Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. 

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Jina Takatifu la B. Maria

Papa Francisko anasema, kila wakati kabla na baada ya hija yake ya kitume, amejijengea utamaduni wa kwenda kumshukuru Bikira Maria, Afya ya Warumi, kwa sababu ya ulinzi na tunza yake ya kimama wakati wote wa hija zake za kitume. Huwa anamwomba ushauri, maneno ya kuzungumza pale inapowezekana pamoja na kuratibu ishara na matendo yake. Ibada kwa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kweli waamini wanataka kuwa wafuasi amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa kuanzia sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini”.

Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kwa waamini na mahujaji waliofika mjini Vatican, Jumatano, tarehe 11 Septemba 2019 anasema, kila wakati kabla na baada ya hija yake ya kitume, amejijengea utamaduni wa kwenda kumshukuru Bikira Maria, Afya ya Warumi, kwa sababu ya ulinzi na tunza yake ya kimama wakati wote wa hija zake za kitume. Huwa anamwomba ushauri, maneno ya kuzungumza pale inapowezekana pamoja na kuratibu ishara na matendo yake. Kwa njia hii anapokwenda katika hija zake za kitume, anaondoka akiwa amejiamini kwamba, anaye Mama wa Mungu na Kanisa anayemsindikiza, aliyemlinda na kumtunza.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija ya kitume Barani Afrika itaweza kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani, haki, amani na upatanisho wa kidugu; sanjari na kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na  uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu alipowasili mjini Roma, Jumanne, tarehe 10 Septemba, 2019, moja kwa moja alikwenda kusali mbele ya Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi.

Papa: Jina la B. Maria

 

11 September 2019, 15:47