Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, tarehe 23 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja na wafanyakazi wake! Papa Francisko, tarehe 23 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja na wafanyakazi wake!  (ANSA)

Papa Francisko & Baraza la Kipapa la Mawasiliano: Utume & Dhamana!

Papa amegusia: Changamoto za mawasiliano, utume wa Kanisa; umuhimu wa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama timu; mfumo wa mawasiliano ya Kanisa unafumbatwa katika ushiriki na kushirikishana kama ushuhuda wa umoja wa Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia. Papa ataendelea kuunga mkono miradi mbali mbali ya ushirikiano kati ya Vatican na Makanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja na wafanyakazi wote wanaunda Baraza hili yaani: wafanyakazi wa Radio Vatican, Gazeti la L’Osservatore Romano, Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV, Kurugenzi ya Msemaji mkuu wa Vatican, pamoja na Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV. Hiki ni kikosi cha kazi kinachomsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ambao kwa mara ya kwanza amekutana nao katika ujumla wao, tangu mwanzo wa mchakato mkubwa wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican ulipoanza kunako mwaka 2015 kwa kusoma alama za nyakati, ili kuleta tija, ufanisi na ubora zaidi katika muktadha wa mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo.

Nyuso za wafanyakazi wengi si ngeni sana machoni pake, lakini anatambua kwamba, kuna umati mkubwa wa wafanyakazi wanaoendelea kujisadaka kila siku ya maisha yao, wakimsindikiza Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake wa kila siku. Ni watu wanaojituma kwa ajili ya huduma kwa Mama Kanisa, kwa kuweka nguvu, weledi, kipaji cha ubinifu, ari na moyo mkuu katika utekelezaji wa majukumu yao. Baba Mtakatifu anawashukuru wafanyakazi hawa wote kwa sababu wamekuwa kweli ni kichocheo cha safari ya imani, wakitiwa shime, kumtafuta, ili hatimaye, kukutana na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawashukuru wafanyakazi hawa wanaomwezesha kuzungumza takribani lugha arobaini na kwa hakika huu ndio “muujiza mpya wa Pentekoste” Katika lugha hizi arobaini, Lugha ya Kiswahili pia imo, hata kama haivumi! Ni kwa njia ya sadaka na majitoleo ya wafanyakazi hao, ujumbe wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unaweza kusomwa kwenye magazeti, unaweza kusikilizwa kwenye radio, unaweza kuonwa kwenye luninga pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, ambayo watu wanashirikishana kwenye ulimwengu wa kidigitali, matendo makuu ya Mungu!

Baba Mtakatifu amegusia changamoto za mawasiliano, mawasiliano kama utume wa Kanisa; umuhimu wa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama timu na kwamba, mfumo wa mawasiliano ya Kanisa unafumbatwa katika ushiriki na kushirikishana kama ushuhuda wa umoja wa Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia na kwamba, Papa Francisko ataendelea kuunga mkono miradi mbali mbali ya ushirikiano kati ya Vatican na Makanisa mahalia. Baba Mtakatifu amesema, “cheche za mageuzi” ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican imekuwa ni “shughuli pevu” kutokana na ugumu wa mchakato wenyewe pamoja na hali ya kudhaniana vibaya. Baba Mtakatifu anaridhishwa na hatua mbali mbali za mageuzi zilizokwisha kufikiwa, kwa kuwa na mikakati ya utekelezaji kwa muda mfupi na mrefu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, rasilimali watu, fedha na vitu vinatumika kikamilifu, ili kupunguza pia gharama za uendeshaji wa sekta ya mawasiliano ndani ya Kanisa.

Mawasiliano ndani ya Kanisa ni utume unaoliwezesha Kanisa kuwekeza katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu. Katika muktadha huu, kila karama inapaswa kutumiwa vizuri ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa sanjari na kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko ya kile ambacho Kanisa linatangaza. Wafanyakazi wawe na ujasiri wa kufanya mabadiliko, bila kukata wala kukatishwa tama, kwa kujimanua kutoka kwenye mtego wa usalama usiokuwa na uhakika, tayari kukumbatia changamoto za mbeleni kwa moyo wa matumaini. Katika muktadha huu, wafanyakazi waendelee kuambata kumbu kumbu za mambo msingi waliyotenda, tayari kuunganisha nguvu ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Baba Mtakatifu anaungana na wafanyakazi kumshukuru Mungu kwa nguvu anayowakirimia ili kuendelea mbele katika mchakato wa safari hii ya mageuzi. Anatambua pia udhaifu na mapungufu ya wafanyakazi wa Baraza la Mawasiliano ikilinganishwa na dhamana kubwa iliyoko mbele yao.

Lakini, kama alivyowahi kusema, Mtakatifu Paulo VI kuna haja kufikiria mwelekeo wa nguvu mpya, namna ya kuhukumu mambo kwa kujifunza kutoka katika shule ya Kristo Yesu. Nguvu ya imani, iwatie shime katika udhaifu wao wa kibinadamu, wawe ni vyombo vya Mungu vinavyotekeleza kazi yake, kwa kutambua kwamba, wao ni wadogo sana kuliko hata “piliton” lakini wanao moyo wa ukarimu. Changamoto katika ulimwengu wa mawasiliano zinazidi kuongezeka maradufu, lakini watambue kwamba, wanaitwa kutekeleza wajibu wao kama Wakristo na watu wa mawasiliano. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Kanisa tarehe 2 Juni 2019 uliongozwa na kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25): Kutoka Jumuiya ya mtandaoni kwenda kwenye Jumuiya halisi ya watu! Hii ni changamoto ya ujenzi wa Jumuiya halisi ya binadamu.

Hii ndiyo kauli mbiu pia inayoongoza Mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa na Baba Mtakatifu anasema nguvu yao kama watu wa mawasiliano inafumbatwa katika umoja, kwa kutambua kwamba, kila mmoja wao ni kiungo cha mwenzake na kwa njia hii, wataweza kutekeleza vyema utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anakazia kusema, kama wakristo utambulisho wao ni udugu kama vile wana familia moja yaani Kanisa, Mwili mmoja ambao kichwa chake ni Kristo Yesu Mwenyewe. Umoja wao unaofumbatwa katika Imani moja Takatifu Katoliki ya Mitume ambayo kwayo wanatambuana na hivyo kuwatazama wengine kama watoto wa Mungu. Umoja ni kiini cha utambulisho wao unaofumbatwa katika imani na kuwakutanisha katika upendo wa Mungu unaowapatia “jeuri” ya mawasiliano, kwa kumpokea, kumtambua na kumjibu jirani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mawasiliano ndani ya Kanisa yanafumbatwa katika kanuni ya ushiriki na kushirikishana na ufanisi wake unajionesha katika ushuhuda wa sadaka ya maisha inayotolewa na Roho Mtakatifu, kiasi cha kuwawezesha kutambua umoja unaowaunganisha na hivyo kuwawezesha kuwa kiungo kwa wenzao!

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, mawasiliano iwe ndani ya Kanisa au na walimwengu, hayana budi kusimikwa katika ukweli na uwazi, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kwa kujenga ushirikiano kati ya waamini walei na viongozi wa Kanisa, kwa ajili ya ustawi na ufanisi wa maisha pamoja na utume wa Kanisa ulimwenguni. Katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kila siku, Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa Baraza la Mawasiliano wajenge moyo wa umoja na mshikamano kama “Kikosi cha ushindi”. Huu ni ushirikiano unaojionesha kati ya waamini walei, wakleri na watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaozungumza lugha tofauti, amana na utajiri wa Kanisa. Mtindo wa maisha yao, uwe ni ushuhuda wa umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa Baraza kutumia vyema kipaji cha ubunifu ili kujenga na kukuza mtandao wa ushirikiano na Makanisa mahalia. Waendelee kujikita katika mchakato wa majiundo makini na endelevu katika ulimwengu wa kidigitali, ambao kwa bahati mbaya, watu wanawasiliana sana, lakini bila ya watu kuwa na umoja wa dhati, unaowafungamanisha katika mambo msingi.

Huduma ya mawasiliano ya jamii kimsingi ni kwa ajili ya wote. Miradi mbali mbali ya mawasiliano inayotekelezwa na Baraza la Kipapa la Mawasiliano, itaendelea kuungwa mkono na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa njia ya kazi na huduma yao, wafanyakazi hawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa sanjari na kuratibu mawasiliano ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Hapa anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kutembea bega kwa bega huku wakiwa wameshikamana; kwa kusoma alama za nyakati na kuzipatia tafsiri sahihi ili kuratibu mwenendo wa nyakati hizi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa mawasiliano ndani ya Kanisa utaendelea kujidhihirisha katika umoja kama mwili mmoja!

Papa: Baraza

 

23 September 2019, 17:15