Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewasili tayari nchini Msumbiji, akiwa njiani amewatumia salama na matashi mema viongozi wakuu wa Serikali pamoja na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko amewasili tayari nchini Msumbiji, akiwa njiani amewatumia salama na matashi mema viongozi wakuu wa Serikali pamoja na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania. 

Papa Francisko awasili Msumbiji, atuma salam kwa Rais Magufuli

Baba Mtakatifu Francisko alipoingia kwenye anga la Tanzania, amemtumia salam na matashi mema Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, akiwatakia watanzania wote amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Kwa watu wa Mungu nchini Malawi, amewaombea baraka na amani na hatimaye, kwa familia ya Mungu nchini Zambia, ameiombea amani, baraka na ustawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya thelathini na moja ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa Barani Afrika, kuanzia tarehe 4 – 10 Septemba 2019 inatarajiwa kuzaa matunda ya: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote,  sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya watu wa Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Baba Mtakatifu amewasili mjini Maputo Msumbiji na kulakiwa na bahari ya watu. Amekagua gwaride la heshima, wakatambulishana wageni waliokuwa kwenye msafara na baadaye, Baba Mtakatifu amepata fursa ya kuangalia ngoma za asili kutoka sehemu mbali mbali za Msumbiji.

Gari ambalo anatumia Baba Mtakatifu nchini Msumbiji kwa sasa ni lile ambalo alilitumia wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya. Hiki ni kielelezo cha ufukara wa Kiinjili na udugu na ujirani mwema kutoka Kenya. Maelfu ya familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za Msumbiji, walijipanga barabarani wakati Baba Mtakatifu na msafara wake ulipokuwa unapita kuelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Msumbiji. Yaani hadi rahaa! Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Msumbiji, Jumatano tarehe 4 Septemba 2019 ametuma salam na matashi mema kwa Marais na wakuu wa nchi mbali mbali ambamo amebahatika kupitia katika anga zao. Nchi hizi ni pamoja na Italia, Ugiriki, Misri, Sudan, Sudan ya Kusini, Uganda, Tanzania, Malawi pamoja na Zambia.

Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Rais Sergio Mattarella wa Italia akimjuza kwamba ameanza hija yake ya kitume kuelekea Msumbiji, Madagascar na hatimaye Mauritius. Baba Mtakatifu anasema kwamba, ana kiu kubwa ya kukutana na ndugu zake wapendwa katika imani wanaoishi katika mataifa haya. Anapenda pia kumhakikishia sala zake kwa ajili ya ustawi wa watu wa Mungu nchini Italia. Baba Mtakatifu amewatakia baraka, amani, furaha na maendeleo fungamani wananchi wote wa Bara la Afrika na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea katika sala zake. Kwa familia ya Mungu huko Sudan Kongwe, Baba Mtakatifu amewatakia amani na upatanisho wa kidugu. Kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini, Baba Mtakatifu anawatakia ustawi na maendeleo fungamani. Kwa wananchi wa Uganda, Baba Mtakatifu anawaombea amani na utulivu wa kweli.

Baba Mtakatifu Francisko alipoingia kwenye anga la Tanzania, amemtumia salam na matashi mema Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, akiwatakia watanzania wote amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Kwa watu wa Mungu nchini Malawi, amewaombea baraka na amani na hatimaye, kwa familia ya Mungu nchini Zambia, ameiombea amani, baraka na ustawi.

Papa: Viongozi wa Afrika
04 September 2019, 19:02