Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasaidia wagonjwa na wale wanaowatunza kwa hali na mali! Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasaidia wagonjwa na wale wanaowatunza kwa hali na mali!  (REMO CASILLI)

Katekesi: Safari ya Injili Duniani: Mshikamano wa Kikristo!

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi amesema kwamba, mshikamano wa umoja na upendo ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa. Waamini wajitahidi kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kuishi katika misingi ya ukweli, uwazi, upendo na mshikamano wa dhati, changamoto makini inayo bubujika kutoka katika Injili. Umoja na mshikamno muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, binti mmoja mzuri, lakini mgonjwa alimwendea na kumwomba baraka. Baba Mtakatifu baada ya katekesi yake, amewaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanapokutana na wagonjwa kama hawa, wawasaidie kwa hali na mali pamoja na kuwaombea, wazazi, ndugu na jamaa wanaoteseka pamoja nao, ili waweze kuwahudumia kwa moyo wa huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Kwa mfano wa Mtakatifu Papa Pio X, anawaalika waamini wote kujiandaa kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya kusikiliza Neno lake ambalo watalimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu ameendelea kufafanua kwamba, mshikamano wa Kikristo ni tofauti kabisa na huduma zinazotolewa kijamii. Mshikamano wa umoja na upendo ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa.

Waamini wajitahidi kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kuishi katika misingi ya ukweli, uwazi, upendo na mshikamano wa dhati, changamoto makini inayo bubujika kutoka katika Injili. Kristo Yesu, atawakirimia Roho wake Mtakatifu, ikiwa kama waamini wako tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao, kama ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa ukarimu wa kidugu, kwa njia ya matendo, kwa kuwasaidia maskini na wale wanaohitaji zaidi: kiroho na kimwili na kwa njia hii, watakuwa wanamsaidia na kumhudumia Kristo Yesu, anayejifunua kati pamoja na ndugu zake maskini. Waamini wamwachie nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao, kwa kuwakirimia nguvu na mapaji yake, yatakayowasaidia kumwilisha Injili ya upendo kwa jirani zao. Upendo kwa Mungu na jirani kamwe usiwe wa kinafiki, Mwenyezi Mungu hapendi wanafiki!

Papa: Ushuhuda
21 August 2019, 14:25