Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar amefafanua kuhusu wajibu, dhamana na utume wa Maaskofu mahalia. Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar amefafanua kuhusu wajibu, dhamana na utume wa Maaskofu mahalia.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Dhamana & Utume wa Maaskofu Mahalia

Askofu ni kiongozi anayesimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za ndugu zake. Ni kiungo cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa. Askofu anapaswa kuwa mwaminifu kwa Injili; ajenge uhusiano mwema na wakleri wake ambao ni wenza wa mchakato wa uinjilishaji. Askofu ajitahidi kutunza miito; ashirikiane na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani na matumainii”. Jumamosi, tarehe 7 Septemba 2019, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar kwenye Kanisa kuu la Andohalo, Jimbo kuu la Antananarivo. Alipowasili Kanisani humo, Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusali kitambo mbele ya Ekaristi Takatifu na baada ya mkutano wake na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar, amepata nafasi ya kukutana na kusalimiana na viongozi wa Makanisa ya Kikristo nchini Madagascar na kubadilishana zawadi kama kumbu kumbu endelevu ya tukio hili la kihistoria na baadaye akaenda kutembelea na kusali kwenye kaburi la Mwenyeheri Victoire Rasoamanarivo, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Madagascar, miaka thelathini iliyopita.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amesema, licha ya Askofu kuwa na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, lakini pia ni mpanzi wa amani, matumaini na imani. Ni kiongozi anayesimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za ndugu zake. Ni kiungo cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu anapaswa kuwa mwaminifu kwa Injili sanjari na kujenga uhusiano mwema na wakleri wake ambao ni wenza wa mchakato wa uinjilishaji. Askofu apalilie na kutunza miito ya kipadre na kitawa; ashirikiane na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kudumisha urika wa Maaskofu kwa njia ya majadiliano na ushirikiano wa Makanisa mahalia!

Mpanzi wa amani na matumaini ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar. Anasema, Maaskofu pia ni wapanzi wa amani, matumaini na imani kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Uhuru wa kuabudu na kidini uwasaidie waamini kupata ukamilifu wa furaha katika maisha yao, daima wakijitahidi kutafuta na kudumisha mafao ya wengi. Viongozi wa Kanisa wakizingatia mchango unaotolewa na sayansi kwenye medani mbali mbali za maisha wanayo haki ya kutoa maoni kuhusu mambo yote yanayoathiri maisha ya watu kwani hii ni sehemu muhimu ya uinjilishaji wa kina. Dini inapaswa kushuhudiwa katika maisha ya hadhara na kamwe haiwezi kufungiwa na kubakia kuwa ni sehemu ya faragha ya mtu binafsi.

Maaskofu wanao wajibu na dhamana ya kulinda utu, heshima na haki msingi za ndugu zao wanaochakarika usiku na mchana kujenga taifa linalosimikwa katika mshikamano wa kidugu pamoja na kuwa na taasisi imara. Viongozi wa Kanisa wanayo haki ya kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni kiungo imara cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, ingawa ushirikiano huu unaendelea kubaki kuwa ni sehemu ya changamoto za Kanisa, lakini Kanisa halina budi daima kusoma alama za nyakati, kwa ajili ya kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa liwasaidie watu kupata: ustawi na maendeleo;  elimu na huduma bora za afya; fursa za ajira na demokrasia ili kukuza utu wa binadamu. Ni kwa njia ya kazi inayotekelezwa kwa uhuru, kwa ubunifu, kwa kushirikiana na kusaidiana na wengine hudhihirisha mchakato wa maendeleo fungamani kwa ajili ya wengi.

Maaskofu kama sehemu ya wajibu wao msingi waendelee kusimama kidete kulinda watu wao na hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa na kwamba, wao ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu na wadau makini wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Maskini wanapaswa kulindwa na kutetewa na Mama Kanisa, kwani kwa kawaida ni watu wanaonyonywa, kudhalilishwa pamoja na kudharauliwa sana. Maaskofu wanao wajibu wa kujenga na kudumisha umoja, udugu na upendo wa dhati na wakleri wao. Kati yao wawe ni mababa na ndugu wa imani na kamwe wasiwaache mapadre wao kujisikia wapweke na yatima. Wawasaidie wakati wa raha na karaha katika maisha na utume wao; wawasikilize na kujiaminisha kwao.

Maaskofu kama viongozi wa Makanisa mahalia, wanao wajibu na dhamana ya kupandikiza mbegu ya miito ya kipadre na kitawa kwa kuiendeleza na kuitunza. Maaskofu watoe malezi na majiundo makini kwa vijana wanaotaka kujisadaka katika maisha ya kipadre na kitawa, ili waweze kukua na kukomaa, huku wakiendelea kupyaisha na kutakasa nia zao. Wito wa jumla kwa wote ni utakatifu wa maisha ambao ni mvuto wa sura ya Kanisa. Maaskofu washirikiane kikamilifu na waamini walei katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Waamini walei wapewe malezi na majiundo ya kutosha, ili mwisho wa siku waweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Na kwa njia hii, wataweza kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii na katika maisha na utume wa Kanisa nchini Madagascar.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki nchini Madagascar kujenga na kudumisha urika wao kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ushirikiano na mshikamano kati ya Makanisa mahalia sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, bila kusahau kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia umuhimu wa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Waamini wanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kumtambua Kristo Yesu kati ya wakimbizi na wahamiaji wa nyati zote, ili kuweza kumfungulia malango ya maisha yao na kumkaribisha.

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar kwa kuwakumbuka na kuwaombea wakleri wazee na wagonjwa. Amewataka Maaskofu kuwahudumia kwa moyo wa ukarimu na upendo. Mwenyeheri Victoire Rasoamanarivo na Bikira Maria ndio walinzi wakuu wa Kanisa kuu la Andohalo; wanawake hawa wawili wawe ni mfano bora wa kuigwa katika huruma na upendo kwa watu wanaohisi kwamba, wamesahaliwa ili waweze kuwa wapanzi wa amani na matumaini katika maisha yao.

Maaskofu: Madagascar
07 September 2019, 17:49