Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka wananchi wa Madagascar: Kushikamana, Kupambana na rushwa pamoja na kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Papa Francisko anawataka wananchi wa Madagascar: Kushikamana, Kupambana na rushwa pamoja na kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili.  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Maendeleo fungamani ya binadamu: Utu & Heshima yake.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi mbali mbali nchini Madagascar amekazia: Mshikamano unaokumbatia uhai, siasa kama chombo cha ujenzi wa Jumuiya kibinadamu; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani na matumaini” Baba amewasili nchini Madagascar, Ijumaa jioni tarehe 6 Septemba 2019 na kulakiwa na umati wa watu wa Mungu nchini Madagascar walioongozwa na Rais Andry Rajoelina pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Baba Mtakatifu alikagua gwaride la heshima na hatimaye, kuondoka kuelekea kwenye ubalozi wa Vatican nchini Madagascar. Alipowasili, Baba Mtakatifu alitumbuizwa na Kwaya ya vijana wa Jimbo kuu la Antananarivo lililoundwa kunako mwaka  1989 na baadaye kusalimiana na kila mmoja wao! Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Septemba 2019 ameianza siku hii kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Madagascar na baadaye alikwenda Ikulu ya Madagascar ili kumtembelea Rais Andry Rajoelina ambaye ni kijana aliyezaliwa kunako mwaka 1974 na kubahatika kuchaguliwa kuwa Rais wa Madagascar hapo tarehe 8 Januari 2019.

Ni kiongozi mwenye uzoefu katika masuala ya kisiasa, licha ya kuwa ni mfanya biashara maarufu, lakini pia amewahi kuwa Meya wa Jiji la Antananarivo, Rais wa uongozi wa kipindi cha mpito na hatimaye, akachaguliwa kuwaongoza watu wa Mungu nchini Madagascar baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa kampeni za uchaguzi nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa: viongozi wa Serikali na kidini wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Madagascar amekazia kwa namna ya pekee mshikamano unaokumbatia uhai, siasa kama chombo cha ujenzi wa Jumuiya kibinadamu; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Madagascar yataletwa na wananchi wa Madagascar wenyewe na kwamba, majadiliano ya kidini, kiekuemene katika misingi ya ukweli na uwazi ni muhimu sana kwa muktakabali wa nchi yao.

Baba Mtakatifu ameishukuru familia ya Mungu nchini Madagascar kwa mapokezi na ukarimu mkubwa waliomwonesha tangu alipowasili nchini humo. Anakiri na kutambua sadaka kubwa iliyotolewa na wadau mbali mbali ili kufanikisha hija hii ya kitume nchini Madagascar. Utamaduni wa watu wa Mungu nchini Madagascar unajikita katika mshikamano unaofumbatwa katika uhai pamoja na kusaidiana kama ndugu wamoja. Ni utamaduni unaothamini na kujali tunu msingi za maisha ya kifamilia, udugu, urafiki na utunzaji bora wa mazingira. Ni katika mshikamano wa kidugu, wananchi wa Madagascar wanaweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazowaandama katika maisha. Uzuri wa mazingira asilia hauna budi kwenda sanjari na maboresho ya maisha ya kiroho pia, ili kukumbatia na kuendeleza uhai ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Madagascar tangu ilipojipatia uhuru wake wa bendera imekuwa na amani na utulivu, matunda ya demokrasia na siasa ambayo inatumika kama chombo madhubuti cha ujenzi wa jamii ya binadamu na taasisi zake.

Siasa inapaswa kutumika kama chombo cha huduma kwa jamii nzima. Wanasiasa na wajibu msingi wa siasa ni changamoto changamani kwa wale ambao wamepewa jukumu la kuwahudumia na kuwalinda raia wenzao, hasa wale ambao ni wanyonge katika jamii, ili kuwajengea mazingira yatakayowawezesha kupata maendeleo ya kweli kwa kuzingatia utu na haki zao msingi. Kimsingi, maendeleo yanapaswa kuwa fungamani ili kukidhi mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu nchini Madagascar kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; mambo yanayochangia kuongezeka kwa pengo kubwa kati ya umati mkubwa wa maskini ambao ndio wale “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na kikundi cha watu wachache ambao wanamiliki utajiri wa kutupwa! Mazingira kama haya yanachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la kiwango cha umaskini pamoja mipasuko mbali mbali ya kijamii inayoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kumbe, kuna haja ya kuwa na ugawi na matumizi bora zaidi ya rasilimali za nchi. Mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu hauna budi kuwahusisha kikamilifu wananchi wenyewe ili kuchangia mustakabali wa nchi yao kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madagascar imebahatika sana kuwa na utajiri mkubwa wa viumbe hai, mali asili na madini; lakini amana na utajiri huu wote vinatishiwa sana na ukataji ovyo wa misitu; unaowanufaisha watu wachache katika jamii. Uchafuzi wa mazingira unaendelea kutishia ustawi na maendeleo ya mazingira nyumba ya wote kwa siku za usoni. Uchomaji wa misitu, vitendo vya kijangiri na uvunaji ovyo wa misitu ni mambo yanayochangia kwa kasi kubwa biashara ya magendo ya mazao ya misitu. Shughuli mbali mbali za kibinadamu zinachangia pia uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Ni kutokana na muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kutengeneza fursa za ajira, kulinda mazingira na kuwasaidia wananchi kuondokana na umaskini; kwa kujizatiti katika haki jamii, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa sasa na kwa kizazi kijacho!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Madagascar imebahatika kuonja mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa njia ya misaada mbali mbali kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maendeleo. Lakini, kwa bahati mbaya, misaada hii imekuwa ni chanzo cha mkakati wa kutaka kufisha amana, utajiri na urithi wa utamaduni wa watu mahalia kwa kisingizio cha utandawazi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, utandawazi wa kiuchumi hauna budi kuheshimu tunu msingi za maisha ya watu mahalia, mtindo wao wa maisha na matamanio yao halali. Ikumbukwe kwamba, maendeleo ya Magascar yataletwa na wananchi wa Madagascar wenyewe na kwamba, wanapaswa kusimama kidete kushiriki katika mchakato huu kwa ajili ya maendeleo yao kwa sasa na kwa siku za usoni. Huu ndio msingi na umuhimu wa kuheshimu vyama vya kiraia kwa sababu ni sauti ya watu mahalia. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Madagascar kufuata mwelekeo huu, ili kamwe asiwepo mtu anayetengwa, anayeachwa pweke au kupotea.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa nchini Madagascar kwa upande wake, litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya: kidini, kiekumene na kitamaduni katika ukweli na uwazi kama alivyotekeleza katika maisha yake Mwenyeheri Victoire Rasoamanarivo, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Madagascar, miaka thelathini iliyopita. Mwenyeheri Victoire Rasoamanarivo alionesha upendo na uzalendo kwa nchi na tamaduni zake; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini kama kielelezo cha imani tendaji kwa Kristo Yesu, mwaliko wa kufuata njia hii. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, majadiliano ya kidini na kiekumene hayana budi kuendelezwa, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, yanayowaambata wote.

Papa: Viongozi

 

07 September 2019, 16:06