Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amefafanua kuhusu umuhimu na utume wa mashirika ya utawa wa ndani kwamba: Watawa hawa ni kielelezo cha faraja, ukarimu na mbereko wasafiri kuelekea mbinguni. Papa Francisko amefafanua kuhusu umuhimu na utume wa mashirika ya utawa wa ndani kwamba: Watawa hawa ni kielelezo cha faraja, ukarimu na mbereko wasafiri kuelekea mbinguni.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Watawa wa ndani: Utume: Sala, Faraja & Ushuhuda

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Ushuhuda, amana na utajiri wa maisha ya kitawa; umuhumi wa sala; Monasteri kama faraja kwa maskini; utume wa sala katika mchakato wa uinjilishaji na sala inayomwilishwa katika matendo kama kielelezo cha imani thabiti. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza watawa wote wa Mashirika ya ndani kwa utume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Madagascar, Jumamosi, tarehe 7 Septemba 2019 amepata nafasi ya kusali Sala ya Adhuhuri kwenye Monasteri ya Wakarmeli wa ndani. Watawa 100 kutoka katika mashirika ya watawa wa ndani walikuwa ndani ya Kanisa na nje ya Kanisa kulikuwepo na Wanovisi 70 wanaojiandaa kujisadaka katika huduma kwa Mungu na jirani zao katika maisha ya kuwekwa wakfu. Baada ya masifu ya adhuhuri, Baba Mtakatifu ametabaruku Altare ya Kanisa kuu la Jimbo la Morondava. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Ushuhuda, amana na utajiri wa maisha ya kitawa; umuhumi wa sala; Monasteri kama faraja kwa maskini; utume wa sala katika mchakato wa uinjilishaji na sala inayomwilishwa katika matendo kama kielelezo cha imani thabiti.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza watawa wote wa Mashirika ya ndani kwa kuendelea kuungana naye katika maisha na utume wa Kanisa zima, lakini zaidi na Kanisa nchini Madagascar. Nchi hii inasiginwa sana na umaskini, lakini imesheheni utajiri unaobubujika kutoka katika kazi ya uumbaji, rasilimali watu pamoja na utajiri wa maisha ya kiroho: haya ni mambo ambayo watawa wa Mashirika mbali mbali wanayashuhudia. Baba Mtakatifu anasema, Zaburi ya 119 ni ndefu kuliko Zaburi zote na inazungumzia kuhusu Sifa za Sheria ya Mungu; inaonesha mang’amuzi ya uzuri wa sala kwa mwamini aliyevunjika na kupondeka moyo; anayetamani kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Hii ni kiu ya watu wa Mungu na kwamba, maisha ya taamuli yanazima kiu ya matamanio ya ndani. Wao ni dira na mwongozo wa jumuiya ya waamini wanaosafiri, ili kufikia utimilifu, siku ambayo Kristo Yesu atakua yote katika yote ili kutangaza utukufu wa mbinguni.

Watawa wa ndani watambue kwamba, walimwengu wanawapenda na kuwathamini, kwani kwa sala na maombi yao, wanatambua kwamba, wanaweza kufika salama salimini mbinguni. Watawa wa ndani waendelee kuwa ni nguzo imara kwa jirani zao wa karibu na wale walioko mbali. Wawe ni taa angavu kwa watu wanaosafiri katika giza na utupu wa maisha; kwa mfano wa maisha na ukimya ili mwisho wa siku, watu wafurahie ushuhuda wa maisha na utume wao Watawa wa ndani ni kielelezo cha ukarimu na faraja kwa watu wanaoteseka na kuelemewa na mizigo ya maisha. Ni mahali pa kujenga na kukuza utamaduni wa kusikiliza kwa makini ili watu waweze kupata faraja, amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu anawataka watawa kusikiliza kwa makini kilio cha watu wanaoteseka, wanaodhulumiwa na kukata tamaa.

Watawa wa ndani wana utume maalum wa sala kwani wao wanayo nafasi ya pekee mbele ya Mwenyezi Mungu na wengi wanawatambua kuwa wawakilishi wao mbele ya Mwenyezi Mungu na chemchemi ya faraja ili kusonga mbele kwa imani na matumaini. Kuna watu ambao wamepoteza imani na matumaini; wanajisikia watu pweke sana; wanaomkimbilia Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili aweze kuwasikiliza na hatimaye, kujibu kilio chao, kwani Mwenyezi Mungu ni mwamba wa usalama wa maisha yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sala ni amana na utajiri mkubwa kwa maskini. Hawa ni watu wanaotaka kuona imani ikimwilishwa katika matendo, ili kuishi kwa matumaini zaidi. Mafumbo ya maisha ya Mungu yanafumbatwa katika Vipindi vya Liturujia ya Sala ya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo watu wanaweza kugundua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao.

Kwa njia ya sala zao, watawa wanakuwa ni mbereko ya kuwabebea watu wanaosafiri kwenda kwenye nchi ya ahadi. Tafakari ni muhimu sana katika kukoleza mchakato wa utakatifu wa maisha. Sala ni kielelezo cha mshikamano na upendo wa kidugu. Watawa wa ndani ni mashuhuda na vyombo vya mchakato wa uinjilishaji. Ni chachu inayopyaisha maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuwa ni sadaka inayowawezesha kushirikishana Fumbo la Ukombozi nchini Madagascar. Watawa wa ndani ni kama kiriba cha moto; watu wanaoteketea kutokana na magumu ya ulimwengu mamboleo, lakini kwa upande mwingine wanateketea kwa ajili ya upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa kamwe wasishiriki maisha ya sala kwa mazoea tu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kujiaminisha kwa sala na sadaka zao. Amewabeba katika sakafu ya moyo wake kwa ajili ya nia njema alizojiwekea wakati huu wa hija yakitume Barani Afrika.

Papa: Wamonaki

 

 

07 September 2019, 16:55