Vijana wa kizazi kipya nchini Ufaransa wanaendelea kutafakari waraka wa kitume wa Papa Francisko: "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" dira na mwongozo wa Kanisa kwa utume wa Vijana. Vijana wa kizazi kipya nchini Ufaransa wanaendelea kutafakari waraka wa kitume wa Papa Francisko: "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" dira na mwongozo wa Kanisa kwa utume wa Vijana. 

Waraka wa Kitume: Christus vivit: Utume wa Kanisa kwa vijana!

Jumuiya ya Emmanuel Jimbo kuu la Paris, imetumia fursa ya likizo ya kipindi cha kiangazi na kuwakusanya vijana waliobaki mjini humo kwa ajili ya kusali, kutafakari Neno la Mungu, Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa amani na utulivu wa ndani. Umekuwa ni muda wa shuhuda za maisha ya imani na matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Likizo ya Kipindi cha Kiangazi barani Ulaya ni fursa kwa watu wengi kukimbilia milimani na kwenye fukwe za bahari na wale wanaoweza kwenda kutalii nchi za nje, ili kuweza kujichotea tena nguvu ya kupambana na majukumu pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Lakini, kutokana na ukata na hali ngumu ya maisha, si watu wengi wanaoweza kujipatia fursa kama hizi, kumbe, bado kuna idadi kubwa ya vijana wa kizazi kipya wanaojikuta wakiwa wamebaki mijini kama inavyojitokeza huko Paris, nchini Ufaransa. Jumuiya ya Emmanuel Jimbo kuu la Paris, imetumia fursa ya likizo ya kipindi cha kiangazi na kuwakusanya vijana waliobaki mjini humo kwa ajili ya kusali, kutafakari Neno la Mungu, Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa amani na utulivu wa ndani, pasi na haraka wala purukushani za mijini kama ilivyo kawaida. Umekuwa ni muda wa shuhuda za maisha ya imani, matumaini na mapendo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya mintarafu wito na maisha ya kipadre na kitawa; changamoto na ushuhuda katika maeneo ya kazi, shule na vyuo.

Juhudi zote hizi zinasimamiwa na kuratibiwa kwa uwepo wa karibu wa Askofu Yves Le Saux wa Jimbo Katoliki la Le Mans ambaye pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Emmanuel. Kipindi hiki kimekuwa cha manufaa makubwa kwa vijana kwani wamepata pia fursa ya kuweza kushirikishana yale mambo msingi ambayo yamebanishwa katikaWosia wa kitume wa Baba Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, ambao umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”.

Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anakita tafakari yake kwenye Neno la Mungu kuhusu vijana katika Maandiko Matakatifu, yaani: tangu katika Agano la Kale hadi Agano Jipya. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, wengi wa vijana hawa waliishi katika mazingira ambamo kwa kweli vijana walikuwa si mali kitu! Sehemu ya Maandiko ya Matakatifu inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu anaangalia undani wa mtu, anaangalia moyo na wala si mambo ya nje. Kati ya vijana wa Agano la Kale wanaokumbukwa ni Yosefu, Gideoni, Samueli, Mfalme Daudi, Sulemani na Jermia. Maandiko Matakatifu yanamtaja pia Kijana wa Naaman na Ruth. Baba Mtakatifu anavuka kutoka Agano la Kale na kuingia katika Agano Jipya, kwa kumwonesha Kristo Yesu ambaye ni kijana milele yote na anapenda kuwakirimia waja wake moyo wa ujana. Katika maisha na utume wake, Kristo Yesu, hakufurahia sana kuwaona wazee wakiwadharau vijana au kuwatumikisha kinyume cha utu na heshima yao! Aliwaasa daima kuiga mfano wa vijana katika huduma, kwa kutumikia kwa umakini mkubwa.

Kwa Kristo Yesu, umri hakuwa ni mali kitu, jambo la msingi ni jinsi gani mtu alivyoweza kuutumia umri wake! Hakuna sababu ya kwa vijana kusikitika kwa sababu ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kuwa wema na hatimaye, kufungua nyoyo zao, kwa kuishi kitakatifu! Katika Sura ya Pili, Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ni kijana milele yote! Simulizi la maisha ya Yesu pale mjini Nazareti linaonesha ujana wa Yesu, wazazi wale walipomkuta Hekaluni akiwa ameketi katikati ya waalimu akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Huu ni ushuhuda kwamba, Kristo Yesu, katika ujana wake, “alipenda kujichanganya” na vijana wenzake na wala hakuelemewa na upweke hasi. Alijenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na wananchi wengine pale kijijini na wala hakuonekana kuwa ni kijana wa ajabu sana au kijana ambaye alijitenga na wenzake! Yote haya yanapata chimbuko lake katika malezi, makuzi na imani kutoka kwa wazazi wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tunu hizi msingi zinazobubujika kutoka katika undani wa maisha ya Kristo Yesu zinapaswa kumwilishwa katika mchakato wa utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuunganisha pia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili hatimaye, kumwezesha kijana kuishi vyema duniani. Sera na mikakati ya utume kwa vijana, ijielekeze zaidi katika mchakato wa kuwasindikiza na kuwajengea uwezo wa kukutana na wengine, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Kanisa na watu wanaotaka kulizeesha, kwa kulishinikiza libaki katika mambo ya kale; kwa kulidhibiti na kulifanya kushindwa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mwenyezi Mungu aliokoe Kanisa na kishawishi cha kudhani kwamba, Kanisa ni kijana kwa vile limemezwa na malimwengu. Au kwamba, Kanisa linapyaisha kwa vile linataka kuficha ujumbe wake au kuiga mambo kutoka kwa wengine. Kanisa ni kijana kutokana na ukamilifu wake unaofumbatwa katika Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu pamoja na uwepo wa Kristo na nguvu za Roho Mtakatifu kila siku!

Watoto wa Kanisa wanayo haki ya kuwa tofauti, lakini kwa kuwa makini kushuhudia uzuri wa ujana, huduma, usafi, nguvu, msamaha na uaminifu katika wito wa kila mbatizwa; ari na moyo wa sala pamoja na kuendelea kusimama kidete kupigania haki, ustawi na mafao ya wengi; daima kwa kuonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na urafiki wa kijamii. Kanisa lisitumbukie katika kishawishi cha kutafuta usalama kwa kujificha katika malimwengu na kwamba, ni vijana peke yao, wanaoweza kulisaidia Kanisa kubaki katika ujana wake! Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kutojitafuta lenyewe, bali kutoa kipaumbele cha kwanza, ili kumtafakari Kristo Yesu, ili kwa unyenyekevu, Kanisa liweze kutambua mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebisho ya dhati! Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndani ya Kanisa kuna baadhi ya vijana “wanaochefuka” na kusononeshwa sana kutokana na kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, wizi na ufisadi wa mali ya Kanisa; wakleri na watawa ambao hawakuandaliwa vyema ili kutambua mahitaji msingi ya vijana wa kizazi kipya; kiasi hata kushindwa kuwapatia nafasi na dhamana katika maisha na utume wa Jumuiya ya Kikristo pamoja na Kanisa kushindwa kutetea msimamo wa mafundisho na kanuni maadili mbele ya jamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna vijana wanaolitaka Kanisa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini badala ya kuendelea kulaani ulimwengu! Hawataki kuona Kanisa ambalo liko kimya kwa woga au Kanisa ambalo daima linapambana na watu wawili watatu. Vijana wanafurahishwa kuona Kanisa linalonyenyekea na kusikiliza kwa makini katika mwanga wa ukweli na uwazi, ili kutambua zaidi tunu msingi za Injili. Kanisa linapaswa kujiepusha na mtazamo wa mfumo dume unaopingana na haki msingi, utu na heshima ya wanawake. Kanisa linapaswa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanawake, hata kama haliwezi kukubaliana na baadhi ya mambo yanayopiganiwa na wanaharakati wa wanawake! Bikira Maria msichana kutoka Nazareti kwa kukubali kwake kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake, amekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wote wanaothubutu kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anawauliza vijana ikiwa kama wako tayari kuthubutu katika maisha yao kama alivyofanya Bikira Maria? Hata Bikira Maria katika maisha na utume wake, alikumbana na changamoto za maisha, lakini akakubali mpango wa Mungu. Ndani ya Kanisa kuna umati mkubwa wa watakatifu vijana. Hawa ni akina: Sebastiani, Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mtakatifu Giovanna D’Arco; Mwenyeheri Andrea Phu Yen, Mtakatifu Kateri Tekakwitha, Mtakatifu Dominiko Savio, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Mwenyeheri Ceferino Namuncurà. Wengine ni: Pier Giorgio Frassati, Mwenyeheri Marcel Callo na Chiara Badano. Kutoka Barani Afrika kwa msisitizo kuna Mwenyeheri Isidori Bakanja.

Vijana: Paris
21 August 2019, 15:56