Papa Francisko asema, hotuba yake ya mwisho ni: wimbo wa shukrani, kumbu kumbu, utambuzi na urithi wa wa kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji wa kina. Papa Francisko asema, hotuba yake ya mwisho ni: wimbo wa shukrani, kumbu kumbu, utambuzi na urithi wa wa kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji wa kina. 

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Shukrani kwa Wakleri & Watawa: Utume & Uinjilishaji

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya mwisho nchini Madagascar imekuwa ni wimbo wa shukrani, kumbu kumbu na utambuzi wa urithi wa kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji; changamoto za uinjilishaji, utambulisho wa maisha ya kipadre na kitawa; furaha ya uinjilishaji na sala kama silaha ya mapambano katika maisha ya kipadre na kitawa. Ushuhuda wa uinjilishaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 amekuwa akifanya hija ya kitume nchini Madagascar, iliyoongozwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani na matumaini”. Jumapili jioni tarehe 8 Septemba 2019, Kumbu kumbu ya Siku kuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Madagascar. Kwa namna ya pekee, amewakumbuka na kuwaombea wakleri na watawa wagonjwa. Baba Mtakatifu katika hotuba yake ya mwisho nchini Madagascar imekuwa ni wimbo wa shukrani, kumbu kumbu na utambuzi wa urithi wa kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji; changamoto za uinjilishaji, utambulisho wa maisha ya kipadre na kitawa; furaha ya uinjilishaji na sala kama silaha ya mapambano katika maisha ya kipadre na kitawa.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwa mambo haya amewaficha wenye hekima na akili, akawafunuliwa watoto wachanga. Hii ni furaha inayobubujika kutoka katika shuhuda za matatizo, changamoto na fursa zinazoelezea uhai wa Kanisa. Ni shuhuda za watu wanaojisadaka kila siku kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake; Kanisa linalotaka kuwa karibu zaidi na kutembea bega kwa bega na watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika wakleri na watawa nchini Madagascar kutafakari kwa kina kumbu kumbu na utambuzi wa wale wote waliojisadaka kwa ajili ya Kristo sanjari na ujenzi wa Ufalme wake.

Watambue kwamba, wao kwa sasa ni warithi wa amana na utajiri wa uinjilishaji uliotekelezwa na wakleri pamoja na watawa wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume nchini Madagascar. Katika kipindi cha madhulumu, wamisionari walilazimika kuondoka nchini Madagascar, Kanisa changa likaongozwa na waamini walei, walioendelea kuhakikisha kwamba, moto wa imani unaendelea kuwaka nchini Madagascar. Changamoto na mwaliko wa kukumbuka dhamana na wajibu waliojitwalia katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowafanya kuwa ni watoto wateule wa Mungu; mwaliko wa kuendelea kupyaisha upendo ule walioonjeshwa tangu mwanzoni.

Wamisionari wa mwanzo, walithubutu kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kushirikishana amana na utajiri uliokuwa unabubujika kutoka katika sakafu ya maisha yao. Hata leo hii, wakleri na watawa bado wanathubutu kuendelea kujizatiti katika maisha na utume wao, licha ya changamoto mbali mbali kama vile ukosefu wa  mahitaji msingi, miundombinu mibovu, pamoja na “afya mgogoro”. Lakini mwisho wa siku, bado wako pamoja na kati ya watu wa Mungu; ushuhuda wa wito unaopania kuboresha maisha ya watu wa Mungu nchini Madagascar. Licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, lakini bado wanaendelea kuzama zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wakitambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya upendeleo katika moyo wa Kristo pamoja na waja wake.

Wakleri na watawa ni watu wa sifa na shukrani; wenye uwezo wa kutambua uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake, ni watu wanaotaka kuishi uwepo huu, kwani wamejifunza kuuonja na kuwashirikisha wengine. Ni watu wenye ari na kiu ya kutaka kuendeleza utume wao, kwa kubaki wakiwa wameungana na watu wao; wanasaidiana kutambua vigezo na shughuli nzima ya kimisionari, ili kukoleza ile chachu ya Injili. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, changamoto kubwa wanayoweza kukabiliana nayo wakleri na watawa ni kishawishi cha kushindwa; kwa kujiona kuwa “si mali kitu”; mambo ambayo yanawapotezea muda katika majadiliano yao ya kila siku. Ni watu wenye ndoto za miradi mikubwa ya shughuli za kitume, iliyopangwa na kutekelezwa kwa umakini mkubwa.

Lakini kufanya hivi ni kuikana historia yao kama Kanisa inayosimikwa katika sadaka, matumaini na mapambano ya kila siku “hadi kieleweke”. Haya ni maisha ya watu wanaojisadaka kila siku katika huduma na udumifu wa kazi ngumu. Huu si wakati wa kukata tamaa kwa kutamani mambo makubwa kana kwamba, haya ndiyo lengo la maisha na utume wa kipadre na kitawa. Jambo muhimu ni watu kuwa na mahitaji yao msingi. Sadaka na majitoleo yanachochea ukuaji, ukomavu na hatimaye, watu wa Mungu wanaweza kuzaa matunda yanayoridhisha moyo. Furaha na maisha ya kipadre na kitawa inazungukwa na changamoto inayowataka kuwa kweli ni mashuhuda wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu inayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha, katika ukweli; wanaweza “wakateleza na kuanguka” lakini lengo na hatima ya maisha yao, liko salama. Ni watu wanaomsifu na kumwabudu Mungu kama sehemu ya ushuhuda wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anawakumbusha wakleri na watawa kwamba, kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi 72 waliporejea na kusimlia kwa furaha matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu aliwawezesha kufanya, watambue kwamba, yote haya wanayafanya kwa jina la Kristo Yesu na wala si kwa jeuri na nguvu zao binafsi. Furaha ya kweli ya mfuasi amini wa Kristo inabubujika katika utekelezaji wa shughuli mbli mbali kwa niaba ya Kristo mwenyewe; kwa kuishi utume, kwa kutekeleza miradi na kushiriki maisha ya Kristo Yesu, kiasi cha kumchangamotisha kuwashirikisha wengine pia! Wafuasi wa Yesu wataweza kushinda nguvu za Shetani, Ibilisi kwa jina la Yesu.

Katika maisha na utume wa wakleri na watawa, hapana shaka kuna wakati wameshinda vita lakini pia kuna wakati ambao “wamegalagazwa mchangani”. Wakleri na watawa wajifunze kushinda ubaya kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu; kwa kufundisha Injili na Katekesi; kwa kutembelea na kuwafariji wagonjwa; kwa kuwapatanisha watu; kwa kuwalisha na kuwanyweshwa wenye kiu na njaa ya haki; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kutoa fursa za ajira kwa watu wasiokuwa na kazi; kwa kujikita katika sekta ya elimu na afya; kwa kuheshimu na kuhimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kupanda miti pamoja na kuwasaidia watu wa Mungu kupata maji safi na salama, ili kulinda na kudumisha afya ya wananchi. Huu ndio ushindi unaopatikana kwa jina la Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi yanafumbatwa katika masifu na sala dhidi ya hali ya mtu kutaka kujitafuta mwenyewe, ili kupata uhuru usiokuwa na mipaka. Sala ni kitovu cha maisha na wito wa kipadre na kitawa. Ni chachu ya kuweza kukutana na wengine tayari kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji kwa ari na moyo mkuu. Wakleri na watawa, kamwe wasisali kwa mazoea, kwani kwa kufanya hivi, wanamfungulia Ibilisi malango katika maisha na wito wao. Hapa, kuna umuhimu wa kujikita katika mashauri ya Kiinjili yaani: Ufukara, Utii na Useja; chemchemi ya furaha ya maisha ya kimisionari. Watawa wasikubali watu kuwapoka furaha hii katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu amewakirimia furaha wanayoweza kuiona na kuishuhudia,  kwa kugundua na kutambua uwepo wa Mungu kati ya wagonjwa na watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu wenye kiu na njaa ya haki; watu ambao kimsingi ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Heri Kanisa ambalo ni maskini kwa ajili ya maskini na linaishi umaskini kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni amana na hazina ya Kanisa, wanao upendeleo wa pakeee mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewataka wakleri na watawa kwa niaba yake, kuwafikishia baraka zake za kitume watu wanaowahudumia, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na baraka aendelee kuwabariki watu wake. Na kwa wakleri na watawa, wawe amana hai ya uwepo wa Mungu kati ya waja wake.

Papa: Viongozi wa Kanisa

 

09 September 2019, 18:40