Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko atoa muhtasari wa yale yaliyojiri wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. Baba Mtakatifu Francisko atoa muhtasari wa yale yaliyojiri wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. 

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Yaliyojiri wakati wa ziara

Baba Mtakatifu Francisko anasema: Matumaini ya watu ni Kristo na Injili yake, chachu makini ya udugu, uhuru, haki na amani kwa watu wote. Baba Mtakatifu kwa kufuata nyayo za watakatifu waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili, amesema, hija yake Barani Afrika ilikuwa ni kupandikiza chachu hii kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4 hadi 10 Septemba 2019, kimsingi ilipania kukuza: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu iliyoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini” na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 11 Septemba 2019 ameshuhudia yale mambo msingi “yaliyomkuna kutoka katika undani wa moyo wake” wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. Matumaini ya watu ni Kristo na Injili yake, chachu makini ya udugu, uhuru, haki na amani kwa watu wote. Baba Mtakatifu kwa kufuata nyayo za wamisionari na watakatifu waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili, amesema, hija yake Barani Afrika ilikuwa ni kupandikiza chachu hii kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius.

Nchini Msumbiji amekwenda kupandikiza mbegu ya matumaini, amani na upatanisho wa kidugu, ili kuwawezesha watu wa Mungu kuandika ukurasa mpya wa matumaini kutokana na majanga ya vita na maafa asilia. Kanisa linaendelea kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu ameishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa mchango wake katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, viongozi wakuu wa Serikali wataendelea kujikita katika kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amewataka vijana wa kizazi kipya kujenga na kudumisha umoja, upendo, ushirikiano na urafiki, sanjari na kuendelea kuchota hazina na utajiri kutoka kwa tamaduni za wazee wao. Kwa wakleri, watawa na majandokasisi, amewahimiza kuwa ni mashuhuda na vyombo imara vya uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu anasema, ameguswa na Injili ya Msamaria mwema inayohubiriwa na kushuhudiwa nchini Msumbiji katika Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” iliyozinduliwa tarehe 7 Juni 2018.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaendesha mradi mkubwa wa kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto unaojulikana kama “DREAM” yaani “Disease Relief Through Excellent and Advanced Means”. Mradi wa “The Dream” unapania kutoa dawa za kurefusha maisha sanjari na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto unaendelea kuonesha mafanikio makubwa Barani Afrika. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na kizazi ambacho hakina virusi vya Ukimwi. Mradi huu pia unawajengea uwezo wa kiuchumi waathirika wa Virusi vya Ukimwi, ili kujitegemea na kuzisaidia familia zao kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. Dr. Cacilda Massango, Mratibu wa Mradi wa “DREAM” nchini Msumbiji ni kati ya wanawake waliopata bahati ya kujifungua watoto bila maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, leo hii ni kati ya wafanyakazi wa Hospitali hii wanaotoa huduma kwa waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi.

Hii ni familia mpya ambayo imemwezesha kupata tiba na kurudisia tena utu na heshima yake kama binadamu na kwamba, anayo matumaini kwa leo na kesho iliyo bora si tu kwake binafsi, bali hata kwa watoto wake. Kwa njia ya Mradi huu, wananchi wengi wa Msumbiji wamepata matumaini mapya. Baba Mtakatifu anasema, kilele cha hija yake ya kitume nchini Msumbiji ni Ibada ya Misa takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa michezo wa Zimpeto. Watu wa Mungu wameshuhudia ile furaha, kiasi hata cha kusahau mvua kubwa iliyokuwa inanyeesha. Hii ilikuwa ni changamoto ya kumwilisha ujumbe wa upendo kwa adui sanjari na kupandikiza mbegu ya mageuzi ya Injili ya upedo ili kuzima chuki na uhasama tayari kuchipusha udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu anasema amekwenda nchini Madagascar kama “Mpanzi wa amani na matumaini”. Hii ni nchi iliyokirimiwa utajiri mkubwa wa mali asili, lakini inasiginwa na umaskini.

Lakini, kwa njia ya mshikamano wa upendo, watu wa Mungu nchini Madagascar, wanaweza kuvuka kuta za utengano na kuanza mchakato wa ujenzi wa uchumi unaoheshimu mazingira kwa kujikita katika haki jamii. Kama alama ya kinabii, Baba Mtakatifu anasema, alipata nafasi ya kutembelea Mji wa Akamasoa ulioanzishwa na Padre Pedro Opaka ili kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu. Hiki ni kilio cha watu wasiokuwa na makazi; kilio cha watoto wanaozama katika dimbwi la ujinga, njaa na utapiamlo wa kutisha; kilio cha umati mkubwa watu wasiokuwa na fursa za ajira; watu wanaodhalilishwa na kutezwa; kilio cha watu wasiokuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kila shule na kituo cha zahanati eneo la Akamasoa ni wimbo wa imani na matumaini unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili, kwa kukazia kazi, utu, heshima, huduma kwa maskini pamoja na elimu makini kwa watoto. Baadaye aliweza kushiriki katika sala ya kuombea wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anasema alipata pia bahati ya kusali na watawa wa mashirika ya ndani, ili kuhamasisha ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu anasema Askofu ni mpanzi wa amani, matumaini na imani. Ni kiongozi anayesimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za ndugu zake. Ni kiungo cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu anapaswa kuwa mwaminifu kwa Injili sanjari na kujenga uhusiano mwema na wakleri wake ambao ni wenza wa mchakato wa uinjilishaji. Papa Francisko katika mkesha na vijana wa kizazi kipya, amewataka vijana kumtafuta Kristo Yesu kwa njia ya huduma; wajitahidi kuwa ni watu wema zaidi, kwani Kristo Yesu anaishi na anawataka vijana nao kuishi kikamilifu, kwa kutambua kwamba wao ni matumaini ya Madagascar na Kanisa. Vijana wanaitwa kuwa mitume wamisionari wa Yesu na watambue kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu inayowajibikiana. Baba Mtakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu, alikazia umuhimu wa kuangalia mahusiano na mafungamano ya kifamilia; Ujenzi wa ufalme wa Mungu kadiri ya mapenzi ya Mungu na mwishoni ni jinsi ya kushirikishana maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuwa ni kiini na mwongozo wa maisha ya waja wake.

Baba Mtakatifu amesisitiza kuhusu umuhimu wa kufuata masharti ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya mwisho nchini Madagascar imekuwa ni wimbo wa shukrani, kumbu kumbu na utambuzi wa urithi wa kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji; changamoto za uinjilishaji, utambulisho wa maisha ya kipadre na kitawa; furaha ya uinjilishaji na sala kama silaha ya mapambano katika maisha ya kipadre na kitawa. Ushuhuda unaofumbatwa katika uinjilishaji. Baba Mtakatifu anasema, katika hija yake ya kitume nchini Mauritius amekazia zaidi kuhusu: Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa kuendeleza demokrasia shirikishi pamoja na kuendelea kujikita katika sera na mikakati ya uchumi ufungamani unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Papa: Afrika

 

11 September 2019, 16:12