Tafuta

Vatican News
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika hatua kuu tatu: Upendo, Ukweli na Unabii wa Kanisa unaofumbatwa katika huduma kwa maskini. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika hatua kuu tatu: Upendo, Ukweli na Unabii wa Kanisa unaofumbatwa katika huduma kwa maskini. 

Mchakato wa Majadiliano ya Kiekumene: Upendo, Ukweli & Unabii

Kanisa la Kiorthodox linaendelea kujiimarisha katika uekumene wa udugu. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza unafumbatwa katika: upendo, ukweli na unabii, hatua ambayo kwa sasa ndiyo inayovaliwa njuga na viongozi wa Makanisa. Na hii ndiyo maana halisi ya zawadi ya Masalia ya Mtakatifu Petro kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani alitoa zawadi ya Masalia ya Mtakatifu Petro kwa ajili ya Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol ili yaweze kuheshimiwa hata huko. Baba Mtakatifu anasema, hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili hatimaye, siku moja kuweza kufikia umoja kamili, kama ilivyo kwa watakatifu hawa huko mbinguni. Zawadi hii ni kumbu kumbu endelevu ya hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Paulo VI mjini Yerusalemu takribani miaka 50 iliyopita, akazawadiwa Picha ya Mtakatifu Andrea, ikiwa inawaunganisha wote katika imani na mapendo kwa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kuongeza jitihada za majadiliano ya kiekumene ili kufikia umoja kamili na amani; ambayo inabubujika kutoka katika sala. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Masalia ya Mtakatifu Petro yatawekwa karibu na Masalia ya Mtakatifu Andrea anayeheshimiwa sana kwenye Kanisa la Costantinopol.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika mahojiano maalum na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anasema zawadi ya Masalia ya Mtakatifu Petro ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili. Anasema, ameshangazwa sana na ujasiri wa Baba Mtakatifu Francisko kwa zawadi hii adhimu. Anasema, mbinu mkakati wa uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo kwanza kabisa ni huduma makini kwa watu wa Mungu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu na mali zao. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, Baba Mtakatifu anawahamasisha wakristo kumwilisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika uhalisia wa maisha kama ndugu. Zawadi ya Masalia ya Mtakatifu Petro kwa Kanisa la Kiorthodox haikuzingatia protokali wala kutanguliwa na majadiliano ya kiekumene, huu ni ushuhuda wa imani, furaha na upendo wa kidugu unaowaunganisha waamini wa Makanisa haya mawili.

Masalia haya ni baraka, kisakramenti na changamoto ya kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha. Kuna mambo mengi ya kuendelea kujifunza kutoka katika maisha ya Mtakatifu Petro: Imani kuu kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu; Udhaifu wake kwa kumkana Yesu mara tatu; ushupavu wa kutubu na kumwongokea tena Kristo Yesu ili aweze kumwiimarisha katika imani. Mtume Andrea pamoja na Mtakatifu Petro ni wasimamizi wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Masalia ya Mtakatifu Petro ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa umoja na ushirika. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa katika upendo, dhamana iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita, baraka ambayo kwa wakati huu imewekwa chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Petro, Mtume. Huu ni mwaliko kutoka kwa Mtume Petro anayewataka watoto wa Mungu kuishi katika upendo, unyoofu; kwa kujitakasa roho zao, ili kutii kweli, ili hatimaye kufikia upendo wa kidugu usiokuwa na unafiki!

Mwaliko kwa Wakristo ni kupendana kwa dhati kabisa. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014 alifanya hija ya kitume katika Nchi Takatifu kama kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu. Tangu wakati huo majadiliano ya kiekumene yameendelea kushika kasi, ili kuvuka kipeo cha kashfa ya utengano kati ya Makanisa, ili hatimaye, katika umoja, upendo na mshikamano Wakristo waweze kutoa ushuhuda wa Injili unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kanisa Katoliki linaendelea kujipambanua kama chombo cha kuhamasisha umoja wa Wakristo. Kwa upande wake, Kanisa la Kiorthodox linaendelea kujiimarisha katika uekumene wa udugu miongoni mwa Wakristo. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza unafumbatwa katika: upendo, ukweli na unabii, hatua ambayo kwa sasa ndiyo inayovaliwa njuga na viongozi wa Makanisa. Na hii ndiyo maana halisi ya zawadi ya Masalia ya Mtakatifu Petro kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Maadhimisho ya Liturujia Takatifu chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa, yanawahamasisha waamini kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kanisa halina budi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya huduma makini kwa jirani, yaani diakonia! Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yanapania pamoja na mambo mengine, kuganga na kuponya uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na hivyo kuanza mchakato njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani. Huu ni utekelezaji wa dhamana na wajibu wa kinabii Ukanda wa Amazonia. Imegota miaka 30 tangu maadhimisho ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira yalipoanzishwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kunako mwaka 1989. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira, maadhimisho haya yakaendelezwa hadi kufikia kilele chake tarehe 4 Oktoba, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Matukio yote kuhusu utunzaji bora wa mazingira katika kipindi hiki chote, yanapania kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiekolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu na heshima ya binadamu pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kwa njia ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanaweza kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuelewa matatizo, changamoto na umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Machapisho mbali mbali yaliyowahi kutolewa na Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika kipindi hiki cha miaka thelathini ni utajiri na amana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo kwa sasa ni kati ya majanga makubwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Hii inatokana na dhambi ambayo imempelekea mwanadamu kubeza tunu msingi za maisha ya mwanadamu, hali ambayo kwa sasa inahitaji toba na wongofu wa kiekolojia.

Umefika wakati wa kujifunga kibwebwe kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kusimama kidete ili kudumisha haki jamii; mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana. Moto ulioteketeza sehemu kubwa ya msitu Ukanda wa Amazonia umesababisha janga la kimataifa na madhara yake yataendelea kuviandama hata vizazi vijavyo. Kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa kiekolojia kwa kubadili mtindo wa maisha kwa kutambua na kuthamini utakatifu wa kazi ya uumbaji! 

Bartolomeo wa kwanza
18 September 2019, 10:09