Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru watu wa Mungu nchini Madagascar kwa wema, ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wote wa hija yake nchini mwao! Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru watu wa Mungu nchini Madagascar kwa wema, ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wote wa hija yake nchini mwao!  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Shukrani za dhati!

Mama Bikira Maria ambaye Jumapili tarehe 8 Septemba 2019, Kanisa linaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake na huo ukawa ni mwanzo wa kupambazuka kwa wokovu wa wanadamu, Baba Mtakatifu amemwomba Mama Mtakaifu wa Mungu ambaye anaheshimiwa na kuadhimishwa kama Msimamizi wa Madagascar, alilinde taifa la Madagascar katika njia ya matumani na amani.

Na Padre Angelo Shikombe – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 8 septemba 2019 baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Soamandrakizay wa Jimbo kuu Katoliki la Antananarivo, Madagascar na baada ya sala ya Malaika wa Bwana, amewashukuru taifa la Mungu na wananchi wote wa Madagascar kwa mapokezi na ukarimu mkubwa waliomuonesha wakati wa ujio wake nchini humo. Akitoa neno lake la shukrani mwishoni mwa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko, amemshukuru Askofu mkuu Odoni Marie Arsène Razanakolona na Maaskofu wengine nchini Madagascar kwa utme wanaoufanya wa kulichunga kundi la Bwana.  Baba Mtakatifu akiwashukuru wote waliohudhuria ibada hiyo ya Misa Takatifu akiwemo  Rais Andry Rajoelina, na viongozi wengine wa Serikali,  wakleri, watawa, wenye maisha ya wakfu, makatekista na watu wote wa Taifa la Mungu; amewashukuru pia wananchi wote wa Madagascar kwa ukarimu na furaha waliyomwonesha yenye kudokeza tumaini kubwa walilonalo katika maisha ya imani, na upendo unaojifunua katika ushirikiano wao unaoeleza uhai na uwepo wa Mungu kati yao.

Aidha Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa vyama vya kiraia na serikali  kwa moyo wao wa ukarimu katika kumkaribisha na kufanikisha safari yake ya uinjlishaji Nchini humo.  Kutoka katika kina cha moyo wake, Baba Mtakatifu amewatakia baraka na neema za Mwenyezi Mungu.  Kwa maombezi ya Mwenye heri Rafaeli Louis Rafiringa, na Mwenye heri Victoria Rasoamanarivo  ambaye masalia yake yalikuwepo kwenye Altare hiyo, ameiweka Nchi ya Madagascar chini ya ulinzi na maombezi yao. Akiendelea kumwomba Mama Bikira Maria ambaye Jumapili tarehe 8 Septemba 2019, Kanisa linaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake  na huo ukawa ni mwanzo wa kupambazuka kwa wokovu wa wanadamu, Baba Mtakatifu amemwomba Mama Mtakaifu wa Mungu ambaye anaheshimiwa na kuadhimishwa kama Msimamizi katika altare hiyo  kulilinda taifa la Madagascar na familia yote ya Mungu katika njia ya matumani na amani.

Wakati huohuo, kwa upande wa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar, na taifa la Mungu nchini Madagascar, wakiwakilishwa na Askofu mkuu  Razanakolona wa Jimbo Kuu la Antananarivo , wametoa shukrani zao kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali kulitembelea Taifa la Mungu na wananchi wote wa Madagascar. Akiwa amejawa furaha isiyokifani, Askofu Mkuu Razanakolona amesema, hakuna neno linaloweza kuilezea furaha waliyonayo Taifa la Mungu na wanachi wa Madagascar kwa   heshima kubwa na fursa waliyopewa na Baba Mtakatifu Francisko ya kufika katika Nchi ya Madagascar “Terra Rossa”, na kupanda mbegu ya amani, na matumanini, akiwaimarisha ndugu zake katika imani, na mapendo. Aidha Askofu mkuu Razanakolona amemshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaasa kutunza amani na kuwataka wawe na na bidii katika kumtafuta Mungu, wakiishi mashauri ya ufukara wa Kiinjili. 

Sambamba na shukrani hizo, Askofu mkuu Razanakolona ameeleza bayana furaha na amani waliyonayo wanamadagascar iliyopyaishwa kwa ujio wake na uinjilishaji wa kina alioufanya kwa taifa la Mungu, na hapohapo kumhakikishia kuwa, wameyapokea kwa furaha mafundisho ya kitume aliyowaasa katika ujio wake na zaidi sana kujifunza kwa unyenyekevu wake na  mfano hai wa utumishi aliouonesha kwa watu waliomaskini walioko nchini Madagascar.  Katika kumshukuru huko Askofu mkuu Razanakolona hakusahau kumpongeza na kumwahidia ushirikiano wa karibu katika sala na utumishi wa kitume ambao kwao utume wa Kanisa umesimikwa.

[ Audio Embed Madagascar: Shukrani]  

08 September 2019, 17:37