2019 ametembelea Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaohudhuria mkutano wao wa mwaka huko mjini Frosinone, nje kidogo ya mji wa Roma pamoja na wanachama na wasichana wanaohudumiwa na Jumuiya hii. Jumuiya hii ina zaidi ya wanachama 700, 000 wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza upendo na huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Wanachama hawa wamekuwa kweli ni Injili ya matumaini kwa wasichana wengi waliokuwa wamekata tamaa, wakajikuta wametumbukizwa kwenye utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake yaliyojikita katika Liturujia ya Neno la Mungu, amekazia kwa namna ya pekee kuhusu ujenzi wa Hekalu la Mungu; mchakato wa ujenzi wa maisha mapya yanayosimikwa katika neema ya Mungu; nguvu ya Fumbo la Msalaba katika maisha ya waamini na umuhimu wa Sala na Kazi katika upyaisho wa maisha ya mwamini.

Baba Mtakatifu anasema, watu wa Mungu walipata changamoto kubwa kujenga tena Hekalu lililokuwa limebomolewa kwa miaka mingi. Mfalme Dario akataka kodi inayotolewa kwa Mfalme isaidie  ujenzi wa Hekalu na wakafanikiwa kukamilisha kazi hii nyeti kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa anatenda kazi pamoja nao! Ni rahisi hata kwa watu kurekebisha maisha yao, lakini yataka moyo: kwa mwanamke kupata mimba, kuzaa na kumlea mtoto kadiri ya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kuna haja ya kubadili mwelekeo na kuanza kujenga fikra mpya; kwa kuondokana na mazoea, tayari kujiaminisha katika huruma na upendo wa Mungu. Kamwe waamini wasikubali kutumbukia kwenye kishawishi cha kukata tamaa. Waisraeli walifanikiwa kukamilisha ujenzi wa Hekalu kwa sababu walibeba mikononi mwao matofali kwa ajili ya ujenzi na upanga kwa ajili ya kulinda kazi ya ujenzi. Baba Mtakatifu anasema, ujenzi na upyaisho wa maisha ya mwanadamu ni mapambano pevu; yanayohitaji neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini inayopaswa kulindwa na kutunzwa kwa njia ya sala na kazi, ili kutowapatia nafasi watu wenye nia mbaya, wanaotaka kulibomoa tena Hekalu la Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, historia ya watu wa Mungu inaonesha ukweli wa mambo: mafanikio, matatizo na fursa mbali mbali zilizojitokeza, lakini kwa namna ya pekee kabisa wameshuhudia nguvu ya Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu; nguvu ya uwepo wa Mungu katika historia na safari ya maisha yao. Hii ndiyo kazi kubwa iliyofanywa na Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti". Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka ameonesha ushindi mkubwa katika maisha yao, chemchemi ya Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa; tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mwenyezi Mungu anaendelea kuonesha nguvu yake katika kazi ya uumbaji inayopata utimilifu wake katika kazi ya ukombozi. Huu ndio ushindi wa Kristo Yesu unaomwezesha kujenga upya, Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa pamoja na kupyaisha maisha ya waja wake. Waamini wanakumbushwa kwamba, bila ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao, hawataweza kuthubutu kusimama kwa jeuri yao wenyewe.

Imani kwa Kristo Yesu ni muhimu sana ili kupyaisha na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha. Baba Mtakatifu anasema, amependa kuyatafakari haya pamoja nao, ili kusimama kidete katika mchakato wa ujenzi wa Hekalu la Mungu; ujenzi na upyaishaji wa maisha, kwa kuonesha ari na moyo wa kutaka kupyaisha maisha kila wakati, kwa kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Ujenzi na upyaishaji wa maisha ukite mizizi yake katika sala na kazi; kwa njia hii, Mwenyezi Mungu ataweza kuwalinda na wao watafanikiwa kusonga mbele. Daima wawe na ari na moyo mkuu wa kutaka kushiriki katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa pamoja na kupyaisha maisha yao kwa sala na kazi. Na kwa njia hii wataweza kushinda mapambano haya! Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, wale waliojiweka wakfu ndani ya Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti", wamejiweka tena wakfu kwa Moyo Safi wa Bikira Maria, asiyekuwa na doa.

Papa: Misa: Orizzonti

 

25 September 2019, 15:10