Papa Francisko asema kijiji cha Akamasoa ni jibu la kilio na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Madagascar. Papa Francisko asema kijiji cha Akamasoa ni jibu la kilio na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Madagascar. 

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Mji wa Akamasoa ni wimbo wa imani na matumaini

Hiki ni kilio cha watu wasiokuwa na makazi; kilio cha watoto wanaozama katika dimbwi la ujinga, njaa na utapiamlo wa kutisha; kilio cha umati mkubwa watu wasiokuwa na fursa za ajira; watu wanaodhalilishwa na kutezwa; kilio cha watu wasiokuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kila shule na kituo cha zahanati eneo la Akamasoa ni wimbo wa imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Madagascar, Jumapili tarehe 8 Septemba 2019 alipata nafasi ya kutembelea Jumuiya ya Akamasoa, maarufu kama “Mji wa urafiki”, kielelezo cha uwepo wa Mungu ambaye ameamua kubaki kati ya waja wake. Huu ni mji ambao umejengwa kwa jasho na mikono yao wenyewe ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Hii ni fursa ya kumshukuru Mungu anayesikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa njia ya upendo na mshikamano kutoka kwa Wasamaria wema. Hiki ni kilio cha watu wasiokuwa na makazi; kilio cha watoto wanaozama katika dimbwi la ujinga, njaa na utapiamlo wa kutisha; kilio cha umati mkubwa watu wasiokuwa na fursa za ajira; watu wanaodhalilishwa na kutezwa; kilio cha watu wasiokuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kila shule na kituo cha zahanati eneo la Akamasoa ni wimbo wa matumaini unaotaka kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu anasema, umaskini si kifo! Kijiji cha Akamasoa ambacho kwa sasa umegeuka kuwa ni mji ni matokeo ya historia ya ujasiri na mshikamano wa upendo na kazi ngumu iliyosukumwa na imani iliyomwilishwa katika matendo, kiasi hata cha kuweza kuhamisha mlima! Mahali ambapo palionekana kuwa ni shimo la taka na hali ngumu ya maisha, pamekuwa ni chemchemi ya matumaini na maisha mapya yanayotangazwa na kushuhudia na watu waliokuwa wamekufa na sasa wamefufuka. Hii ni imani ambayo iliyomwilishwa katika matendo. Hii ni kazi ambayo imefanyika kwa mtazamo wa kifamilia na kijumuiya; katika hali ya uvumilivu na kuaminiana, kiasi cha kumwezesha kila mtu kuwa ni mdau katika ujenzi wa “Mji wa urafiki”. Padre Pedro Opeka akawa ni muasisi wa elimu makini, ili kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kujiheshimu wao wenyewe, nidhamu, uaminifu, kuwajali pamoja na kuwaheshimu jirani zao, kwa kutambua kwamba, ndoto ya Mungu ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao si tu kwa ajili ya mtu mmoja, bali kwa ajili ya Jumuiya ya watu.

Ubinafsi ni utumwa uliokithiri. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Akamasoa kutokubali “kupigishwa magoti na kunyenyekeshwa na umaskini” wala kutafuta njia ya mkato katika maisha au kujitafuta wao wenyewe. Vijana wanapaswa kuendeleza kazi hii kubwa iliyofanywa na wazee wao kwa nguvu ya imani na ushuhuda hai waliorithishwa katika maisha. Vijana wawe na ujasiri wa kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, kielelezo na mfano bora wa kuigwa kwa sasa na kwa siku za usoni. Kazi ya Mungu iwe ni kielelezo cha ushuhuda wa upendo kwa kizazi hiki na kile kijacho. Mwishoni wa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amesali kwa ajili ya kuombea Madagascar ili mwanga huu wa Injili ya maendeleo fungamani ya binadamu, usaidie mchakato wa kupambana na umaskini na hivyo kujenga jamii inayosimikwa katika mahusiano fungamani ya binadamu; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ushuhuda wa kinabii unaowaletea watu matumaini katika maisha!

Papa: Hotuba: Akamasoa

 

09 September 2019, 17:43