Tafuta

Vatican News
Papa Francisko kuanzia tarehe 19 - 26 Novemba 2019 anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Thailand na Japan. Papa Francisko kuanzia tarehe 19 - 26 Novemba 2019 anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Thailand na Japan.  (AFP or licensors)

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia: Thailand & Japan

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019 atakuwa na hija ya kitume Barani Asia: Thailand na Japan ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan pamoja na Serikali ya Japan wa kutembelea nchini humo kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema, Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019 atakuwa na hija ya kitume Barani Asia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan pamoja na Serikali ya Japan wa kutembelea nchini humo kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019. Hija ya Baba Mtakatifu nchini Japan inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Nembo ya hija hii ni mwali wa moto unaohimiza upendo unaopaswa kumwilishwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kulinda maisha. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan inapania pamoja na mambo mengine, kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote” anawaalika waamini pamoja watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato utakaoleta mabadiliko katika mtindo wa maisha yao kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na Dunia Mama. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yanayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba dunia na kuifanya, ndiye aliyeifanya imara, hakuimba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu. Ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kuna haja wanasema Maaskofu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote.

Changamoto kubwa kwa sasa nchini Japani zinahusu Injili ya uhai, amani, uchumi na uhusiano na nchi jirani. Japan inaendelea kupambana ili kukabiliana na athari za majanga asilia pamoja na kuvuja kwa mtambo wa nyuklia. Kanisa nchini Japan, limeeendelea kuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ndiyo maana hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan inapania kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na matumaini dhidi ya utamaduni wa kifo, ili kweli amani iweze kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu akiwa nchini Japan, atatembelea mji mkuu wa Tokyo, Nagasaki na Hiroshima. Ratiba elekezi inatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand pamoja na Serikali ya Thailand wa kutembelea nchini humo kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019. Kauli mbiu inayoongoza hija hii ya kitume ni “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Siam kuanzia mwaka 1669 hadi mwaka 2019. Wakatoliki nchini Thailand wanaungana na vijana wa kizazi kipya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wanahimizwa kuzaa matunda ya ushuhuda wa imani yao, kwa kutambua kwamba, wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa.

Papa Francisko: Asia
13 September 2019, 16:12