Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya kitume barani Afrika, amejikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi. Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya kitume barani Afrika, amejikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi. 

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Ulinzi & tunza ya B. Maria

Kama ilivyo ada, Baba Mtakatifu, Jumanne asubuhi, tarehe 3 Septemba, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Gregori Mkuu, amekwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi. Hija ya Baba Mtakatifu inapania kukoleza: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano asubuhi anatarajiwa kuanza hija ya thelathini na moja ya kitume ya Barani Afrika kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius, kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2016. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Kama ilivyo ada, Baba Mtakatifu, Jumanne asubuhi, tarehe 3 Septemba, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Gregori Mkuu, amekwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi.

Hija ya Baba Mtakatifu Barani Afrika pamoja na mambo mengine kimsingi inapania kukoleza mchakato wa amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na familia ya Mungu Barani Afrika kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka mjini Roma saa 2:00 za asubuhi na kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maputo majira ya saa 12:30 jioni ambako atafanyiwa mapokezi ya kitaifa.

Alhamisi, tarehe 5 Septemba 2019, Baba Mtakatifu atamtembelea Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji pamoja na kufanya naye mazungumzo ya faragha. Baadaye, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia, viongozi wa kisiasa pamoja na vyama vya kiraia. Itakumbukwa kwamba, majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kuzungumza na vijana kutoka dini na madhehebu mbali mbali nchini Msumbiji, ili kuwaimarisha katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama sehemu pia ya mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya vita na kinzani, zilizoipekenya Msumbuji kwa miaka zaidi ya kumi na mitano.

Baada ya chakula cha mchana kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Msumbiji, Baba Mtakatifu Francisko, Alasiri atakutana na kuzungumza na Maaskofu, Mapadre, Watawa, Makatekista, Waseminari pamoja na walezi wao kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji. Na kwa tukio hili, Baba Mtakatifu atakuwa anahitimisha siku yake ya pili nchini Msumbiji. Ijumaa, tarehe 6 Septemba 2019, Baba Mtakatifu asubuhi kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zimpeto, atatembelea Hospitali ya Zimpeto na kusalimiana na wagonjwa. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu atakuwa amemaliza hija yake ya kitume nchini Msumbiji kama hujaji wa matumaini, amani na upatanisho.

Papa: Bikira Maria
03 September 2019, 17:04