Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya nchini Venezuela kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wote bila ubaguzi. Papa Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya nchini Venezuela kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wote bila ubaguzi.  (AFP or licensors)

Papa: Vijana wa Venezuela tangazeni Injili ya matumaini!

Dhamana, wajibu na utume wa uinjilishaji unapata chimbuko lake kutoka katika imani kwa Kristo Yesu, zawadi waliyoipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni imani inayomwilishwa, inakuzwa na kuendelezwa katika Jumuiya ya Kanisa. Ni imani inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa vitendo; kwa kuwashirikisha vijana wengine. Vijana ni mashuhuda wa Injili ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utume wa Mama Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mambo makuu matatu: kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana kufanya mang’amuzi makini katika maisha na wito wao. Vijana ni amana na utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wazazi kwa kushirikiana vyema na wazee wanaweza kuwasaidia malezi na majiundo bora zaidi ya vijana wa kizazi kipya, jambo la msingi ni marika haya kujenga utamaduni wa majadiliano unaofumbatwa katika sanaa na utamaduni wa kusikilizana! Vijana katika maisha na utume wao, wanapaswa kuzingatia mambo makuu matatu, kwanza kabisa ni: Uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha na historia ya kila kijana; pili, ni umoja na mshikamano utakaowawezesha vijana kuandika historia ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake; na tatu, ni utume  kwa kutambua kwamba, wameitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu José Luis Azuaje Ayala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini humo, yaliyoanza kutimua vumbi hapo tarehe 13-15 Septemba 2019, huko Maracaibo, Venezuela, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu” Lk. 5:10. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kusimama kidete ili kutangaza na kushuhudia matumaini na furaha ya Injili. Vijana wanakumbushwa kwamba, hii ni dhamana na wajibu wa vijana wote kwa ajili ya watu wote na wala hakuna cha mtu kujibakiza na “kujiegesha kando” kama mtazamaji. Dhamana, wajibu na utume wa uinjilishaji unapata chimbuko lake kutoka katika imani kwa Kristo Yesu, zawadi waliyoipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni imani inayomwilishwa, inakuzwa na kuendelezwa katika Jumuiya ya Kanisa. Ni imani inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa vitendo; kwa kuwashirikisha vijana wengine.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na watu wote bila ubaguzi, tayari kujisadaka, ili kuwaendea watu wote, bila kumtenga mtu awaye yote! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza vijana kwa moyo na utayari wao wa kupyaisha na kushirikishana imani, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake; tayari kutangaza na kushuhudia kwa ari na moyo mkuu, matumaini na furaha inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo Yesu. Vijana wawe na ujasiri wa kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inapenya katika medani mbali mbali za maisha ya watu, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia wote baraka zake za kitume na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa mateso!

Papa: Venezuela

 

15 September 2019, 12:46