Papa Francisko asema, vyama na mashirika ya kitume ni mbegu ya haradali itakayo zaa matunda ya upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni! Papa Francisko asema, vyama na mashirika ya kitume ni mbegu ya haradali itakayo zaa matunda ya upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni! 

Papa Francisko: Vyama na mashirika ya kitume ni mbegu ya upyaisho wa utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji hii anakazia umuhimu wa Kanisa kutoa kipaumbele kwa watu wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya kijamii; kwani wao ni sawa na mbegu za haradali zitakazo zaa matunda kwa wakati wake. Vyama na mashirika haya ni chachu ya upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Jambo la msingi ni USHUHUDA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu cha “L’irruzione dei Movimenti Popolari. Rerum Novarum dei Nostri Tempi” kilicho haririwa na Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na kupigwa chapa na idara la uchapaji ya Vatican (LEV) anakiri kwamba, vyama na mashirika ya kitume yamekuwa ni chachu muhimu sana katika mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Vyama na mashirika haya yamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ujinga, magonjwa na baa la njaa kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili hasa Amerika ya Kusini. Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini kwa muda wa miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2014, imeendesha semina, mikutano na makongamano mbali mbali huko Amerika ya Kusini.

Kumbe, kitabu hiki ni mkusanyo wa mada na tafakari mbali mbali zilizochambuliwa wakati wa mikutano hii. Baba Mtakatifu katika dibaji hii anakazia umuhimu wa Kanisa kutoa kipaumbele kwa watu wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya kijamii; kwani wao ni sawa na mbegu za haradali zitakazo zaa matunda kwa wakati wake. Vyama na mashirika haya ni chachu ya upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa linapaswa kuwapatia watu hawa uzito wanaostahili, kwa sababu wao ni wakala wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwa sasa na kwa siku za usoni, kwani waswahili wanasema, “Eti yajayo yanapendeza”. Baba Mtakatifu anasema, watu hawa wanaleta mageuzi na upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa katika hali ya amani na utulivu pasi na makelele wala mbwembwe. Kwa hakika vyama na mashirika haya ya kitume ni mfano bora wa kuigwa kwa kumwonesha Kristo Yesu ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.

Baba Mtakatifu anasema, watu hawa wanapaswa kupewa ushirikiano na mshikamano wa kutosha. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, anafahamu baadhi ya vyama na mashirika ya kitume ambayo yana hadhi ya kimataifa. Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anasema watu hawa ni kielelezo cha furaha mpya, furaha ambayo inashirikishwa kwa jirani ili kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa wanadamu pamoja na kuendelea kuboresha maisha ya ndani yanayobubujika kutoka katika Moyo wa Kristo Mfufuka. Vyama na mashirika haya yanaendelea kujenga utamaduni wa watu kukutana, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ni alama ya matumaini kwamba, kila kitu kinaweza kubadilika, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Hawa ni watu ambao kamwe hawawezi kumezwa na malimwengu, uchu wa mali, fedha na madaraka. Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu Francisko, ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto kubwa ya: hofu, woga na wasi wasi; nyanyaso na dhuluma dhidi ya wageni pamoja na aina mbali mbali za ubaguzi unaoendelea kujifunua kwenye uso wa dunia. Vyama na mashirika ya kitume yanaweza kuwa ni chemchemi ya nguvu inayokita mizizi yake katika kanuni maadili na utu wema; kwa kuendelea kupyaisha dhana ya demokrasia katika ulimwengu mamboleo, ili kuganga na kuponya madhara na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Ni vyama vinavyoweza kuwasaidia watu kukuza na kudumisha fadhila ya unyenyekevu badala ya kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko.

Ni vyama na mashirika yanayotoa mwelekeo wa demokrasia shirikishi, kwa kuheshimu na kuthamini uwepo wa jirani zao, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano kwa kuondokana na sera za ubinafsi pamoja na watu kutaka kujitafuta wao wenyewe. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu hiki anafafanua umuhimu wa kazi kama sehemu ya utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Haki msingi, utu na heshima ya wafanyakazi zinapaswa kuheshimiwa na wote. Kuna haja ya kuwa na utu mpya unaofyekelea mbali tabia ya watu kutindikiwa fadhila ya huruma, upendo na mshikamano wa dhati; ili kukuza na kudumisha maendeleo na utamaduni unaothamini: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa: Dibaji
24 August 2019, 14:07