Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa vijana amewaambia kwamba, wao ni matumaini ya Madagascar na Kanisa katika ujumla wake wajibidiishe kuwa watu wema zaidi! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa vijana amewaambia kwamba, wao ni matumaini ya Madagascar na Kanisa katika ujumla wake wajibidiishe kuwa watu wema zaidi!  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Injili ya matumaini

Papa Francisko amewataka vijana kumtafuta Kristo Yesu kwa njia ya huduma; wajitahidi kuwa ni watu wema zaidi, kwani Kristo Yesu anaishi na anawataka vijana nao kuishi kikamilifu, kwa kutambua kwamba wao ni matumaini ya Madagascar na Kanisa. Vijana wanaitwa kuwa mitume wamisionari wa Yesu na watambue kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu inayowajibikiana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani na matumaini”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 7 Septemba 2019 ameongoza mkesha wa bahari ya vijana kutoka ndani na nje ya Madagascar. Mkesha huu umefanyika kwenye Uwanja wa michezo Soamandrakizay unaomilikiwa na Jimbo kuu la Antananarivo. Katika mkesha huu, Baba Mtakatifu amesikiliza kwa makini shuhuda mbali mbali zilizotolewa na vijana wa Madagascar kuhusu matumaini na changamoto mbali mbali wanazokaliana nazo katika maisha. Ameshuhudia sanaa za maonesho kutoka kwa vijana wa Madagascar, kielelezo cha furaha na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewataka vijana kumtafuta Kristo Yesu kwa njia ya huduma makini; wajitahidi kuwa ni watu wema zaidi, kwani Kristo Yesu anaishi na anawataka vijana nao kuishi kikamilifu, kwa kutambua kwamba wao ni matumaini ya Madagascar na Kanisa katika ujumla wake.

Vijana wanaitwa kuwa mitume wamisionari wa Yesu na watambue kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu inayowajibikiana! Baba Mtakatifu amewashukuru vijana wote waliotoa shuhuda na changamoto za maisha na kwamba, Kristo Yesu anawapatia marafiki zake mitume neema na baraka za kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini. Hata vijana wanapaswa kujizatiti kwa kutenda zaidi, kwani Kristo Yesu daima anawasindikiza katika safari ya maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka vijana kumtafuta Kristo Yesu katika maisha yao, ili aweze kuwakirimia furaha ya kweli, ambayo kamwe hawawezi kupokonywa na walimwengu. Furaha ya kweli inamwilishwa katika huduma ya upendo kwa jirani kama ilivyokuwa kwa kijana Rova Sitraka aliyetimiza ndoto ya kuwatembelea na kuwahudumia wafungwa gerezani. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, maisha yao ni utume unaobubujika kutoka katika imani inayowawajibisha kujizatiti kikamilifu katika maisha, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Huduma ya upendo ni chachu ya mabadiliko katika maisha, kwa kuwaona na kuwathamini wengine jinsi walivyo na huu ni ushuhuda wa furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ambayo hakuna mtu awezaye kuwapokonya hata kidogo.  Kila mtu ana thamani kubwa mbele ya macho ya Mungu na anapenda kuwapatia utume wa kutekeleza katika maisha. Hata gerezani kuna watu wema zaidi. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga na kudumisha urafiki na Kristo Yesu ambaye anataka kuwa karibu na kutembea nao bega kwa bega katika maisha, ili kusherehekea Injili ya uhai. Vijana wanapaswa kuwa makini, ili wasijenge maisha yao katika ndoto za mchana, kwani zinaweza kuwanyima furaha ya kweli katika maisha, kwa kuwageuza kuwa “mateja” na matokeo yake ni kifo. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujitahidi kuwa watu wema zaidi, hata kama bado kuna miundo mbinu inayokwamisha msingi ya haki jamii.

Hakuna sababu ya kukata tamaa, kwani Kristo anaishi na anawataka vijana kuishi; kwa kutumia vyema karama na mapaji katika huduma, ili hatimaye, waweze kuwa mitume wamisionari, tayari kumfuasa Kristo Yesu katika njia ya uzima. Matumaini ya Madagascar na Kanisa katika ujumla wake yako mikononi mwa vijana wa kizazi kipya. Vijana wanatakiwa kuwa na ujasiri ili kuandika kurasa zinazojibu kero na changamoto za maisha kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kristo Yesu anawataka vijana kuwa ni wajenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa njia ya furaha na ushuhuda wa imani! Kwa hakika Kristo Yesu anawategemea vijana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana wanaitwa na kutumwa kama Jumuiya ili waweze kuwa mitume wamisionari; ili kushirikisha mang’amuzi, upendo na imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Vijana wanahimizwa kuutafuta Uso wa Yesu mwingi wa huruma na mapendo kati ya ndugu na jirani zao wanaowazunguka kama alivyofafanya vyema kijana Navy Elyssa.

Vijana wajitahidi kuadhimisha imani katika familia zao, wajenge na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; washiriki kikamili katika vyama na mashirika ya kitume, ili kujenga mshikamano wa dhati. Kamwe vijana wasitembee pweke pweke, huko wanaweza kushambuliwa na hatimaye, kutekwa na “watu wasiojulikana”. Maisha pweke pweke ni kishawishi cha hatari katika ujana! Ni katika maisha ya kijumuiya, vijana wataweza kujifunza miujiza mbali mbali katika kumfuasa Kristo na kuwapenda jirani zao licha ya tofauti zao za kikabila, kidini, kiimani na kitamaduni. Kila kijana anapaswa kuwa ni sadaka safi inayotolewa Altareni. Vijana wanahitaji mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kama: wakleri na makatekista, ili kuwasikiliza na kuwasindikiza katika hija ya maisha, malezi na makuzi yao. Kila mtu ni sehemu muhimu sana ya mpango wa Mungu katika kazi ya ukombozi. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu.

Bikira Maria na Watakatifu wasimamizi wa Madagascar, wanawalinda na kuwasindikiza. Vijana wawe tayari kusema, “Ndiyo na iwe kwangu kama ulivyosema”. Bikira Maria kwa kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake, leo hii ni Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Madagascar kuendelea kuwasha moto wa matumaini, imani na mapendo licha ya “maneno na changamoto za maisha zinazoendelea kujitokeza”.

Papa: Mkesha

 

08 September 2019, 16:52