Tafuta

Papa Francisko asema, mgogoro wa utambulisho wa maisha na wito wa upadre na kitawa unapyaishwa kwa kuwa: wachungaji wema, wafuasi amini na mitume wamisionari wa Kristo Yesu. Papa Francisko asema, mgogoro wa utambulisho wa maisha na wito wa upadre na kitawa unapyaishwa kwa kuwa: wachungaji wema, wafuasi amini na mitume wamisionari wa Kristo Yesu. 

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Maisha na utume wa Kanisa!

Mgogoro wa utambulisho wa kipadre unapyaishwa kwa kujikita katika msingi unaowataka kuwa wachungaji wema, wafuasi wamisionari, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika shughuli za kichungaji katika huduma ya ukarimu na upendo. Zakaria alionesha mashaka kinyume kabisa cha Bikira Maria, aliyekubali na kujiaminisha katika mpango wa Mungu. Uaminifu wa Kipadre & Kitawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Msumbiji, Alhamisi tarehe 5 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na: wakleri, watawa, waseminaristi, makatekista na wafanyakazi katika jumuiya mbali mbali za Kikristo nchini Msumbiji. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia zaidi kuhusu: Umuhimu wa Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa; Mgogoro wa utambulisho wa maisha na utume wa Kipadre; Maisha na utume wa watawa nchini Msumbiji mintarafu mfano wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu amewashukuru wote waliotoa shuhuda mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa nchini Msumbiji. Wamegusia changamoto changamani, udhaifu wa kibinadamu bila kusahau neema ya Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza Makatekista nchini Msumbiji ambao ni sehemu ya watu wa Mungu ambao katika kipindi cha vita na mipasuko ya kijamii nchini humo wameonesha ushupavu wa imani na upendo thabiti kwa maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka Makatekista kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu. Fumbo la Umwilisho linaonesha utayari na ukarimu wa Bikira Maria katika historia ya ukombozi. Kwa maisha na utume wa Yohane Mbatizaji na pamoja na Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu anataka kuonesha umuhimu wa kushirikiana, kushikamana, kutegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei watambue na kuthamini utambulisho wao katika Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mgogoro wa utambulisho wa maisha na wito wa kipadre na kitawa, unawakumba hata waamini walei! Hapa hakuna mtu anayeweza kujidai kubaki salama. Baba Mtakatifu anawataka wakleri kupata utambulisho wao kutoka kwa Bikira Maria, aliyetenda zaidi pengine kuliko Zakaria anayepata utambulisho wake kutokana na Mahali anapofanyia utume wake. Mapadre wanapaswa kuchota utajiri wao kutoka kwenye ufukara wa Kristo Yesu, tayari kujisadaka katika huduma, wakitambua kwamba, kwa njia ya Daraja takatifu wamekuwa ni marafiki wa Kristo. Wamwige Kristo Mchungaji mwema, wawe tayari kukiri udogo na mapungufu yao ya kibinadamu.

Mgogoro wa utambulisho wa kipadre unapyaishwa kwa kujikita katika msingi unaowataka kuwa wachungaji wema, wafuasi amini na wamisionari, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika shughuli za kichungaji katika huduma ya ukarimu na upendo. Zakaria alionesha mashaka kinyume kabisa cha Bikira Maria, aliyekubali na kujiaminisha katika mpango wa Mungu. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na furaha ya Injili inayomwilishwa katika maisha na utume wao. Wajitahidi kufurahi na wale wanaofurahi; Kuomboleza na wale wanao omboleza; wawe wapesi kuwapatia waamini Sakramenti za Kanisa. Mapadre wanapohisi kuvunjika na kupondeka moyo, wawe tayari kupyaisha maisha yao ya kiroho kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kujenga mahusiano ya karibu na Kristo Yesu.

Mapadre wajiangalie wasitumbukie na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Kila siku wajitahidi kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na utume wao; watafute muda wa ukimya, ili kutafakari na hatimaye, wakiwa wameungana na Kristo Yesu, waweze kutambua vyema wito wao. Bikira Maria na Mtakatifu Elizabeth, Mama mzazi wa Yohane Mbatizaji, wawasaidie mapadre na watawa kupyaisha furaha na masifu yao katika huduma na mchakato wa uinjilishaji nchini Msumbiji, ili kuendeleza dhamana na utume waliojichotea kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Wajenge madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kushirikishana tunu msingi za maisha, tamaduni na imani inayomwilishwa katika matendo. Utamadunisho anasema Baba Mtakatifu ni mchakato wa uinjilishaji unaotekelezwa kwa kusoma alama za nyakati, tayari kurithisha tunu msingi za Injili katika tamaduni mbali mbali za watu.

Makanisa mahalia, hayana budi kuendelea kujielekeza zaidi katika uinjilishaji wa awali bila wasi wasi wala woga wa kupita kiasi. Ubunifu upewe msukumo wa pekee katika mchakato wa uinjilishaji kihistoria na kamwe wasiwe ni watazamaji peke yao! Fumbo la Umwilisho, liwahamasishe watu wa Mungu nchini Msumbiji kujikita katika mchakato wa majadiliano kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kumtembelea Elizabeth, ili kudumisha mapendo kwa jirani, Kanisa pia linapaswa kufanya hija ya kutembelea, ili kudumisha mchakato wa amani na upatanisho wa kidugu, kwa kuondokana na dhana ya uadui ambao ni chanzo cha maafa makubwa katika jamii. Familia ya Mungu nchini Msumbiji ijenge utamaduni wa kufungua malango yake kwa heshima, ili kubadilishana mawazo na kujadiliana katika ukweli na uwazi kwani haya ni mambo ambayo yanawezekana kabisa!

Baba Mtakatifu Francisko amegusia pia ndoa mseto na changamoto zake katika maisha na utume wa Kanisa nchini Msumbiji. Ndoa hizi zimekuwa ni chanzo cha mpasuko na wala si katika mchakato wa kujenga na kuimarisha Injili ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika muktadha huu tofauti hizi zinaweza pia kuwa ni chanzo cha mipasuko na kinzani kati ya watu wa rangi mbali mbali; Kaskazini na Kusini; kati ya jumuiya mbali mbali; kati ya Mapadre na Maaskofu. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, mchakato ambao unapaswa kuwashirikisha watu wote, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Huu ni mchakato wa ujenzi wa jamii ya watu wa amani, haki na udugu kwa ajili ya maendeleo ya watu wote. Kanisa nchini Msumbiji, halina budi kutembea ili kutafuta suluhu ya kudumu katika maisha na utume wake; kwa kumwomba Roho Mtakatifu, kwani Roho Mtakatifu ndiye Mwalimu anayeweza kuwaonesha dira na mwongozo wa kufuata.

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka wakleri, watawa, waseminaristi, makatekista na waamini walei katika ujumla wao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria; ili waweze kuwa tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Mwenyezi Mungu awakirimie matumaini, amani na upatanisho wa kidugu, watu wa Mungu nchini Msumbiji.

Papa: Wakleri

 

05 September 2019, 17:12