Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema mbio za "Via Pacis" ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni kati ya watu wa Mataifa. Papa Francisko asema mbio za "Via Pacis" ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni kati ya watu wa Mataifa.  (ANSA)

Papa: Mbio za Via Pacic: Majadiliano ya kidini & Kitamaduni!

Mbio za “Via Pacis” za marathoni za kilometa 22 kwa kupitia: Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Sinagogi la Wayahudi na hatimaye, kupitia pia katika Msikiti mkuu wa Roma. Baba Mtakatifu anasema, lengo la mbio hizi ni kutangaza na kushuhudia ujumbe wa amani na udugu, lakini zaidi umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 22 Septemba 2019, amewashukuru na kuwapongeza wanariadha elfu saba, waliojihimu kukimbia mbio za “Via Pacis” za marathoni za kilometa 22 kwa kupitia katika viunga vya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Sinagogi la Wayahudi na hatimaye, kupitia pia katika Msikiti mkuu wa Roma. Baba Mtakatifu anakaza kusema, lengo la mbio hizi ni kutangaza na kushuhudia ujumbe wa amani na udugu, lakini zaidi umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni kati ya watu wa Mataifa. Kwa mara ya kwanza, Askofu Jean Paul Vesco wa Jimbo la Oran, Algeria ameshiriki kikamilifu. Wanamichezo wa Vatican wanaotoka katika mataifa 42 wameshiriki katika mbio hizi.

Sr. Marie Theo, kutoka katika Shirika la Wadomican, amewashangaza walimwengu kwa jinsi alivyokuwa “anafukuza upepo” kana kwamba, amezaliwa kwenye mbuga za Manyara. Sr. Marie Theo anasema, hata watawa katika makazi yao wanafanya mazoezi, lakini kuna utamu wake, kukimbilia pamoja na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwani haya ni mang’amuzi ya ujenzi wa jumuiya kubwa ya watu wa Mungu. Mtakatifu Augostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa alikuwa anasema, kuimba ni kusali mara mbili, lakini kukimbia mbio ndefu ni njia nyingine ya kusali na kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha. Askofu Jean Paul Vesco anawahamasisha wakleri na watawa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi. Kwa upande wake, Monsinyo Melchor Sànchez de Toca, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, anawapongeza wafanyakazi wote wa Vatican walioshiriki kwa wingi katika mbio hizi, kwani lengo ni kuendelea kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama walivyofanya Watakatifu Petro na Yohane, Siku ile ya kwanza ya Juma, walipoambiwa kwamba, hakika Kristo Yesu amefufuka kutoka kwa wafu!

Papa: Via Pacis

 

 

23 September 2019, 14:45