Tafuta

Papa Francisko asema: Unyenyekevu unamwilishwa katika ukarimu na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Papa Francisko asema: Unyenyekevu unamwilishwa katika ukarimu na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Papa Francisko: Unyenyekevu wa kweli unafumbatwa katika ukarimu

Papa Francisko anasema, unyenyekevu wa kweli unajenga na kudumisha urafiki na mafungamano ya kijamii. Mfano wa pili unaelekezwa kwa mtu anayewaalika watu, ili aweze kuwa makini zaidi kwa kuwaalika maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, kwa maana watalipwa katika ufufuo wa wenye haki. Ukarimu na upendo wao, utalipwa na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 1 Septemba 2019 alianza tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa kuchelewa takribani dakika saba, hali ambayo ilizua wasi wasi miongoni mwa waamini, mahujaji na vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii, vilivyokuwa vimeungana na Vatican kwa ajili ya kufuatilia Sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu kabla ya tafakari yake, amewaambia waamini na mahujaji kwamba, kutokana na itilafu ya umeme, alijikuta akiwa amebaki kwenye “Lift” kwa takribani dakika 25 na baadaye Kikosi cha Zima Moto cha Vatican kiliweza kurekebisha hitilafu na Baba Mtakatifu kuweza kuendelea tena na shughuli zake. Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu mkubwa alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha yote kwenda salama na akawaomba waamini pamoja na mahujaji kuwashangilia wanajeshi wa Kikosi cha Zima Moto mjini Vatican kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu sanjari na kuendeleza ulinzi na usalama!

Baba Mtakatifu akirejea katika tafakari yake, amesema kwamba, Injili ya Jumapili ya XXII ya Mwaka C wa Kanisa inamwonesha Kristo Yesu, akishiriki chakula kwenye nyumba ya mtu mmoja ambaye alikuwa miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya Sabato. Katika muktadha huu, Yesu aliangalia na kuona jinsi ambavyo wageni waalikwa walivyokimbilia viti vya mbele, hali ambayo hadi leo hii inaendelea katika maisha ya watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Falsafa ya vitendo vyote hivi ni watu kutaka kuonesha ukuu, ufahari na umuhimu wao katika jamii ikilinganishwa na watu wengine. Baba Mtakatifu anasema, hii ni hatari sana si tu kwa wafanyakazi Serikalini na hata katika maisha ya Jumuiya ya waamini kwa sababu ni mambo yanayoharibu umoja na udugu wa kibinadamu. Yesu alivyoona wakichagua viti vya mbele akatoa mifano miwili kama fundisho kuhusu unyenyekevu unaofumbatwa katika huduma upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Yesu anawaambia wasikilizaji wake, wakialikwa na mtu wasikimbilie viti vya mbele wasije wakaaibika mbele ya watu, bali wajichagulie viti vya nyuma, ili waweze kukwezwa na wenyeji wao kwa kuwapeleka viti vya mbele. Waamini wanapaswa kuonesha fadhila ya unyenyekevu unaobubujika kutoka katika undani wa mtu na wala si unyenyekevu wa kinafiki. Unyenyekevu wa kweli unajenga na kudumisha urafiki na mafungamano ya kijamii. Mfano wa pili unaelekezwa kwa mtu anayewaalika watu, ili aweze kuwa makini zaidi kwa kuwaalika maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, kwa maana watalipwa katika ufufuo wa wenye haki. Ukarimu na upendo wao, utalipwa na Mwenyezi Mungu.

Unyenyekevu wa kweli ni fadhila ya Kikristo anasema Baba Mtakatifu Francisko, vinginevyo, ukarimu unaweza kugeuzwa kuwa ni biashara ya “nipe nikupe”. Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake, kukita maisha yao katika ukarimu kama njia ya kuanza kushiriki upendo wa Mungu anayewangojea kuwashirikisha kwenye Karamu ya mbinguni. Ni kwa njia ya fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amejinyenyekesha, ili kuwakomboa watu wote kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, kuwashirikisha Karamu ya maisha na uzima wa milele. Bikira Maria, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu na ukarimu, awasaidie waamini kujitambua jinsi walivyo, yaani hali yao ya udogo na unyonge, ili kuweza kufurahia kwa kujisadaka bila ya kujibakiza bila kutegemea kurudishiwa tena! Unyenyekevu unaomwilishwa katika ukarimu uwe ni kigezo cha ujenzi wa urafiki na mafungamano ya kijamii.

Papa: Tafakari: Ukarimu

 

02 September 2019, 10:03