Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 10 Septemba 2019 anafanya hija ya kitume Barani Afrika. Anawaomba waamini kumsindikiza kwa sala na sadaka zao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 10 Septemba 2019 anafanya hija ya kitume Barani Afrika. Anawaomba waamini kumsindikiza kwa sala na sadaka zao. 

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: 4-10 Septemba 2019

Baba Mtakatifu Francisko anawaomba waamini kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, ili hija yake Barani Afrika iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewaambia waamini na mahujaji waliokuwa wameungana naye kwa njia ya sala kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, akipenda, kuanzia Jumatano tarehe 4 hadi 10 Septemba, atakuwa anafanya hija thelathini na moja ya kitume Barani Afrika. Atapata nafasi ya kuwatembelea watu wa Mungu nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius. Baba Mtakatifu anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, ili hija yake Barani Afrika iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote,  sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”.

Baba Mtakatifu Francisko ni Papa wa pili kutembelea Msumbiji baada ya hija iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1988 na akapata nafasi pia kutembelea Madagascar mwaka 1989 na Mauritius mwaka 1989. Itakumbukwa kwamba, Msumbiji ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno kunako mwaka 1975 chini ya uongozi wa Rais Samora Machel aliyekuwa kiongozi wa Chama cha FRELIMO msimamo wake wa kisiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji, ukamgharimu maisha. Msumbiji ikatumbukia na kuzama katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka 15 hadi tarehe 4 Oktoba 1992 FRELIMO na RENAMO vikawekeana sahihi Mkataba wa Amani ambao umepyaishwa tena mwaka 2019. Demokrasia shirikishi imekuwa ikisuasua nchini Msumbiji. Ulinzi, haki, amani, usalama na upatanisho wa udugu kitaifa ni kati ya changamoto pevu nchini Msumbiji. Umaskini, magonjwa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mambo ambayo yameendelea kusababisha majanga kwa watu na mali zao.

Kanisa Katoliki nchini Msumbiji linaundwa na Majimbo 9 yenye idadi ya Parokia 343 zenye waamini milioni sita sawa na asilimia 28% ya wananchi wote wa Msumbiji na zinahudumiwa na Mapadre 659. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kumekuwepo na maboresho makubwa ya mahusiano kati ya Serikali na Kanisa. Aslimia 60% ya mali ya Kanisa iliyokuwa imetaifishwa na Serikali ya Msumbiji kunako mwaka 1977, tayari imekwisha rejeshwa tena mikononi mwa Kanisa Katoliki. Kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, Kanisa limeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na maendeleo fungamani ya binadamu. Changamoto changamani kwa sasa ni: rushwa na ufisadi; uhalifu wa kutumia silaha; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na utumwa mamboleo sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ukanimungu na utamadunisho ni changamoto zinazoendelea kuvaliwa njuga na Mama Kanisa kwa kutoka kipaumbele cha kwanza: maisha ya ndoa na familia; malezi na na makuzi ya vijana wa kizazi kipya; utamadunisho wa imani katika maisha pamoja na kuendeleza dhamana na utume wa vyama na mashirika ya kitume nchini Msumbiji bila kusahau uhamasishaji wa miito ya kitawa na kipadre, ambayo hadi wakati huu ni “kiduchu sana”.

Kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini”. Madagascar ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Wafaransa kunako mwaka 1960. Kwa miaka mingi Madagascar imeongozwa kwa “mkono wa chuma” hali iliyosababisha mapinduzi ya mara kwa mara pamoja na kuchechemea kwa mfumo wa demokrasia, ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo ya watu. Madagascar ni kati ya nchi maskini sana duniani, ambayo inakumbwa mara kwa mara na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha pamoja na magonjwa ya mlipuko. Matatizo yote haya yanachangiwa na maafa makubwa kwa watu na mali zao kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Madagascar ilianza kuinjilishwa kunako Karne ya XVI. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Madagascar ni sawa na asilimia 35% ya Idadi ya wananchi wote wa Madagascar. Kipaumbele cha kwanza ni utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na katekesi. Kanisa Katoliki nchini Madagascar linaundwa na Majimbo 22 yenye jumla ya Parokia 438 zinazohudumiwa na Mapadre 1, 747 na kila Jimbo lina kituo chake cha Radio! Madagascar wako vizuri kwa mawasiliano ya jamii. Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unajikita katika uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama njia ya kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu. Kanisa pia liko mstari wa mbele katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”.  Mauritius ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Wafaransa kunako mwaka 1968. Changamoto kubwa nchini humu ni ubaguzi wa kidini na kikabila hali inayoshuhudiwa pia hata katika masuala ya kidemokrasia. Lakini, Mauritius ni kati ya nchi za Bara la Afrika ambazo uchumi wake unakuwa kwa kiwango cha asilimia 5%. Kilimo cha miwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mauritius. Mwelekeo kwa sasa ni kuendelea kuwekeza katika kilimo cha nafaka na uanzishaji wa viwanda. Kiwango cha umaskini ni asilimia 2% kiwango cha chini sana Barani Afrika. Wastani wa maisha ya watu ni miaka 73 na idadi ya vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka 5 imepungua kutoka idadi ya watoto 64 hadi kufikia idadi ya watoto 15 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa. Watoto walioandikishwa shule ya msingi ni asilimia 90% ya idadi ya watoto wote nchini Mauritius. Uinjilishaji wa awali ulifanyika kuanzia Karne XVII na Ibada ya Misa ya kwanza nchini humo ikaadhimishwa kunako mwaka 1616. Leo hii Kanisa Katoliki nchini Mauritius lina Majimbo mawili yanayohudumiwa na Mapadre 95 wakisaidiwa na Makatekista 1, 335.

Waamini wa Kanisa Katoliki wanaunda asilimia 28% ya Idadi ya wananchi wote wa Mauritius. Kuna uhusiano mwema kati ya Kanisa na Serikali ya Mauritius katika kukuza na kudumisha uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu. Ili kuepukana na kinzani pamoja na mipasuko ya kidini na kiimani, inayoweza kukwamisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kunako mwaka 2001, Serikali iliunda Baraza la Viongozi wa Kidini, ili kukuza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni pamoja na kukoleza huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii. Kanisa nchini Maurtius, katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji, linatoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya ndoa na familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo na mshikamano sanjari na utume kwa vijana wa kizazi kipya. Kuyumba na kutopea kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; utumwa mamboleo na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na ukanimungu ni kati ya changamoto zinazo ikabili familia ya Mungu nchini Mauritius.

Idadi ya miito ya kitawa na kipadre inaendelea kuporomoka mwaka hadi mwaka. Jambo la kumshukuru Mungu ni ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji pamoja na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Malezi na majiundo makini ya Makatekista yanaendelea kupewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 ataweza kushuhudia hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius.

Papa: Hija Barani Afrika
02 September 2019, 12:08