Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika hotuba yake amekazia: Majadiliano; Wahamiaji, Demokrasia na Uchumi fungamani unaojalia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Francisko katika hotuba yake amekazia: Majadiliano; Wahamiaji, Demokrasia na Uchumi fungamani unaojalia utu, heshima na haki msingi za binadamu.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Mauritius: Uchumi fungamani

Baba Mtakatifu amekazia zaidi kuhusu: Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa kuendeleza demokrasia shirikishi pamoja na kuendelea kujikita katika sera na mikakati ya uchumi ufungamani unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu ambayo imeongoza hija ya Baba Francisko nchini Mauritius kuanzia Jumatatu tarehe 9 hadi Jumanne 10 Septemba 2019 ni “Hujaji wa amani”. Mara baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, Jumatatu tarehe 9 Septemba 2019, Baba Mtakatifu amepata chakula cha mchana na Baraza la Maaskofu Katoliki Bahari ya Hindi, “CEDOI” lililoanzishwa kunako mwaka 1985 na kwa sasa linaundwa na Maaskofu watano ambao pia ni wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM. Papa Francisko amepata pia fursa ya kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Père Laval, yaliyozinduliwa kunako mwaka 2014 wakati wa Jubilei ya Miaka 150 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Jacques Dèsirè Laval, aliyejisadaka kwa ajili ya uinjilishaji wa kina nchini humo. Kila mwaka ifikapo tarehe 9 Septemba anakumbukwa na Kanisa mahalia. Baba Mtakatifu Francisko jioni amepata pia nafasi ya kukutana na kusalimiana na wagonjwa pamoja na ndugu na jamaa zao.

Baba Mtakatifu alikamilisha siku ya Jumatatu nchini Mauritius kwa kukutana na kuzungumza na: viongozi wa Serikali na kidini wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Mauritius. Kabla ya kukutana na viongozi hawa, Baba Mtakatifu alimtembelea Ikulu Bwana Barlen Vyapoory kwa faragha na kusalimiana naye pamoja na familia yake. Amekutana pia na Waziri mkuu wa Mauritius Rais Pravind Kumar Jugnauth na baadaye wote hawa wakaongozana kuekelea kwenye ukumbi ambamo Baba Mtakatifu amepata fursa ya kuzungumza na viongozi pamoja na wanadiplomasia wanaoziwalisha nchi zao huko Mauritius. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia zaidi kuhusu: Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa kuendeleza demokrasia shirikishi pamoja na kuendelea kujikita katika sera na mikakati ya uchumi ufungamani unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi na watu wa Mungu nchini Mauritius, wanaotoka katika tamaduni, makabila, dini na imani mbali mbali. Licha ya tofauti hizi msingi, bado familia ya Mungu nchini Mauritius inaendelea kushuhudia uzuri wa maisha ya pamoja katika misingi ya amani, utulivu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hiki ni kiini cha historia ya watu wa Mungu nchini Mauritius ambao wengi wao ni wale wanatoka katika kizazi cha wahamiaji, waliofika Kisiwani humo wakiwa wamesheheni: tamaduni, imani, mila na desturi zao, lakini wakajifunza kutajirishana na jirani zao, kiasi cha kuishi na kujenga udugu wa kibinadamu kwa ajili ya mafao ya wengi. Ni katika muktadha wa tofauti zao msingi, wameweza kujenga na kudumisha amani kwa kutambua kwamba, tofauti ni jambo jema inapoweza daima kuingia kwenye mchakato wa upatanisho, na matokeo yake ni “tofauti iliyopatanishwa”. Huu ni msingi na fursa ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa familia kubwa ya kibinadamu bila kuwatenga watu.

Baba Mtakatifu anasema, historia na kumbu kumbu ya familia ya Mungu nchini Mauritius inafumbatwa katika vinasaba vya wahamiaji na wakimbizi, waliojikita katika ujenzi wa amani na utulivu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ndiyo changamoto ya kuendelea kukita maisha yao kwenye mizizi ya asili; kwa kukubali kupokea changamoto ya kuwakaribisha wahamiaji, kwa kuwalinda wahamiaji wanaotafuta kazi na fursa za maisha bora zaidi kwa ajili yao binafsi na familia zao. Wananchi wa Mauritius wawe na ukarimu kama ule uliooneshwa na mababu zao, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini utu na haki zao msingi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza wananchi wa Mauritius kwa kujenga utamaduni wa demokrasia shirikishi tangu walipojipatia uhuru wa bendera, kiasi kwamba, Mauritius kimekuwa ni Kisiwa na amani. Mwelekeo huu wa kidemokrasia unapaswa kukuzwa na kudumishwa, kwa kufyekelea mbali mbali mifumo yote ya ubaguzi.

Hii inatokana na ukweli kwamba,siasa ya kweli inajikita katika majadiliano pamoja na kutambua thamani ya kila mtu, chemchemi na nguvu mpya ya mafungamano ya kiakili, kitamaduni na kiroho. Viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa na wananchi wao wanaowategemea, lakini zaidi vijana wa kizazi kipya. Viongozi wa kisiasa wasimame kidete kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma; wajipambanue kwa huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili waweze kuaminiwa na wananchi wao. Mauritius tangu ilipojipatia uhuru wake wa bendera imeendelea kucharuka katika ukuaji wa uchumi, ingawa si kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Kuna idadi kubwa ya vijana wa kizazi kipya ambao hawana fursa za ajira. Kumbe, hapa kunahitaji maamuzi, mipango, mifumo na michakato maalum kwa ajili ya ugavi bora wa mapato, ubunifu wa vyanzo vya ajira pamoja na mapambano dhidi ya umaskini kwa kujenga uchumi fungamani.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi kuondokana na kishawishi cha ujenzi wa mfumo wa uchumi unaojikita katika faida kubwa na matokeo yake ni wananchi kuwa na hali ngumu ya maisha, kiasi hata cha kushindwa kuwalinda na kuwatetea maskini. Mfumo kama huu anasema Baba Mtakatifu, unachangia pia uharibifu wa mazingira pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa nchi. Hapa kuna umuhimu wa familia ya Mungu kujikita katika wongofu wa kiekolojia, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kubadili mtindo wa maisha, ili ukuaji wa uchumi uweze kuwanufaisha wote bila kulitumbukiza taifa katika majanga asilia au kusababisha machafuko makubwa ya kijamii. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ameridhishwa na mchakato wa majadiliano ya kidini unavyoendeshwa nchini Mauritius kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Majadiliano haya yamekuwa ni msingi wa amani jami inayothamini na kujali utu na heshima ya binadamu.

Kanisa Katoliki nchini Mauritius litaendelea kujielekeza katika mchakato wa majadiliano ya kidini ili kudumisha historia hii inayofumbatwa katika ushuhuda. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Mauritius na anawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili jitihada za ujenzi wa utamaduni wa watu kutoka tamaduni, staarabu, dini na imani kuweza kukutana ili kudumisha jamii inayosimikwa katika haki na ambayo kamwe haiwezi kuwasahau watoto wake, hasa wale maskini.

Papa: Hotuba

 

10 September 2019, 15:06