Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufaransa kujenga utu mpya unaosimikwa katika imani kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufaransa kujenga utu mpya unaosimikwa katika imani kwa Kristo Yesu.  (ANSA)

Ajali ya moto: Kanisa kuu la Notre Dame: Jengeni utu mpya katika Kristo Yesu & Kanisa lake.

Papa Francisko kwa maombezi ya Bikira Maria, anapenda kumwomba Mwenyezi Mungu ili ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame, uwe ni kielelezo cha upyaisho wa imani miongoni mwa watu wa Mungu, Jimbo kuu la Paris. Waamini waendelee kuwa ni watu wa matumaini, ili kweli ukarabati wa Kanisa kuu uwe ni alama ya maisha mapya kwa ajili ya ujenzi wa utu mpya katika Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Michel Aupetit wa Jimbo kuu la Paris Ufaransa, wakati Kanisa kuu la Notre Dame, lilipoungua moto hapo tarehe 14 Aprili 2019 alisema kwamba, alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Alisikitika sana kuungua kwa Kanisa kuu la Notre Dame, kielelezo na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa katika umoja na utofauti wao! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, baada ya ukarabati, Kanisa kuu la Notre Dame litaendelea kuwa ni nyumba ya wote, alama ya imani, amana na utajiri wa kihistoria na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni utajiri wa familia ya Mungu nchini Ufaransa, lakini pia ni kwa ajili ya binadamu wote! Kutokana na ajali hii, watu wa Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufaransa, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, hawakuweza kutumia Kanisa la Notre Dame, jambo ambalo limewahuzunisha wengi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anawataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufarasa, kuanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa utu mpya unaokita mizizi yake kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kutokana na ajali ya moto uliosababisha sehemu kubwa ya Kanisa kuu la Notre Dame kuteketea vibaya, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa limeadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kwenye Daraja la “Saint-Louis”, mahali ambapo, kadiri ya Mapokeo ya Jimbo kuu la Paris, pamekuwa pakitumika kwa ajli ya kufanyia maandamano ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni, mwili na roho kuelekea kwenye Kanisa la “Saint-Suplice” ambako Askofu mkuu Michel Aupetit ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Paris, imerudia tena ahadi ya kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kama alivyofanya Mfalme Aloyce tarehe 10 Februari 1638. 

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Anawakumbusha waamini kwamba, Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waja wake wote wanaokimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Bikira Maria anaendelea kushikamana na watoto wake wote wanaopambana huku bondeni kwenye machozi, ili kuwaonjesha ukaribu, upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Bikira Maria anashiriki kikamilifu katika historia ya watu wa Mungu waliopokea Habari Njema ya Wokovu na kuimwilisha, kiasi kwamba, imekuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa historia ya watu husika. Baba Mtakatifu Francisko kwa maombezi ya Bikira Maria, anapenda kumwomba Mwenyezi Mungu ili ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame, uwe ni kielelezo cha upyaisho wa imani miongoni mwa watu wa Mungu, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa. Waamini waendelee kuwa ni watu wa matumaini, ili kweli ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame uwe ni alama kwa ajili ya familia pamoja na jumuiya zao, mahali pa maisha mapya kwa ajili ya ujenzi wa utu unaokita mizizi yake katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, moto ulitikisa alama na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa unaofumbatwa katika umoja na tofauti zao. Kanisa kuu la Notre Dame, ni kito cha thamani, mahali pa watu kukutana katika matukio mbali mbali. Kanisa hili limekuwa ni ushuhuda wa imani na mahali pa sala kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Paris, Ufaransa.

Papa: Paris

 

 

17 August 2019, 13:49