Tafuta

Vatican News
Papa Francisko mwishoni mwa hija yake ya kitume nchini Msumbiji, amewashukuru na kuwapongeza wote kwa sadaka na majitoleo yao. Muhimu: Mshikamano, Matumaini na Upatanisho. Papa Francisko mwishoni mwa hija yake ya kitume nchini Msumbiji, amewashukuru na kuwapongeza wote kwa sadaka na majitoleo yao. Muhimu: Mshikamano, Matumaini na Upatanisho.  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Matumaini ni kiini cha Upatanisho

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wananchi wote wa Msumbiji wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini aliyoyashuhudia wakati wote wa uwepo wake nchini humo. Waendelee kujikita katika matumaini, umoja na mshikamano wa dhati na kamwe wasikubali wajanja wachache kuwapoka matumaini haya ambayo ni chemchemi ya upatanisho nchini Msumbiji. Shukrani kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija yake ya kitume nchini Msumbiji kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyomwachia furaha kubwa moyoni mwake. Amewashuruku wadau mbali mbali waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa kama ilivyo pangwa. Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Serikali, vikosi vya ulinzi na usalama; viongozi wa kamati ya maandalizi pamoja na watu wa kujitolea bila kusahau umati mkubwa wa watu wa Mungu uliojitokeza kumlaki kwa shangwe na nderemo! Licha ya mvua kunyeesha lakini waamini wamevumilia hadi dakika ya mwisho ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mvua hii ilikuwa ni alama ya baraka!

Baba Mtakatifu anakiri na kutambua sadaka kubwa waliyoitoa wananchi wa Msumbiji ili kufanikisha maadhimisho na mikutano yote hii. Anawashukuru na kuwapongeza kutoka katika sakafu ya moyo wake. Amewakumbuka wale wote ambao hawakuweza kuhudhuria kutokana na kukumbwa na maafa. Kwa njia ya sala na sadaka zao, ameonja uwepo wao wa karibu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, wananchi wote wa Msumbiji wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini aliyoyashuhudia wakati wote wa uwepo wake nchini humo. Waendelee kujikita katika matumaini, umoja na mshikamano wa dhati na kamwe wasikubali wajanja wachache kuwapoka matumaini haya ambayo ni chemchemi ya upatanisho nchini Msumbiji. Mwishoni kabisa, amewaomba kumkumbuka kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Shukrani
06 September 2019, 17:02