Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake Barani Afrika amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa majanga asilia duniani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake Barani Afrika amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa majanga asilia duniani. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Msumbiji: Achonga na Wanahabari

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea waathirika wa majanga haya asilia ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa mali zao. Baba Mtakatifu anasikitika kusema hawa ni watu wa kawaida ambao kufumba na kufumbua wanajikuta wamepoteza kila kitu, huku kifo kikiwakodolea macho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Msumbiji katika hija yake ya kitume Barani Afrika, Jumatano tarehe 4 Septemba 2019 amepata nafasi ya “kuchonga na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake. Kwa namna ya pekee amesikitishwa na maafa yaliyosababishwa na kimbunga kilichopewa jina la Dorian, ambacho kimekwisha kusababisha watu 7 kupoteza maisha na kwamba, pengine idadi hii ikaongezeka zaidi. Kimbunga hiki kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kisiwa cha Bahama na Abacos vimeathirika zaidi. Miji ya Florida, Georgia, North na South Carolina imetangaza hali ya hatari. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea waathirika wa majanga haya asilia ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa mali zao. Baba Mtakatifu anasikitika kusema hawa ni watu wa kawaida ambao kufumba na kufumbua wanajikuta wamepoteza kila kitu, huku kifo kikiwakodolea macho!

Maafa haya yanaendelea kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa umuhumi wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani hata Msumbiji hivi karibuni ilikumbwa na maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha “Idai”. Mazungumzo ya Baba Mtakatifu na waandishi wa habari 70 walioko kwenye msafara wake, yalitanguliwa na neno la shukrani kutoka kwa Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican ambaye, kwa mara ya kwanza anasafiri na Baba Mtakatifu kama Msemaji mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu amefurahishwa na idadi kubwa ya waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake, ambao wengi wao wanaonekana kuwa ni wapya kabisa. Baba Mtakatifu analipongeza Shirika la Habari la Hispania, EFE, ambalo mwaka huu linatimiza miaka 80 tangu lilipoanzishwa.

Baba Mtakatifu amesema, atawapatia nafasi ya kuuliza maswali zaidi wakati watakapokuwa wanarejea kutoka katika hija yake ya kitume Barani Afrika. Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Valentina Azlaraki, mwandishi wa habari kutoka Kituo cha Televisheni cha “Televisiva” ambaye katika maisha yake ya kitaaluma ameshiriki hija za kitume 153 zilizofanywa na Mapapa mbali mbali 153. Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Valentina Azlaraki kutokana na mchango ambao umewaachia wasomaji wake mintarafu nyanyaso na utumwa mamboleo wanaofanyishwa wanawake sehemu mbali mbali za dunia. Huyu ni mwandishi wa habari ambaye amewasaidia walimwengu kugusa uchungu na madhara ya utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana.

Baba Mtakatifu kabla ya kuondoka mjini Roma, alipata nafasi ya kukutana na kusalimiana na wakimbizi pamoja na wahamiaji kutoka Msumbiji, Madagascar na Mauritius. Hii ni safari ni ya muda wa saa 10 angani. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Fumicino, Baba Mtakatifu ameagana na viongozi wa Serikali y Italia pamoja na viongozi wa Kanisa. Akiwa nchini Msumbiji, ratiba rasmi inaanza siku ya Alhamisi kwa kumtembelea Rais Filipe Jacinto Nyusi kwa kuzungumza na viongozi wa Serikali, siasa na wanadiplomasia. Anatarajiwa kukutana na kuzungumza na vijana kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu anatarajia kukutana na Jumuiya ya Xai-Xai (Shaishai) kwa faragha, kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Msumbiji. Baadaye atatembelea pia Nyumba ya Matteo 25. Hivi ndivyo mambo yanatarajia kufanyika Alhamisi, tarehe 5 Septemba 2019.

Papa: Safarini
04 September 2019, 14:52