Tafuta

Papa Francisko: Vatican na Poland Mwaka 2019 wanaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu nchi hizi mbili ziliporejesha tena uhusiano wa kidiplomasia. Papa Francisko: Vatican na Poland Mwaka 2019 wanaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu nchi hizi mbili ziliporejesha tena uhusiano wa kidiplomasia. 

Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 100: Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Poland

Kunako mwaka 1971 chini ya uongozi wa Mtakatifu Paulo VI, Vatican na Serikali ya Poland zilifanya marekebisho makubwa na tarehe 28 Julai 1993, Poland na Vatican zikaridhia Mkataba wa makubaliano hayo tarehe 25 Machi 1998. Utekelezaji wake ukaanza tarehe 25 Aprili 1998. Huu ukawa mwanzo wa ukurasa mpya wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, 15 Agosti 2019, aliyaelekeza mawazo yake Jimbo kuu la Czestochowa nchini Poland, ambako umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za Poland ulikuwa umekutanika kwa ajili ya kuadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu Poland iliporejesha tena uhusiano wake wa Kidiplomasia na Vatican. Tukio hili limeadhimishwa huko kwenye Madhabahu ya Jasna Gora na Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatumia salam na matashi mema na kuwasihi kuliombea Kanisa zima! Itakumbukwa kwamba, Vatican na Poland zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia kunako mwaka 1919. Kutokana na sababu msingi, Vatican haikuitambua Serikali ya Umoja wa Kitaifa, iliyoundwa huko Warsaw, Poland tarehe 28 Juni 1945 hadi mwaka 1958, Vatican iliendeleza uhusiano wake na Serikali ya Poland iliyokuwa uhamishoni.

Kunako mwaka 1971 chini ya uongozi wa Mtakatifu Paulo VI, Vatican na Serikali ya Poland zikafanya marekebisho makubwa na tarehe 28 Julai 1993, Poland na Vatican zikaridhia Mkataba wa makubaliano hayo tarehe 25 Machi 1998. Utekelezaji wake ukaanza tarehe 25 Aprili 1998. Huu ukawa mwanzo wa ukurasa mpya wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Poland na hivyo kufutulia mbali uhasama wa kidiplomasia, uliokuwa umedumu kwa takribani miaka 53. Poland ikafungua ubalozi wake mjini Vatican na kwa upande wake, Vatican ikaanzisha ubalozi wake nchini Poland. Hija za kitume zilizofanywa na viongozi wa Kanisa tangu wakati huo sanjari na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni kati ya matukio yaliyo endelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Poland. Waswahili wanasema, usione vinaelea, ujue vimeundwa!

Baba Mtakatifu Francisko,  tarehe 4 Juni 2018 alikutana na kuzungumza na Bwana Mateusz Morawiecki, Waziri mkuu wa Poland pamoja na msafara wake. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili waliridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili; sanjari na ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na Kanisa Katoliki nchini Poland, katika utekelezaji wa huduma makini kwa familia ya Mungu nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake, waligusia tema mbali mbali ikiwa ni pamoja na sera na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kusimama kidete: kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Poland na Vatican, huko Varsavia, Juni, 2014 alikazia zaidi kuhusu uhuru na mshikamano kuwa ni mambo msingi wakati Poland na Vatican zilipokuwa zinaadhimisha Kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 25 tangu nchi hizi mbili zilipoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia.

Mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Poland katika historia ya miaka ya hivi karibuni, ni kielelezo makini cha utashi wa wananchi wa Poland kutaka mabadiliko ya dhati yanayojikita katika uhuru na mashikamano wa kweli, hali iliyopelekea kuanguka kwa ukuta wa Berlin, hapo ukawa ni mwanzo mpya wa maisha ya wananchi wa Poland. Kardinali Pietro Parolin anasema, uhuru wa kidini ni mwendelezo wa mambo msingi katika maisha ya wananchi wa Poland yanayojionesha katika Katiba na Sheria za Kimataifa. Uhuru wa kidini ni jambo ambalo limeendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika mabadiliko yanayojitokeza nchini Poland, ili kuwawezesha watu kujenga misingi ya imani na matumaini thabiti, sanjari na utekelezaji wa demokrasia ya kweli dhidi ya vitendo vya kutovumiliana, ubaguzi na misimamo mikali ya kidini, mambo ambayo yanapaswa kukemewa na kuoneshwa kwamba, hayafai kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Kanisa linaheshimu na kuthamini kazi zinazotekelezwa na Serikali ya Poland na kwamba, ushiriki wake katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Poland unajikita katika uhuru wa kuabudu pamoja na utekelezaji wa haki msingi za binadamu, ili kudumisha amani na utulivu. Utekelezaji wa uhuru wa kuabudu kwa namna ya pekee unahitaji kuongozwa na kanuni auni na mshikamano. Aliwakumbusha waamini kwamba, ushindi wa uhuru wa kidini umepatikana kwa njia ya Msalaba. Kumbe, hakuna sababu ya kuwa na wasi wasi, licha ya ukosefu wa fursa za ajira, tatizo la watu kukimbia nchi yao na watu kutokuwa na uhakika wa maisha yao kwa siku za usoni, mambo ambayo yanayumbisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kardinali Pietro Parolin aliwataka wananchi wa Poland kujiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kwa maombezi yake, Mwenyezi Mungu aendeleee kutekeleza mpango wake kwa ajili ya familia ya binadamu. Mtakatifu Yohane Paulo II anaweza kuitwa kuwa ni msimamizi wa uhuru wa wananchi wa Poland.

Diplomasia: Poland

 

15 August 2019, 15:31