Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva: Chombo cha Sheria Kimataifa kinachodhbiti athari za vita. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva: Chombo cha Sheria Kimataifa kinachodhbiti athari za vita. 

Papa: Kumbu kumbu ya Miaka 70: Mkataba wa Kimataifa wa Geneva: Vita & Ugaidi ni udhaifu wa binadamu!

Tarehe 12 Agosti 2019, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva kunako mwaka 1949. Mkataba huu ni chombo cha sheria kimataifa unaodhibiti matumizi ya nguvu wakati wa vita, umuhimu wa kuwalinda raia na wafungwa wakati wa vita. Vita na ugaidi ni kielelezo cha udhaifu mkubwa wa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 11 Agosti 2019 amewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 12 Agosti 2019, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu  ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva kunako mwaka 1949. Mkataba huu ni chombo cha sheria kimataifa unaodhibiti matumizi ya nguvu wakati wa vita, umuhimu wa kuwalinda raia na wafungwa wakati wa vita. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Mkataba wa Kimataifa wa Geneva utazihamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutambua na kuthamini maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu hata katika mazingira ya vita na mapambano ya silaha. Wadau wote wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanaheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na haki ya kimataifa kuhusu utu wa binadamu.

Kwa njia hii, wanatakiwa kuwalinda raia na miundo mbinu ya kiraia hasa hospitali, shule, nyumba za ibada pamoja na kambi za wakimbizi. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko kwa uchungu mkubwa ameonya kwamba,  vita pamoja na vitendo vya kigaidi ni maafa makubwa kwa binadamu. Hizi ni dalili za kushindwa kwa binadamu. Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949 pamoja na itifaki zilizoongezwa baadaye ni chombo cha sheria kimataifa kinachoratibu hali tete wakati wa vita vya nchi kavu kwa kuwalinda raia, kuwahudumia askari waliojeruhiwa pamoja na kuwalinda mateka wa vita. Hii ni sheria inayozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu kimataifa. Mtakataba wa kwanza ulijihusisha na mchakato wa kuwalinda askari waliojeruhiwa vitani. Mkataba wa pili, ukaongezwa ili kuwasaidia askari wa majini waliojeruhiwa vitani na meli zao kuharibiwa.

Mkataba wa tatu ulikusudiwa kwa ajili ya kuwalinda mateka wa vita, kwa kuzingatia athari zilizojitokeza wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kwamba, mateka wa vita watapaswa kuachiwa huru mara tu vita inapokoma. Mkataba wa Nnne unahusu umuhimu wa kuwalinda na kuwasaidia raia wakati wa mapambano ya silaha; kwa kutenga maeneo maalum ambapo raia wanaweza kupata huduma bila upendeleo wowote ule. Kumbe, Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949 umeridhiwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kwamba nchi zote zinawajibika kutekeleza yote yaliyobainishwa kwenye Mkataba huu.

Papa: Mkataba wa Geneva 70
11 August 2019, 10:18