Tafuta

Papa Francisko katika mahojiano maalum na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake amegisia kwa ufupi maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Papa Francisko katika mahojiano maalum na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake amegisia kwa ufupi maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. 

Hija ya Papa Francisko Afrika: Mahojiano na waandishi wa habari

Baba Mtakatifu Francisko amezungumzia kuhusu familia, vijana na dhamana ya Serikali; amani, upatanisho na msamaha wa kweli; umuhimu wa kutangaza na kushuhudia kweli za maisha ya binadamu; madhara ya ukoloni wa kiitikadi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; cheche za mpasuko wa Kanisa na umuhimu wa unyenyekevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4 hadi 10 Septemba 2019, kimsingi ilipania kukuza: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu iliyoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho”. Kwa upande wa Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini” na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”.

Baba Mtakatifu, akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Jumanne, tarehe 10 Septemba 2019 alipata "muda wa saa 1:30 kuchonga" na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kuhusu yale yaliyojiri katika hija yake ya kitume pamoja na maswali tete katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu familia, vijana na dhamana ya Serikali; amani, upatanisho na msamaha wa kweli; umuhimu wa kutangaza na kushuhudia kweli za maisha ya binadamu; madhara ya ukoloni wa kiitikadi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; cheche za mpasuko wa Kanisa na umuhimu wa unyenyekevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa nchini Msumbiji: Baba Mtakatifu anaipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imesimama kidete ili kuhakikisha kwamba mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa, licha ya matatizo na changamoto zake, unarejea tena na matokeo yake ni kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Amani huko Serra da Gorongosa kati ya Chama cha FRELIMO na Chama cha RENAMO. Hizi ni jitihada za Kanisa, Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na kwa namna ya pekee, Kardinali mteule Matteo Maria Zuppi, enzi hizo akiwa bado Padre kijana. Mkataba huu unafutilia mbali uhasama kati ya ndugu wamoja nchini Msumbiji na kwamba, Mkataba huu utaimarisha zaidi Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi mjini Roma kunako mwaka 1992. Matunda ya mchakato huu yameanza kuonekana kwa kutambuana kama ndugu, wenye dhamana na wajibu wa kuendeleza ustawi wa nchi ya Msumbiji. Kwa vita, watu wanapoteza yote, lakini kwa njia ya amani watu wanapata ustawi na maendeleo endelevu. Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, amani inapeta katika akili na nyoyo za wananchi wa Msumbiji.

Ujasiri unaleta amani ya kweli, unatafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi. Wananchi wa Msumbiji wameteseka sana kwa madhara ya vita na kinzani za kijamii, lakini hawakutaka kukubali kutawalia na chuki, uhasama na mtindo wa kutaka kulipizana kisasi na kwamba, vita haikuwa na usemi wa mwisho katika mustakabali wa wananchi wa Msumbiji. Vita imeharibu sana makazi ya watu, imewatumbukiza wananchi katika baa la njaa, ujinga na maradhi. Vita imewakosesha watu nyumba za sala na ibada; imepelekea watu kukosa fursa za ajira na kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi wa Msumbiji walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama na hifadhi ya maisha yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani ni kito cha thamani kinachotakiwa kutunzwa kama mtoto mchanga! Amani ni ushindi wa taifa katika ujumla wake. Hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilipolipuka. Hakuna sababu msingi ya kuendekeza matumizi ya mtutu wa bunduki unaowanufaisha watu wachache wenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka unaonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia!

Changamoto za maisha ya vijana Barani Afrika: Baba Mtakatifu anasema, Barani Afrika kuna idadi kubwa ya vijana wa kizazi kipya, ikilinganishwa na Bara la Ulaya, ambalo watu wake wengi wanaelekea uzeeni. Kufikia mwaka 2050 kutakuwepo na idadi kubwa ya wazee waliostaafu kazi, kuliko wale wanaofanya kazi kuzalisha bidhaa na kutoa huduma. Kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya ni matokeo ya ubinafsi, choyo na watu kupenda mno anasa na starehe katika maisha. Bara la Afrika limesheheni cheche za maisha, wanafurahia watoto wao kama amana na utajiri wa maisha yao kwa siku za usoni. Wanawaonea fahari watoto hawa kama ilivyo hata katika nchi nyingi zinazoendelea duniani. Baba Mtakatifu anasema, watoto Barani Afrika ni amana na utajiri wa maskini, familia na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anasema, changamoto kubwa kwa Bara la Afrika kwa sasa ni kuhakikisha kwamba watoto na vijana wanapewa elimu bora na makini; wanapata huduma safi za afya, malezi na majiundo makini. Elimu ni haki msingi kwa kila mtoto na pale inapowezekana elimu bure itolewe kwa wote!

Chuki dhidi ya wageni Afrika ya Kusini “Xenofobia”: Baba Mtakatifu anasema, huu ni ugonjwa hatari sana katika maisha mwanadamu na umeenea sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kielelezo cha uchoyo na ubinafsi; kiburi cha baadhi ya watu kujisikia kuwa ni watu wa maana zaidi kuliko wengine na mara nyingi chuki hizi zinachochewa na wanasiasa wanaotaka umaarufu usiokuwa na mvuto wa la mashiko. Haya ndiyo yaliyosababishwa na viongozi kama Adolf Hitler. Ukabila, udini na upendeleo ni magonjwa ambayo yamesababisha mauaji ya kimbari huko Rwanda na hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu mauaji haya yalipotokea na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anasema, alipokuwa nchini Kenya aliwataka vijana kuachana na tabia ya kukumbatia ukabila usiokuwa na mashiko. Hizi pia ni chuki za ndani dhidi ya ndugu wamoja. Ukabila katika baadhi ya nchi za Kiafrika anasema Baba Mtakatifu umekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kama ilivyotokea nchini Rwanda!

Wito wa familia na dhamana ya Serikali katika huduma kwa familia: Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni kitalu cha uhai; shule ya maadili, utu wema na uwajibikaji. Ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, yaani wito wa ndoa na familia, daraja takatifu na maisha ya kuwekwa wakfu. Lakini pia familia ni shule ya mahusiano na mafungamano ya kijamii; hapa ni mahali pa kwanza pa kutekeleza utume na ushuhuda wao kama Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameguswa sana na shuhuda mbali mbali zilizotolewa na vijana wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. Vijana wanapaswa kupewa malezi na makuzi bora ili kujiandaa kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Changamoto kubwa kwa familia nyingi ni umaskini wa kipato na hali ngumu ya maisha inayowafanya wazazi na walezi kushindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu kwa familia zao. Matokeo yake ni wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi au wanaofanyishwa kazi za suluba ili kusaidia kuchangia mahitaji msingi ya familia. Serikali ina dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, inaunda sera na mazingira bora zaidi yatakayozisaidia familia kutekeleza wajibu wake. Jamii inapaswa kutambua kwamba, watoto ni amana na utajiri unaopaswa kukuzwa na kuendelezwa. Watoto ni furaha na matumaini ya jamii!

Mafundisho Jamii ya Kanisa na Utekelezaji wa Sheria na Maamuzi ya Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Mahakama za Kimataifa, ikiwa kama maamuzi haya yanatolewa katika ukweli na haki kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wanapaswa kujifunza kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa, ndiyo maana ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa pamoja na vyombo vya sheria kimataifa. Baba Mtakatifu anasema, lakini suala ya uhuru wa watu kutoka katika makucha ya wakoloni, hii ni haki yao msingi inayopaswa kuheshimiwa. Kwa bahati mbaya nchi nyingi za Afrika zimepewa uhuru wa bendera lakini bado ziko kwenye ukoloni mamboleo. Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ulaya na Mashirika mbali mbali ya Kimataifa yanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu na uhuru wa kweli. Baba Mtakatifu anasema, ukoloni mkongwe umepita, ukaingia ukoloni mamboleo, lakini kwa sasa kuna ukoloni wa kiitikadi. Huu ni mfumo unaokumbatiwa na utandawazi tenge unaotaka kufutilia mbali: tofauti, utambulisho na historia za watu katika medani mbali mbali za maisha. Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha utambulisho na historia ya watu mahalia.

Mchakato wa Majadiliano ya Kidini na Kiekume: Ni kielelezo cha ukomavu wa watu katika mchakato wa ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu; kwa kuheshimu na kuthaminini uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini, sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu ameguswa sana na majadiliano ya kidini yanayoendelezwa nchini Mauritius. Hii ni changamoto ya kuondokana na wongofu wa shuruti hata katika masuala ya kisiasa. Jambo la msingi ni imani inayomwilishwa katika matendo kielelezo cha imani tendaji. Ushuhuda wa imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni msingi wa uinjilishaji mpya, kazi inayotekelezwa na Roho Mtakatifu. Ushuhuda wa imani uwawezeshe waamini kumwabudu Mungu katika roho na kweli; kwa njia ya huduma ya upendo, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Watu wanataka kuona dini ikisaidia kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano, upatanisho na umoja wa kitaifa.

Ushuhuda wa furaha na imani katika matendo: Baba Mtakatifu anasema, ameguswa na kuonja upendo, ukarimu na mshikamano wa watu wa Mungu waliojitekeza barabarani kumlaki. Ameshuhudia watu wa Mungu wakionesha furaha kutoka katika undani wa maisha yao; wakawa tayari kuvumilia mvua kubwa na jua lililokuwa linawawakia.  Hii ni imani ambayo imeshuhudiwa na watu kutembea mwendo mrefu ili kukesha na hatimaye, kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema katika matukio haya yote ya imani akajiona mdogo sana. Ni watu ambao wengi wao wameshinda na kulala na njaa. Hii ndiyo furaha inayojengwa na kudumishwa katika umoja wa udugu wa kibinadamu. Kwa wale watu wanaotembea pweke pweke katika ubinafsi na uchoyo, wanapoteza ari na mwelekeo huu. Kuna haja ya watu kutambua na kuthamini utambulisho wao; kuthamini na kudumisha mambo msingi yanayowajenga na kuwaunganisha kama ndugu wamoja, ili kushirikishana ile furaha inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao! Hii ni furaha ambayo ilioneshwa na wazazi na watoto wakaishiriki pia!

Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia kweli za maisha ya binadamu: Shirika la Habari nchini Hispania, EFE, linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 80 tangu lilipoanzishwa. Baba Mtakatifu anasema, anayo nia thabiti ya kutembelea Hispania, Mwenyezi Mungu akimjalia, lakini kwa sasa kipaumbele ni kwa nchi ndogo ndogo. Kuhusu mchango wa mawasiliano ya jamii, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kujikita katika ukweli unaofumbatwa katika matukio yenyewe. Kwa bahati mbaya, maelezo na ufafanuzi wa matukio unaweza kusababisha ukweli ukapotea. Mawasiliano hayana budi kujikita katika utu na heshima ya binadamu; yawasaidie watu kukua na kukomaa katika maisha yao na kamwe mawasiliano ya jamii yasitumike kama nyenzo ya kuchochea vita, kinzani na mipasuko au kuwachafulia watu heshima yao bali yakoleze ujenzi wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Utunzaji bora wa mazingira na wongofu wa kiekolojia: Huu ni muda wa toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuanza mchakato wa kuwa karibu zaidi na mazingira nyumba ya wote, Kitabu cha Mungu kilichofunguliwa na kuwa wazi mbele ya macho ya binadamu. Ni muda wa kutafakari kuhusu mtindo wa maisha, ili hatimaye, kufanya maamuzi magumu yatakayosaidia kuboresha utunzaji wa mazingira; kwa kuwa na teknolojia na nishati rafiki kwa mazingira na unabii! Baba Mtakatifu Francisko anasema taka za plastiki ni tishio kwa maisha ya viumbe hai. Watu wana wajibika kulinda na kutunza uhai wa viumbe vyote. Vijana waendelee kuwa mstari wa mbele katika utunzaji bora wa mazingira, kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni kati ya mambo yanayopelekea matumizi mabaya ya utajiri na rasilimali za nchi mbali mbali, kiasi kwamba, fursa za uongozi zinaelekezwa kwa ajili ya mafao binafsi badala ya kuwa ni chombo cha huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Leo hii utu, heshima na haki msingi za binadamu zinasiginzwa kutokana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Kumbe, kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira na ukiukwaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Cheche za mpasuko wa Kanisa na umuhimu wa unyenyekevu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema kukosoana kwa heshima ni sehemu ya mchakato wa ukuaji wa mtu katika ukweli, haki na upendo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna shutuma kutoka sehemu mbali mbali za dunia hata ndani ya Sekretarieti kuu ya Vatican, lakini ni mambo ambayo anayasikiliza na kuyapima kwa mizani ya ukweli na haki. Si mtu anayeshabikia “majungu kwani si mtaji”. Watu wajenge utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kufikia muafaka. Wale wanaotoa shutuma kwa kusema au kuandika, wawe pia na ujasiri wa kusubiri majibu kutoka kwa watuhumiwa. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Ikumbukwe kwamba, Kanisa lina Mapokeo, Sheria, Kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa. Kwenda kinyume cha mambo haya msingi yanayoliunganisha Kanisa, matokeo yake ni hayo ya baadhi ya viongozi wa Kanisa kushabikia “usasa” na kuanza kutoa Daraja Takatifu hata kwa wanawake. Kuna baadhi ya waamini wa Kanisa Katoliki ambao hawakukubaliana na mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kama Jumuiya ya Lefebvre, lakini, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu daima anawapatia waja wake uhuru unaowawajibisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko na anasali, ili kusiwepo tena kwa Kanisa kupasuka na kusambaratika, kwani hii ni hatari sana kwa maisha ya waamini kiroho. Kanisa katika maisha na utume wake, halina budi kujikita katika majadiliano yanayosimamiwa na ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya watu wa Mungu.

Katika maisha na historia ya Kanisa, daima wamekuwepo wazushi na wakanimungu, lakini sehemu kubwa ya watu wa Mungu wameendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kama ilivyotokea katika Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa wakatamka kwa unyenyenyekevu mkubwa kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu “Theotokos”. Hata Mtakatifu Yohane Paulo II alishutumiwa kuwa ni Mkomunisti kwa sababu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kukazia: Kanuni maadili; neema pamoja na kufahamu ubaya wa dhambi, ili kuambata na kukumbatia utakatifu unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Mchakato  wa amani na uchaguzi mkuu nchini Msumbiji, Oktoba 2019: Baba Mtakatifu anasema, ameamua kufanya hija ya kitume nchini Msumbiji wakati inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 15 Oktoba 2019, ili wadau mbali mbali waweze kuheshimu na kuthamini mchakato wa amani na upatanisho wa kidugu wakati wote wa kampeni, uchaguzi na kutangazwa kwa matokeo. Mchakato wa amani unapaswa kuimarishwa zaidi, kuliko hata uchaguzi ujao, kwa kukazia umoja na mshikamano wa kitaifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wakati wa hija yake ya kitume nchini Msumbiji amepata bahati ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali pamoja na viongozi wa Chama cha Upinzani, lengo ni kuendeleza mchakato wa umoja, upendo, upatanisho na mshikamano wa kitaifa!

Papa: Waandishi wa Habari
11 September 2019, 17:09