Papa Francisko anaitaka Jumuiya ya Abramo kumwilisha imani katika matendo. Papa Francisko anaitaka Jumuiya ya Abramo kumwilisha imani katika matendo. 

Wito kwa Jumuiya ya "Abramo" Miaka 30: Imani katika matendo!

Baba Mtakatifu amewaasa wamfuate Ibrahim, Baba wa imani aliyekubali kuiacha nchi yake na jamaa zake na kumfuata Mwenyezi Mungu akielekea mahali asipokujua. Akabahatika kuwa ni baba wa imani. Alisafiri na familia yake jambo ambalo linawakumbusha waamini kuambatana na kusafiri pamoja katika jumuiya. Jumuiya ya “Abramo” iwe ni shuhuda wa imani na upendo wa Kristo Yesu.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi ya tarehe 14 Septemba 2019 amekutana na Jumuiya ya “Abramo” mjini Vatican akiwaalika wanajumuiya ya “Abramo” kumsikiliza Roho Mtakatifu katika tafakari ya ukimya na kuishuhudia imani kama Ibrahim alivyoishuhudia. Baba Mtakatifu ameyasema hayo katika maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo. Akiwapongeza kwa furaha wanayoihubiri duniani, Baba Mtakatifu amesistiza waendelee kujituma na hasa wakati jumuiya hiyo ngali na nguvu. Akimnukuu Mtakatifu Petro aliyeandika barua kwa jumuiya changa ili kuwaimarisha katika imani yao, vivyo hiyo na Jumuiya ya “Abramo” inatakiwa kufuata mfano huo. Ikumbuke kuwa, Jumuiya ya Abaramo ni moja kati ya jumuiya za Kanisa Katoliki zilizojengwa katika roho na ushirika wa kikarismatiki. Ni jumuiya ya kimataifa iliyoanzishwa mnamo mwaka 1989 na Mtakatifu Yohane Paulo II na inayotambuliwa na sheria ya Kanisa Katoliki na ni moja kati vyama vya kitume vinavyotambuliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.

Kwa sasa jumuiya hiyo ina jumuiya ndogo ndogo takribani 90 za kikarismatiki ambazo mnamo mwaka 2008 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alielezea utume wake katika  hadhira ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili waVatican ikiwa pamoja na kuhuisha roho ya kikarismatiki ya Kanisa Katoliki. Jumuiya ya “Abramo” imeundwa kwa malengo ya kulinda utambulisho wa kikatoliki wa jamii za hisani na kuwatia moyo waamini kudumisha uhusiano wa karibu na Maaskofu na mamlaka ya kipapa. Utume wao unajikita katika kumtangaza Yesu Kristo kwa watu. Jumuiya ya Abraham kupitia malezi yake, mikutano yake ya maombi ya  uinjilishaji hujibidisha katika utoaji wa huduma kwa wanaohitaji msaada wa wongofu wa kawaida na ukuaji wa kiroho katika kumsifu Mungu Baba. Wakikazia makuzi ya ndani katika kumfuta Yesu Kristo kwa dhati  kwa njia ya Roho Mtakatifu. Aidha Baba Mtakatifu amewaasa kuwa, furaha inayorutubishwa na Roho Mtakatifu na uchangamfu wao wanaouonesha katika utume wao wa kila siku utokane na tumaini la kukutana na Kristo katika maisha yao.

Hivyo ni lazima wajifunze kumsikiliza Roho Mtakatifu ili waweze kulielewa neno lake Mungu. Akitoa hamasa hiyo, Baba Mtakatifu amewaasa wamfuate Ibrahim, Baba wa imani aliyekubali kuiacha nchi yake na jamaa zake na kumfuata Mwenyezi Mungu akielekea mahali asipokujua. Ibrahim aliyaweka matumaini yake yote mikononi mwa Mungu, lakini hakuwa peke yake bali alisafiri na familia yake jambo ambalo kwetu linatukumbusha kusafiri pamoja katika jumuiya zetu. Katika muktadha huo, Jumuiya ya “Abramo” inapaswa kuchota mafundisho yake katika upendo wa Kristo na kuwapelekea Habari Njema waliosetwa, maskini na wahitaji wakiwaaminisha katika mapenzi ya Mungu.  Kama vile imani ya Ibrahimu ilivyoshinda matakwa yote ya kibinadamu ndivyo imani ya waamini ikitegemezwa na maisha pamoja na mafundisho ya Yesu Kristo mwana wa Ibrahimu inavyotakiwa kutangazwa na kutoa mwaliko wa kuendelea kuitika “niko hapa” kwa Baba yetu aliye mbinguni kama Mama yetu Bikira Maria anavyotufundsha. Baada ya wosia huo Baba Mtakatifu Francisko alitawapatia baraka na amani.

[ Audio Embed Papa: Abramo]    

 

15 September 2019, 11:49