Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho: Tafakari ya Bikira Maria anayemwadhimisha Mungu, Mwokozi wake kwa kuwa amemtendea makuu! Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho: Tafakari ya Bikira Maria anayemwadhimisha Mungu, Mwokozi wake kwa kuwa amemtendea makuu! 

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho: Magnificat

Katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, anawafundisha watu wa Mungu kumwadhimisha Mungu kwa sababu amewatendea mambo makuu. Bikira Maria anawaalika watu kumwadhimisha Mungu kutokana na ukuu, uzuri na wema wake katika maisha yake. Waamini wanahamasishwa katika maisha, kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 1 Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio XII katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho, baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na ukweli kwamba, tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, lakini zaidi katika Mapokeo ya Kanisa na hasa wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kwamba Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho,  kama kielelezo cha Bikira Maria kulala usingizi “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”.

Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni. Haya ndiyo matendo makuu ya Mungu anayowatendea waja wake, kiasi hata cha kuthubutu kumwimbia utenzi wa sifa na shukrani! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 15 Agosti 2019 ametafakari utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” yaani “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu”. Baba Mtakatifu ameamua kukita tafakari yake katika maneno makuu mawili “Magnifica et Esulta”; mambo yanayo onesha ile furaha inayobubujika kutoka katika wa maisha ya Bikira Maria, kwa sababu ya Mungu Mwokozi wake. Baba Mtakatifu ana amini kwamba, hata waamini katika hija ya maisha yao, kuna siku ambayo wamefurahi na kumtukuza Mungu kwa sababu ya habari njema waliyoipokea.

Katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, anawafundisha watu wa Mungu kumwadhimisha Mungu kwa sababu amewatendea mambo makuu. Bikira Maria anawaalika watu kumwadhimisha Mungu kutokana na ukuu, uzuri na wema wake katika maisha yake. Waamini wanahamasishwa katika maisha, kuhakikisha kwamba, wanatafuta mambo makuu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao kwani Yeye peke yake ndiye aliye mkuu vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wanazama katika mambo madogo madogo ya maisha. Haya ni mambo ambayo wakati mwingine hayana mvuto wala mashiko! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu wamezama hadi kutopea huko waliko kwa kuwa na mamuzi mbele, kinyongo, wivu, uadui na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, uchu wa mali na madaraka. Haya yote yanawaonesha watu waliovaa ngozi ya Kondoo, lakini ukweli wa mambo, watu hawa ni sawa na “mbwa mwitu wakali”.

Huu ndio unafiki unaofichika katika maisha ya watu wengi. Katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuinua uso wao, tayari kuangalia “mambo makuu” ambayo Mwenyezi Mungu amemtendea katika maisha. Baba Mtakatifu katika tafakari yake anaendelea kufafanua kwamba, wakati huu Mama Kanisa ana mwadhimisha Mwenyezi Mungu kwa kumpaliza Bikira Maria mbinguni, mwili na roho. Mwenyezi Mungu ameutaza unyonge wa mjakazi wake na kumwezesha kuwa wa kwanza kutunukiwa utukufu. Bikira Maria, kiumbe kama viumbe wengine, anapalizwa mbinguni mwili na roho. Huko mbinguni aliko, Bikira Maria, yuko kama Mama mzazi anayesubiri watoto wake warejee nyumbani kwao. Waamini wanakumbushwa kwamba, huku bondeni kwenye machozi, ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu, wako njiani kuelekea nyumbani kwa Baba milele. Kwa njia ya Bikira Maria, waamini wanaweza kuona hatima ya maisha yao.

Hili ni tukio muhimu sana la imani kwani ndani mwake, waamini wanamwona Bikira Maria aliye palizwa mbinguni, mwili na roho. Huyu ndiye yule Mama aliyethubutu kushiriki katika Fumbo la Pasaka na sasa anashiriki pia utukufu wa Mwanaye mpendwa, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, ndiye Eva mpya na Kristo Yesu ni Adamu Mpya; kielelezo makini cha faraja na matumaini kwa wasafiri ambao bado wako huku bondeni kwenye machozi. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwilina roho ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu, lakini zaidi ni faraja kwa wale wanaoteseka; watu wanaohuzunika kiasi cha kupondeka moyo na hawana tena nguvu ya kuweza kunyanyua uso wao kwa matumaini. Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuondoa wasi wasi na hofu nyoyoni mwao na wala tena hakuna umbali unaoweza kuwatenga kwani mbinguni kuna Mama Bikira Maria anayewasubiri kwa mikono miwili.

Huyu ndiye Bikira Maria, Malkia wa mbingu na Mama wa wote. Kwa hakika anawapenda sana watoto wake, anataka kuwafurahisha na kuwaokoa kwa haraka, kwani anatawakia mema kama ilivyo kwa kila mama. Waamini watambue kwamba, wanayo thamani kubwa machoni pa Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha, changamoto na mwaliko kwa waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria; waendelee kuvutwa na uzuri wake na kamwe wasikubali kutiwa giza na mambo mpito, bali wawe tayari kuthubutu kuambata mambo makuu ya mbinguni. Waamini wahamasike kusali Rozari Takatifu kila wakati na kwa njia hii, watambue kwamba, wanapiga hatua kubwa katika safari ya maisha yao. Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari yake wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria mbinguni mwili na roho, kwa kuwakumbusha waamini kwamba, Bikira Maria ni Mlango wa mbingu, awasaidie, kuangalia kwa furaha na matumaini huko juu mbinguni, mahali ambapo kuna makazi yao halisi.

Papa: Bikira Maria

 

15 August 2019, 16:13