Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, watakatifu wanawategemeza waamini wenzao katika mchakato wa utakatifu wa maisha! Papa Francisko asema, watakatifu wanawategemeza waamini wenzao katika mchakato wa utakatifu wa maisha! 

Papa: Watakatifu ni mashuhuda wa mchakato wa utakatifu wa maisha

Baba Mtakatifu Francisko asema, watakatifu ni mifano hai ya mashuhuda na wafuasi wa Kristo, wanaoendeleza kuwategemeza hata waamini wengine katika safari yao kuelekea kwenye utakatifu wa maisha. Papa pia ametambua uwepo wa wafanyabiashara vijana kutoka Barani Afrika, wanaotaka kushikamana katika “Harambee” kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Afrika.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 15 Septemba 2019, aliwapongeza viongozi wa Serikali ya Urussi pamoja na Ukraine kwa kutekeleza mkataba wa kubadilishana wafungwa wa vita na hatimaye, kuachiwa huru, ili waweze kuungana tena na familia zao. Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kusali ili hatimaye, vita huko Ukraine iweze kupata suluhu na amani ya kudumu.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro aliyetangazwa, Jumamosi, tarehe 14 Septemba 2019 huko Forli, nchini Italia. Alifariki dunia kunako mwaka 1964 akiwa na umri wa miaka 28. Ni kijana ambaye maisha yake yote yalipigwa chapa ya “Msalaba wa ugonjwa”. Mwenyezi Mungu akamkirimia neema na baraka za kuweza kubeba ugonjwa wake na kuugeuza kuwa mwanga angavu wa ushuhuda wa imani na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Jumapili, tarehe 15 Septemba 2019, huko Limburg, Ujerumani, Mtumishi wa Mungu Padre Riccardo Henkes wa Shirika la Wapallottini, ametangazwa kuwa Mwenyeheri. Padre Riccardo Henkes aliuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani huko Dachau kunako mwaka 1945. Hii ni mifano hai ya mashuhuda na wafuasi wa Kristo, wanaoendeleza kuwategemeza hata waamini wengine katika safari yao kuelekea kwenye utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu pia ametambua uwepo wa wafanyabiashara vijana kutoka Barani Afrika, wanaotaka kushikamana katika “Harambee” kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Afrika.

Papa: Angelus

 

15 September 2019, 12:34