Tafuta

Papa Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia amekazia: amani, upatanisho, maendeleo na utunzaji bora wa mazingira. Papa Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia amekazia: amani, upatanisho, maendeleo na utunzaji bora wa mazingira. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Msumbiji! Hotuba kwa viongozi!

Papa amekazia: Umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu amewashukuru wananchi wa Msumbiji kwa mapokezi na ukarimu. Amewapongeza kwa utajiri wa tamaduni uoto wa asili, furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji & Upyaisho wa amani na upatanisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu amewasili nchini Msumbiji, Jumatano jioni tarehe 4 Septemba 2019 na kulakiwa na umati wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Msumbiji. Baba Mtakatifu ameianza siku yake ya pili ya hija yake ya kitume, Alhamisi tarehe 5 Septemba 2019 kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Msumbiji. Baadaye amemtembelea Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji pamoja na kubadilishana zawadi. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Msumbiji.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake ameonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji kutokana na majanga asilia. Amekazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa mapokezi na ukarimu wanaoendelea kumwonesha wakati wa hija yake nchini Msumbiji. Amewapongeza kwa utajiri wa tamaduni, uoto wa asili, furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Amewashukuru wadau wote waliojisadaka ili kupyaisha tena mchakato wa amani na upatanisho nchini Msumbiji.

Baba Mtakatifu amependa kuwaonesha uwepo wake wa karibu sanjari na mshikamano wa upendo kutokana na athari za majanga asilia yaliyosababishwa na Kimbunga cha Idai na Kenneth. Madhara yake kwa watu na mali zao, bado yanaonekana wazi na hasa katika maeneo ambayo yameharibika vibaya, kiasi kwamba, hayawezekani tena kufanyiwa ukarabati, maeneo haya yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee. Anasikitika kusema kwamba, hataweza kuwatembea wote, lakini watambue kwamba, anashiriki mateso na mahangaiko yao ya ndani. Jumuiya ya Kanisa Katoliki itaendelea kujibu changamoto hizi kwa hali na mali. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wadau mbali mbali watachangia katika ujenzi wa maeneo yaliyoathirika kwa majanga haya asilia.

Baba Mtakatifu anaipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imesimama kidete ili kuhakikisha kwamba mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa, licha ya matatizo na changamoto zake, unarejea tena na matokeo yake ni kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Amani huko Serra da Gorongosa kati ya Chama cha FRELIMO na RENAMO. Mkataba huu unafutilia mbali uhasama kati ya ndugu wamoja nchini Msumbiji na kwamba, Mkataba huu utaimarisha zaidi Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi mjini Roma kunako mwaka 1992. Matunda ya mchakato huu yameanza kuonekana kwa kutambuana kama ndugu, wenye dhamana na wajibu wa kuendeleza ustawi wa nchi ya Msumbiji.

Ujasiri unaleta amani ya kweli, unatafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi. Wananchi wa Msumbiji wameteseka sana na madhara ya vita na kinzani za kijamii, lakini hawakutaka kukubali kutawalia na chuki, uhasama na mtindo wa kutaka kulipizana kisasi na kwamba, vita haikuwa na usemi wa mwisho katika mustakabali wa wananchi wa Msumbiji. Vita imeharibu sana makazi ya watu, imewatumbukiza wananchi katika baa la njaa, ujinga na maradhi. Vita imewakosesha watu nyumba za sala na ibada; imepelekea watu kukosa fursa za ajira na kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi wa Msumbiji walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama na hifadhi ya maisha yao.

Huu ni wakati wa kukumbatia amani na kuachana kabisa na falsafa ya mtutu wa bunduki. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mchakato wa kutafuta amani ya kudumu ni endelevu na unajikita katika ukweli na uwazi; ujasiri na unyenyekevu pasi na baadhi ya watu kutaka kujikweza. Ni mchakato unaofumbatwa katika ushupavu ili kukuza na kudumisha amani na upatanisho, kwani vita inaleta maafa kwa watu na mali zao. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha hasa wale ambao wamepewa dhamana ya uongozi ili kuhakikisha kwamba wanalinda: utu na heshima ya ndugu zao ili hata wao pia wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa maendeleo kwa mustakabali wa nchi yao.

Ili kudumisha amani ya kweli, kuna haja ya kujenga mazingira ya haki na usawa ili kuondokana na vurugu na migongano inayoweza kupelekea jamii kulipuka kwa vita na misigano ya kijamii. Kukosekana kwa usawa kutawafanya wale waliotengwa kujibu “mapigo” kwa ghasia. Kupatikana kwa amani nchini Msumbiji kumepelekea maboresho makubwa katika sekta ya elimu na afya na kwamba, kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo fungamani ya binadamu na asiwepo hata mtu mmoja atakaye achwa nyuma katika maendeleo. Baba Mtakatifu anasema, vijana wapewe kipaumbele cha kwanza kwani wao wanaunda sehemu kubwa ya familia ya Mungu nchini Msumbiji. Changamoto mamboleo, ziwabidiishe kutumia vipaji vyao vya ubunifu, hawa ni mbegu iliyopandikizwa tayari, wakipewa fursa, watachangia mchakato wa ukuaji wa jamii unaotakiwa na wengi.

Ikumbukwe kwamba, utamaduni wa amani ni mchakato endelevu unaopaswa kuwashirikisha hata vijana wa kizazi kipya; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Kumbe, utulivu ni hitaji muhimu, ili kuweza kufikia malengo yaliyobainishwa, nguvu msingi za maisha na mawazo yanayofyekelea mbali ile tabia ya kudhaniana vibaya. Utajiri mkubwa nchini Msumbiji unapaswa kuwa ni huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuhakikisha kwamba, wanapata elimu makini, makazi bora zaidi pamoja na fursa za ajira. Sanjari na haya, wakulima wawe na mashamba kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Huu ni msingi wa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi na silaha madhubuti ya amani ya kudumu! Ni katika muktadha huu, Msumbiji inapaswa pia kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba yote, kama njia ya kulinda uhai. Ardhi iwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, amani ya kudumu inafumbatwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaambia viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Msumbiji kwamba, wao wote ni wasanii katika ujenzi wa haki na upatanisho wa kidugu nchini Msumbiji; kwa kulinda haki na amani kwa ajili ya watoto wao. Muda huu anapenda pia kuutumia kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Maaskofu Katoliki kwani Kanisa limekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa kutafuta amani, upatanisho na matumaini.

Papa: Diplomasia
05 September 2019, 15:29