Vatican News
Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika inapania pamoja na mambo mengine kuimarisha mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika inapania pamoja na mambo mengine kuimarisha mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha. 

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Uinjilishaji & Ushuhuda

Papa anataka kuwatangazia furaha ya Injili inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Msumbiji tangu ijipatie uhuru wake, imeendelea kuogelea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyopelekea maelfu ya wananchi wa Msumbiji kutafuta hifadhi, usalama na ustawi kwa nchi jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Jumatano tarehe 4 Septemba 2019 anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja na naye, ili kumtolea Mwenyezi Mungu, Baba wa wote sala, ili aweze kuimarisha upatanisho wa kidugu; matumaini na amani ya kweli na inayodumu Barani Afrika. Hii ni hija ya nne ya kitume inayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika. Itakumbukwa kwamba, kuanzia tarehe 24- 30 Novemba 2015 alitembelea: Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Mwezi Machi 2017 akatembelea Morocco na Mwezi Aprili 2019 ametembelea Misri. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwezi Oktoba 2019 ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ni muda wa kusali na kutafakari kuhusu utume kama msingi wa mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa.

Kwa hakika hiki ni kipindi cha ushuhuda wa huruma na upendo Mungu unaaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mwezi Oktoba 2019 Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”.  Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linapaswa kujiekeleza zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji! Ni katika muktadha huu, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika inalenga kukoleza ari na moyo wa kimisionari katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi ili kukoleza moyo wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Kama ilivyokuwa wakati wa hija yake ya kwanza Barani Afrika kunako mwaka 2015, akiwa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, akatangaza Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Wakati huu anataka kuzima kiu ya Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika katika haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Anataka kuwatangazia furaha ya Injili inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Msumbiji tangu ijipatie uhuru wake, imeendelea kuogelea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyopelekea maelfu ya wananchi wa Msumbiji kutafuta hifadhi, usalama na ustawi kwa nchi jirani. Kumekuwepo na wimbi kubwa la majanga asilia, umaskini na magonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwa ni mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho wa kidugu nchini Msumbiji. Ni matumaini ya familia ya Mungu nchini Msumbiji kwamba, hija hii ya kitume, itasaidia pia kukuza mchakato wa demokrasia shirikishi, ili hatimaye, uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Msumbiji hapo tarehe 15 Oktoba 2019 uweze kuwa huru, wa haki na amani, hatua kubwa katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na kuwarejeshea matumaini vijana wa kizazi kipya, tayari kujikita katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Upatanisho wa kidugu katika ukweli na uwazi ni ufunguo wa haki na amani nchini Msumbiji.

Askofu Diamantino Guapo Antunes wa Jimbo Katoliki la Tete, Msumbiji anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji inalenga kuwaimarisha watu wa Mungu katika mchakato wa matumaini, amani na upatanisho. Wananchi wengi wa Msumbiji wanampenda Baba Mtakatifu Francisko kutokana na majitoleo yake kama sauti na mtetezi wa wanyonge, chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu pamoja na kuendelea kujipambanua kama kiongozi anayetetea mchakato mzima wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.Sehemu ya Pili ya Hija ya Baba Mtakatifu Francisko ni Madagascar ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imepia hali ngumu ya kisiasa na mipasuko ya kijamii; rushwa na ufisadi wa mali ya umma; pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa Katoliki limeendelea kuwa ni chombo makini cha uinjilishaji wa kina, kwa kujikita zaidi katika huduma ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Nahtimisho la hija yake ni nchini Mauritius.

Papa: Uinjilishaji
04 September 2019, 15:25