Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa vijana amewaweka vijana wote chini Madagascar chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa vijana amewaweka vijana wote chini Madagascar chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Ulinzi wa B. Maria

Papa Francisko anamshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake; anapenda kumkabidhi vijana hawa ambao wana upendeleo wa pekee machoni pa Mungu. Bikira Maria anatambua matatizo, changamoto na matamanio yao halali; bpamoja na makwazo yanayoweza kukwamisha malezi yao katika ulimwengu wa utandawazi uliochafuliwa na kugubikwa na utamaduni usiojali watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Mkesha na vijana, Jumamosi, tarehe 7 Septemba 2019 amewaweka wakfu vijana wote wa Madagascar chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi na mlinzi wa Madagascar. Baba Mtakatifu anamshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama na sasa anapenda kumkabidhi vijana hawa ambao wana upendeleo wa pekee machoni pa Mungu. Bikira Maria anatambua matatizo, changamoto na matamanio yao halali; bila kusahau makwazo yanayoweza kukwamisha malezi na makuzi yao katika ulimwengu wa utandawazi uliochafuliwa na kugubikwa na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria awaombee kwa Mungu ujasiri na matumaini; awaongoze kwenda kwa Kristo Yesu, ili awakirimie nguvu ya kusonga mbele katika safari na utakatifu wa maisha.

Bikira Maria awasindikize vijana wa Madagascar ili waweze kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu; awalinde dhidi ya vishawishi vya kukata tamaa na uhalifu wa kutumia nguvu. Bikira Maria katika sala na maombezi yake, apende kuwaimarisha vijana wa Madagascar kuwa na kiu ya kutaka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo fungamani nchini mwao, kwa kujizatiti kupambana na umaskini, ujinga na utengano. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyekwenda kwa haraka kumtembelea binamu yake Elizabeth, awasaidie pia vijana wa Madagascar kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na upendo wa Kristo kwa waja wake. Vijana wawe na ujasiri wa kutambua asili yao kwa kuchota hekima kutoka kwa wazee; wawe ni wajenzi wa madaraja kati ya watu ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki na udugu wa kibinadamu.

Bikira Maria ambaye ni chemchemi ya sala kati ya kundi kubwa la vijana waliokuwasanyika, awaombee kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaangaza na kuwaongoza. Mwanga wa Pentekoste upyaishe maisha ya ujana wao, ili kweli waweze kuwa mashuhuda wa Injili katika maisha na hatimaye, waweze kumtangaza Kristo Yesu ambaye ni kijana milele yote. Awabariki, awalinde na kuwaimarisha vijana wa Madagascar ili wawe ni mitume wamisionari wa Kristo Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria aweze kusikiliza sala yao na kuwajalia vijana wa Madagascar kuwa wapanzi wa matumaini, amani na furaha ya mbeleni, yote haya yawe ni kwa ajili ya utukufu wa Mwenyezi Mungu, ustawi, mafao na maendeleo ya wananchi wa Madagascar.

Papa: Ulinzi wa Bikira Maria

 

08 September 2019, 16:30