Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, umoja wa Wakristo unafumbatwa katika: Ekaristi Takatifu, Sala, Mafundisho ya Mitume, Upendo na Mshikamano kielelezo cha imani tendaji! Papa Francisko asema, umoja wa Wakristo unafumbatwa katika: Ekaristi Takatifu, Sala, Mafundisho ya Mitume, Upendo na Mshikamano kielelezo cha imani tendaji!  (Vatican Media)

Katekesi: Safari ya Injili Duniani: "Koinonia": Umoja & Upendo

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala, Mafundisho ya Mitume; Umoja, upendo na mshikamano, ni mambo ambayo yanawaunganisha waamini kuwa na moyo mmoja na roho moja, kielelezo na ushuhuda wa ukarimu, ili kuondokana na “mkono wa birika na roho na korosho”. Sala, Tafakari na maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa ya mwilishwe katika matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji. Maandiko Matakatifu yanasema, Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika na katika kuumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na Mitume katika Jina la Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Maajabu na ishara nyingi zilizotendwa na Mitume wa Yesu zilikuwa ni ufunuo wa Umungu wa Kristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume 4: 32 kinaelezea jinsi ambavyo jamii ya watu walioamini walivyokuwa na moyo mmoja na roho moja kiasi kwamba, walikuwa na vitu vyote kishirika na kila mtu akapewa kadiri ya mahitaji yake. Hiki ni kielelezo cha nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu aliyewawezesha Wakristo wa Kanisa la mwanzo kukuza na kudumisha mshikamano ambao ulipania kulijenga Kanisa kama familia ya Mungu inayojikita katika umoja.

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati vinapata chimbuko lake katika ushiriki mkamilifu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu linalowajenga na kuwaimaarisha kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Umoja wa Kanisa uliliwezesha hata kuweza kusikiliza na kujibu shida na mahangaiko ya Kanisa la Yerusalemu pamoja na Makanisa mengine. Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 21 Agosti 2019 kwenye Ukumbi wa Paulo VI, ulioko mjini Vatican. Anasema, wakristo wema ni wale wanaosali, wanaotafakari Neno la Mungu, wanaoshiriki Mafumbo ya Kanisa kwa njia ya toba, wongofu wa ndani pamoja na ukarimu kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama kielelezo cha imani tendaji. Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala, Mafundisho ya Mitume; Umoja, upendo na mshikamano, ni mambo ambayo yanawaunganisha waamini kuwa na moyo mmoja na roho moja, kielelezo na ushuhuda wa ukarimu, ili kuondokana na “mkono wa birika na roho na korosho”.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kitabu cha Matendo ya Mitume, kinashuhudia jinsi ambavyo waamini wa Kanisa la mwanzo waliokuwa na nyumba, viwanja na mashamba wakaviuza na thamani ya vitu vyote hivi wakaiweka miguuni pa Mitume. Wakristo wa Kanisa la mwanzo, licha ya fedha na mali, lakini pia walisadaka rasilimali muda na kuiwekeza katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili: kwa ajili ya wagonjwa na huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Hii ni Jumuiya iliyokita mizizi yake katika “koinonia” yaani “umoja” kati yao kama waamini na umoja na wafuasi wote wa Kristo Yesu, kiasi cha kuwaacha watu wengi wakiwa wanashangazwa na upendo wa dhati uliokuwa kati yao! Kifungo cha upendo, kikawaunganisha wafuasi wa Kristo pamoja na Kristo mwenyewe, kiasi kwamba, waamini waliweza kuchangia hata rasilimali fedha na wala haikuonena kuwa ni mzigo mzito wa “kutwishwa Mnyamwezi”, kwani waliguswa na ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kuguswa na shida, mahangaiko na mateso ya jirani zao, kiasi hata cha kuwa tayari kuwasaidia kwa hali na mali. Wale wenye uwezo wajitahidi kuwasaidia maskini na wanyonge katika jamii, ili kuinua utu, heshima na haki zao msingi kama binadamu. Hiki ndicho kifungo cha upendo katika uhalisia wa maisha! Katika Maandiko Matakatifu, Mitume Yakobo, Petro na Yohane wanabainishwa kuwa nguzo ya Kanisa la Yerusalemu, waliojikita katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mitume Paulo na Barnaba, wao walitakiwa kujikita pia katika huduma kwa maskini: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ukaribu wa Kristo kwa waja wake. Huu ndio ushuhuda wa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Barnaba aliuza shamba lake na fedha iliyopatikana akaikabidhi kwa Mitume, kwa bahati mbaya Anania na Safira wanavuruga na kuvunja kifungo cha upendo kwa kusema uongo na matokeo yake wakakumbana na kifo!

Hawa ni waamini waliokosa uaminifu, ukweli na uwazi; wakataka kuendekeza: unafiki, uchoyo na ubinafsi; kielelezo cha ubaridi na kifo cha maisha ya kiroho. Mwishoni mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu anawaonya Wakristo kutoligeuza Kanisa kuwa ni kama jumba la makumbusho ya kitalii au makatakombe; bali watambue kwamba, wao ni ndugu na wamoja katika Kristo Yesu. Kanisa na viongozi wake, wawe makini na waamini wanafiki wanaotaka kulitumia Kanisa kwa ajili ya faida zao binafsi. Unafiki wa namna hii unalichafua na kuliangamiza Kanisa. Baba Mtakatifu anawaombea waamini wote ili waweze kupata nguvu ya Roho Mtakatifu atakayewajalia: wema, ukarimu na upendo, ili kuvunjilia mbali unafiki, uchoyo na ubinafsi, tayari kuambata na kujikita katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano wa Kikristo, amana, utajiri, kielelezo na utambulisho wa Kanisa, Mama wa wote, lakini zaidi, Mama wa maskini!

Papa: Umoja

 

21 August 2019, 14:39