Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Ndoto ya vijana wa Msumbiji inafumbatwa katika: matumaini, amani na upatanisho wa kidugu na kamwe wasikubali mtu kuwapoka matumaini yao! Papa Francisko: Ndoto ya vijana wa Msumbiji inafumbatwa katika: matumaini, amani na upatanisho wa kidugu na kamwe wasikubali mtu kuwapoka matumaini yao!  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Msumbiji! Ndoto ya vijana!

Vijana wanapaswa kushikamana kama familia ya Mungu ili kutetea amani; kwa kuendelea kuandika kurasa zinazosheheni matumaini, amani na upatanisho wa kidugu. Ndoto za vijana zinamwilishwa katika sanaa za maonesho na muziki, kiasi cha kuwajengea umoja na mshikamano. Vijana watambue kwamba, wana nguvu na uwezo wa kuangalia ya mbeleni kwa matumaini makubwa. NDOTO!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa hija yake ya kitume nchini Msumbiji, Alhamisi tarehe 5 Septemba 2019 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na vijana kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali nchini Msumbiji. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa njia ya sanaa za maonesho na muziki. Adui mkubwa wa matumaini ni kuchoka na kujikatia tamaa. Vijana wajenge umoja na mshikamano; kamwe wasikubali kujijengea maadui kwani ni chanzo cha maafa. Wafanye kazi kama jumuiya; wawapende na kuwaheshimu wazee; wadumishe ari na moyo wa mshikamano; wasimame kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote na kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda sana!

Baba Mtakatifu amewahakikishia vijana wa kizazi kipya kutoka Msumbiji kwamba, wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wake. Vijana ni matumaini ya Msumbiji kwa leo na kesho iliyo bora zaidi na kwamba, wanapaswa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na matumaini. Vijana wanapaswa kushikamana na kusimama pamoja kama familia ya Mungu ili kutetea amani; kwa kuendelea kuandika kurasa zinazosheheni matumaini, amani na upatanisho wa kidugu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndoto za vijana zinamwilishwa katika sanaa za maonesho na muziki, kiasi cha kuwajengea umoja na mshikamano. Vijana watambue kwamba, wana nguvu na uwezo wa kuangalia ya mbeleni kwa matumaini na kwamba, kamwe wasikubali mtu yeyote awapokonye matumaini yao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumaini yanaweza kufishwa kwa vijana kuchoka na kujikatia tamaa ya maisha;  kwa kujenga maisha na furaha katika ombwe; hali inayoweza kuwatumbukiza katika ugonjwa wa sonona au kuamua kuchukua njia inayoweza kuwapotosha. Matatizo na changamoto za maisha, zinapaswa kukabiliwa kikamilifu kwa kuwajibika barabara pasi na kukata tamaa kama alivyofanya Eusebio da Silva, Mchezaji mashuhuri wa mpira wa miguu kutoka nchini Msumbiji. Hali ngumu ya uchumi na kifo cha baba yake havikumzuia kutekeleza ndoto yake, akajizatiti na kusonga mbele. Katika michezo yote alifanikiwa kufunga magoli 77 kwa timu yake  ya Maxaquene “Mashakene”. Alikuwa na kila sababu ya kujikatia tamaa katika maisha, lakini amesonga mbele na leo hii ni mmoja kati ya watu maarufu kwa kucharaza kabumbu duniani!

Bwana Eusebio da Silva, ni mtu aliyedumisha pia ubora wa karama na mapaji yake kwa kucheza na wengine kama timu. Akajenga utamaduni wa kukutana na jirani zake, licha ya tofauti msingi kati yao. Vijana wathubutu kukutana kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao. Uadui ni chanzo cha maafa makubwa kwa familia na jamii katika ujumla wake. Vijana watafute fursa ya kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii, kwa kudumisha majadiliano; kwa kupania kuwasaidia wengine na kuweka kando tofauti zao kwa ajili ya mustakabali wa nchi yao katika ujumla wake. Huu ndio utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi. Vijana wa Msumbiji wathubutu kuwa na ndoto ya pamoja, ili kuandika ukurasa mpya wa nchi yao kwa kutembea kwa pamoja kama ndugu.

Vijana wa Msumbiji wajitahidi kufanya kazi kwa umoja, upendo na mshikamano kama ndugu. Watambue kwamba, wanaweza kufikia ndoto zao kwa njia ya matumaini, uvumilivu na majitoleo katika hali ya utaratibu bila haraka, tayari kufanya maamuzi mazito katika maisha. Vijana wasikate tamaa wanapofanya makosa, wala kukata tamaa mambo yanapokwenda mrama na kwamba, kosa kubwa ni pale ambapo kijana ataitelekeza ndoto yake ya kuwa na nchi bora zaidi. Mwanariadha maarufu kutoka Msumbiji, Maria Mutola ameshiriki mara tatu katika Michezo ya Olympic, lakini mara ya nne, akajinyakulia Medali ya dhahabu. Na ameshinda mara 9 tuzo la Kimataifa, lakini bado anakumbuka watu, historia pamoja na kuwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kupata mahitaji yao msingi nchini Msumbiji. Michezo ni mwalimu wa maisha anayoweza kuwasaidia vijana kudumu katika ndoto yao!

Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana wa Msumbiji kujenga na kudumisha mafungamano ya kweli na wazee kwani vijana wana utabiri, lakini wazee wana ndoto. Wazee wanaweza kuwasaidia vijana kuendeleza ndoto ya maisha yao, kwani wao wana hazina ya: historia, uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Hata kama inataka moyo kweli kweli kuishi na wazee, lakini bado inalipa. Kwani kwa njia ya mshikamano huu wanaweza kupata uhuru wa kweli, ari, kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi na kuendelea kuwa na maono mapana kwa siku za usoni. Hii ni “mbolea” inayoweza kupyaisha ndoto ya maisha kwa kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha kwa njia ya umoja na mshikamano. Vijana wengi wa kizazi kipya ni wale ambao wamezaliwa wakati wa amani nchini Msumbiji.

Hii ni amani inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa; kwa kusaidiana kwa hali na mali; kwa kujenga na kudumisha urafiki pamoja na kuendelea kushikamana kama wamoja, silaha madhubuti katika mchakato wa mabadiliko ya kihistoria. Vijana washikamane pia kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Wananchi wa Msumbiji wamekwisha kuguswa na kutikiswa na majanga asilia. Waendelee kushikamana kama familia ya Mungu inayowajibika. Vijana watambue kwamba, kwa hakika wanapendwa na Mwenyezi Mungu; anawathamini jinsi walivyo, kwa karama na mapaji yao; kwa udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake kujifunza daima kutokana na makosa yao, kwa sababu anawapenda sana. Vijana wajitahidi kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao kwa njia ya ukimya. Upendo wake unaokoa, unaganga na kuponya. Ni upendo unaowapatanisha watu na kuwapatia mwelekeo wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaambia vijana kwamba, ni matumaini yake kuwa wataendelea kuwa ni vyombo vya upatanisho, upendo na matumaini na kwamba, daima watatembea katika furaha na njia za amani.

Papa: Vijana

 

05 September 2019, 16:01