Papa Francisko amewashauri Maaskofu wapya waliowekwa wakfu hivi karibuni kuwa ni mashuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake kwa njia ya ushuhuda! Papa Francisko amewashauri Maaskofu wapya waliowekwa wakfu hivi karibuni kuwa ni mashuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake kwa njia ya ushuhuda! 

Papa Francisko: Maaskofu kielelezo cha ukaribu wa Mungu!

Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa watu wake. Uwepo wa karibu wa Mungu ni chemchemi ya utume wa Askofu kama unavyofunuliwa katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Ili kuonja ukaribu huo kuna umuhimu wa kupata mang’amuzi ya wema, huruma na upendo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu ana wajibu na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye mchungaji mkuu anayeunda na kuliongoza Kanisa; Kristo ndiye nguzo na mhimili mkuu wa Kanisa lake. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mipango ya Kristo mchungaji mwema. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 4 hadi 11 Septemba 2019 yameendesha mafunzo maalum kwa ajili ya Maaskofu mahali kutoka kwenye Makanisa ya Mashariki walioteuliwa na kuwekwa wakfu katika kipindi cha mwaka mmoja yaani kati ya mwaka 2018 hadi mwaka 2019.

Maaskofu hawa wapya wamepata nafasi ya kukiri kanuni ya imani, muhtasari wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu ili kuendeleza uwepo wake wa karibu katika maisha na utume wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Uwepo wa karibu wa Mungu ni chemchemi ya utume wa Askofu kama unavyofunuliwa katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo makini cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Ili kuonja ukaribu wa Mungu kuna umuhimu wa kupata mang’amuzi ya wema, huruma na upendo kwa waja wake. Maaskofu wajenge utamaduni wa kusali na kutafakari mbele ya Kristo Yesu, ili kumwezesha kuishi kati ya watu wa Mungu.

Katika shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kiaskofu, Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kukimbilia katika sala na tafakari, ili kujenga tena: imani na matumaini mapya, kwa kumtegemea na kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Ukaribu wa Mungu unajionesha kati ya watu wake kwa njia ya utambulisho wa Maaskofu, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kama sadaka safi inayotolewa Altareni. Maaskofu ni mkate unaomegwa kwa ajili ya maisha ya ulimwengu. Kristo Yesu anataka kuwa kati pamoja na watu wake kwa njia ya Maaskofu. Ukaribu wa Mungu unajionesha katika Neno na maadhimisho ya Mafumbo mbali mbali ya Kanisa. Lakini zaidi, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kupenda bila kujibakiza pamoja na kuendelea kujizamisha katika huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuonesha ukaribu wa Mungu kwa waja wake kwa kujitosa kimaso maso katika huduma ya upendo kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, ili waweze kuona, kusikiliza na kujibu kwa vitendo kilio na mhangaiko ya watu wa Mungu kama alivyofanya yule Msamaria mwema: Alipomwona, alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai na hatimaye, akamtunza. Haya ni maneno msingi katika maisha na utume wa Askofu anayetembea bega kwa bega na watu wake, tayari kushirikishana nao mateso na matumaini ya maisha. Maaskofu wawe na ujasiri wa kutekeleza dhamana, wajibu na utume wao bila ya kuogopa. Makanisa yao, yawe ni alama na utambulisho wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Kipimo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake ni huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kumezwa na malimwengu. Maaskofu waguswe na umaskini pamoja na mahangaiko ya watu wao, ili kuinua na kusimamia utu, heshima na haki zao msingi.

Maaskofu wawe karibu zaidi na watu wao, ili waweze kusikiliza mapigo ya nyoyo zao. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Maaskofu watembelee Parokia na waamini wao, ili kuwapelekea faraja, imani, matumaini na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu waoneshe ukaribu wa Mungu kwa mapadre wao, kwa kuwakumbatia, kuwashukuru na kuwapongeza kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Maaskofu wawapende na kuwaheshimu Mapadre wao; wawafuatilie na kuwatia shime, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo makubwa zaidi.

Papa: Maaskofu wapya

 

 

12 September 2019, 16:16