Papa Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kujikita katika mchakato wa upatanisho, msamaha, upendo na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Papa Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kujikita katika mchakato wa upatanisho, msamaha, upendo na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. 

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Upatanisho, Upendo na Msamaha!

Papa Francisko amekazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Msumbiji kujikita katika mchakato wa upatanisho ili kuondokana na vita, chuki na uhasama. Ni wakati wa kusamehe na kusahahu, ili kumwilisha Amri ya upendo inayovunjilia mbali kuta za utengano. Ni muda muafaka wa kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Amani ya kweli iko ndani ya mtu mwenyewe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu ambayo imeongoza hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Ijumaa, tarehe 6 Septemba, 2019 Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zimpeto uliosheheni watu kutoka sehemu mbali mbali za Msumbiji. Ni Ibada ya Misa ambayo imeacha gumzo katika maisha ya familia ya Mungu nchini Msumbiji. Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Msumbiji kujikita katika mchakato wa upatanisho ili kuondokana na vita, chuki na uhasama. Ni wakati wa kusamehe na kusahahu, ili kumwilisha Amri ya upendo inayovunjilia mbali kuta za utengano. Ni muda muafaka wa kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Amani ya kweli inabubujika kutoka katika undani wa mwamini mwenyewe!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amesema, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuwasikiliza na kuwapenda adui zao. Haya ni maneno ambayo yanapaswa kupewa uzito wa pekee hata na watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa kutambua na kuguswa na uhalisia wa maisha yao. Adui ni watu wanao wachukia na kuwatenga wengine; ni watu wanaowachafulia wengine utu na heshima yao pamoja na kuwakashfu jirani zao. Wananchi wengi wa Msumbiji bado wana madonda ya vita, chuki na uhasama. Ni madonda yanayowagusa hata watu wengine ambao tayari wamekwisha tangulia mbele za haki, lakini kuna wengine bado wako hai. Kuna hatari kwamba, madonda ya zamani yataibuliwa tena na hivyo kukwamisha maendeleo yaliyokwisha kupatikana hadi wakati huu kama ilivyojitokeza huko Cabo Delgado.

Kristo Yesu anataka wafuasi wake kufuata ile Njia ya Msalaba aliyoitumia katika kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa kuwakirimia msamaha wale waliomsaliti, waliomhukumu bila haki na hatimaye, wale wote waliomsubilisha na hatimaye, kufa kifo cha aibu Msalabani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, si rahisi kuzungumzia msamaha wakati ambapo bado kuna madonda ya vita, chuki na uhasama ambayo yako wazi. Hata katika muktadha huu, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kupenda na kujitahidi kuwa watu wema zaidi kwa kukubali msamaha na upatanisho na wala wasidhani Kanisa linapuuza uchungu na mahangaiko yao, ili kusahau kumbu kumbu. Lakini ushuhuda wa upatanisho una nguvu zaidi.

Yesu anawataka wafuasi wake kusamehe, kusahau na hata kuwaombea watesi wao, ili waweze kupata utimilifu wa maisha na wala si kuwaombea kifo; kwa kuwaheshimu na wala si kuwakashfu wala kulipiza kisasi, ili kujenga daraja jipya la amani. Huu ni utaratibu wa kiwango cha juu kabisa unaowekwa na Kristo Yesu kwa ajili ya wafuasi wake. Kamwe chuki na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, haitaweza kusaidia kujenga umoja wa familia, jamii na taifa katika ujumla wake. Ukosefu wa fursa sawa na matumizi ya silaha badala ya kuleta suluhu husababisha migogoro mipya na yenye madhara makubwa zaidi. Watu wanayo haki ya kuishi kwa amani, kwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza katika maisha yao “Kanuni ya Dhahabu” kwa kuwapenda wengine kama unavyotaka wao wakupende; kwa kuwasaidia na kutenda mema bila kungoja shukrani.

Baba Mtakatifu amekazia Amri ya Upendo inayowawezesha waamini kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu kwa kujikita zaidi na zaidi katika fadhila ya msamaha na huruma. Vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa itajikuta ikikumbatia utamaduni wa kifo kwa mauaji ya vikongwe, wagonjwa na walemavu, bila hata ya kuguswa na mahitaji wala mahangaiko ya jirani zao. Huu ni wakati muafaka wa kuachana na sera za chuki, uhasama na kutaka kulipizana kisasi, tayari kukumbatia mchakato wa upatanisho na amani. Wema na huruma ni fadhila za watu makini wanaowaheshimu na kuwathamini wengine kama kielelezo cha Unabii unaomwilisha katika huduma. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Msumbiji imebahatika kuwa na utajiri mkubwa na rasilimali nyingi, lakini bado wananchi wake wanasiginwa na kiwango cha juu kabisa cha umaskini.

Rushwa na ufisadi wa mali ya umma vinaendelea kuwatumbukiza wananchi katika majanga. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa ni mbegu ya matumaini, amani na upatanisho. Kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; wakati wa raha na shida! Si vizuri kuwatumia maskini kwa ajili ya faida ya mtu binafsi au kisiasa. Utamaduni wa watu kukutana utawawezesha wananchi wa Msumbiji kupandikiza mbegu na hata wao wenyewe kuwa ni vyombo vya amani na upatanisho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu wana kiu ya kutaka kuona kwamba, amani inapandikizwa katika akili na maisha ya watu pamoja na kuwa ni lengo la maisha kwa sasa na kwa siku za usoni. Amani ya Kristo Yesu iamue moyoni mwao kwa kuendelea kujikita katika njia ya amani, huruma, upendeleo kwa maskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Msumbiji kukumbatia njia ya amani.

Papa: Upatanisho
06 September 2019, 17:24